Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
WAZIRI Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa, ameutaka uongozi wa
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) hapa nchini, kuhakikisha kwamba wanajipanga
kikamilifu katika kuhakikisha kwamba wakulima wa zao la mahindi wanapatiwa magunia
ya kuhifadhia zao hilo, katika maeneo ambayo yametengwa huko vijijini msimu
ujao wa mavuno ya mazao ya chakula.
Agizo hilo amelitoa leo katika ziara yake ya siku tatu ya
kutembelea na kuona maendeleo ya sekta mbalimbali mkoani Ruvuma, na kuhakikisha
kwamba anatekeleza agizo la Rais John Magufuli linalosema hakuna Mtanzania
atakayekufa njaa.
Alieleza kwamba, wafanyabiashara ambao wamekuwa wakipatiwa
magunia na NFRA kwa ajili ya kununulia mahindi na wakulima wanapojaribu
kutafuta namna ya kuyapata magunia hayo, imekuwa ni tatizo kwao kuyapata kwa
urahisi.
Vilevile Waziri Mkuu, Majaliwa alionesha kusikitishwa na vitendo
hivyo vinavyofanywa na wafanyabiashara wajanja, ambao wamekuwa wakipita
vijijini kuwarubuni wakulima na kununua mahindi kwa bei ndogo ambayo hailingani
na uzalishaji wa zao hilo.
Alisema kuwa kumekuwa na mianya ya rushwa inayofanywa na
wafanyabiashara hao kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa Wakala huyo, kwa
lengo la kujinufaisha watu wachache huku mkulima wa kawaida akiendelea kuteseka
na mazao yake shambani, jambo ambalo hivi sasa limekuwa ni kero kubwa hasa
katika maeneo ambayo mazao ya chakula huzalishwa kwa wingi.
“Magunia yanayonunuliwa na serikali kwa ajili ya kuhifadhia
zao hili, ninazo taarifa za kutosha kwamba hayamfikii mkulima kule kijijini,
badala yake yanaishia kwa watu wachache”, alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Vilevile alieleza kuwa serikali inawajibu wa kuhifadhi
chakula katika mazingira yanayokubalika ili kisiweze kuharibiwa na wadudu
waharibifu wa mazao, hivyo ameitaka Wakala wa hifadhi ya taifa ya chakula kanda
ya Songea kuhakikisha kwamba mahindi yaliyohifadhiwa chini ya ardhi
yanatafutiwa sehemu nyingine ya kuhifadhia ili yasiharibike.
Alifafanua kuwa uhifadhi wa nje wa zao hilo, usalama wake ni
mdogo kwa asilimia 75 tu na kwamba mlundikano huo wa magunia yaliyosheheni
mahindi katika hifadhi hiyo ya chakula unasababishwa na hifadhi kuwa na
upungufu mkubwa wa maghala.
Pamoja na mambo mengine, Waziri Mkuu Majaliwa alihoji juu ya msongamano
wa magari aina ya malori yaliyopo kando kando ya barabara ya kutoka Songea
kwenda Mbinga, huku akieleza kuwa hali hiyo imekuwa ikileta malalamiko mengi
kutoka kwa wasafirishaji kuwa magari yanayoingia NFRA kupakia mahindi, huwapatia
watu wanaojulikana kwanza, ndipo huruhusu wengine kitendo ambacho kinaonyesha
kuwa kuna upendeleo.
“Utaratibu unaotumika kuingiza malori hapa kwenu una
malalamiko mengi, taarifa nilizonazo huingiza kwanza mtu anayejulikana, jambo
hili likiendelea linaweza kuleta mtafaruku au matatizo yasiyokuwa ya lazima,
nahitaji tatizo hili liwe mwisho na zingatieni haki na kupanga utaratibu
mzuri”, alisisitiza.
Awali Mbunge wa Jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma, Leonidas
Gama alisema kuwa tatizo la soko la mahindi katika mkoa huo ni kubwa hivyo
ameiomba serikali ya awamu ya tano, iangalie namna ya kutafuta masoko ili
wakulima wadogo waweze kupata fursa ya kuuza mazao yao.
Gama alisisitiza kuwa ni vyema serikali irejeshe utaratibu wa
awali, wa NFRA kununua mahindi vijijini kwa wakulima na kuachana na mfumo wa
kuwatumia mawakala ambao hupita huko na kumkandamiza mkulima, kwa kununua mazao
yao kwa bei ndogo.
No comments:
Post a Comment