Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MAKAMPUNI yanayotumia makaa ya mawe kufua umeme ambao
huendesha viwanda vyao kwa ajili ya kuzalisha bidhaa mbalimbali hapa Tanzania, yametakiwa
kutumia makaa yanayozalishwa hapa nchini na sio kuagiza nchi za nje.
Waziri wa Wizara ya nishati na madini, Profesa Sospeter
Muhongo alitoa agizo hilo jana alipokuwa ametembelea mgodi wa makaa ya mawe
Ngaka uliopo katika kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda, katika ziara yake ya
siku moja wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma.
Profesa Muhongo alifafanua kuwa makampuni hayo yanafanya
hivyo kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru wa ndani, kwa sababu mkaa unaotoka nje
ya nchi wamekuwa hawalipi ushuru au kodi ya aina yoyote ile.
“Tunataka makampuni yanayotumia makaa ya mawe hapa kwetu
yatumie mkaa unaozalishwa hapa nyumbani, malighafi hii tunazalisha kwa wingi na
yana ubora unaokubalika, kwa nini wasitumie mkaa wa kwetu”?, alihoji Profesa
Muhongo.
Kufuatia kuwepo kwa hali hiyo, Profesa Muhongo aliagiza
Wizara yake ifikapo Januari 14 mwaka huu majira ya asubuhi, atafanya kikao na
baadhi ya makampuni yanayotumia makaa ya mawe ambayo waliingia mkataba wa
kutumia mkaa unaozalishwa hapa nchini, ili waweze kutoa ufafanuzi kwa nini
wanaagiza nje ya nchi na kuacha kutumia ya hapa nyumbani.
Alisema kuwa lengo la kufanya mkutano huo ni kujenga
makubaliano ambayo yatafikia muafaka wa kutumia mkaa unaozalishwa hapa kwetu,
na sio kama ilivyo sasa makampuni hayo hufanya hivyo kwa lengo la kukwepa
kulipa ushuru au kodi.
Pamoja na mambo mengine, Waziri Muhongo aliuagiza uongozi wa
mgodi wa makaa ya mawe Ngaka uliopo wilayani Mbinga uhakikishe unashirikiana kwa
karibu na wananchi wanaozunguka mgodi huo, ili kuweza kuondoa malalamiko
yasiyokuwa ya lazima.
Alisisitiza pia suala la ulipaji wa fidia kwa baadhi ya
wananchi ambao waliondolewa katika eneo la mgodi, lifanyiwe kazi haraka na
wahusika wapewe haki zao wanazostahili kupata.
Naye Mkuu wa wilaya hiyo, Senyi Ngaga alipotakiwa kutoa
ufafanuzi juu ya matatizo yaliyopo katika mgodi huo alimweleza Profesa Muhongo
kuwa, tayari hatua husika za upembuzi yakinifu juu ya madai ya wananchi hao
zimeanza kutekelezwa kwa kushirikiana na kampuni ya TANCOAL Energy, ambao ni
wamiliki wa mgodi huo wanaopaswa kulipa fidia wananchi hao.
Ngaga alisema kuwa tayari wananchi 400 walikwisha lipwa fidia
zao kabla ya mradi huo kuanza kufanya kazi na kwamba, waliobakia sasa baada ya
kufanya tathimini ya pili juu ya malipo yao ni watu 350 ambao nao wanatarajia
kulipwa wakati wowote kuanzia sasa.
Mradi huo wa makaa ya mawe unamilikiwa na kampuni
ya ubia ya TANCOAL Energy, ambayo asilimia 30 ya hisa zake zinamilikiwa na
serikali kupitia shirika la maendeleo la Taifa la NDC na asilimia 70 ya hisa
zinamilikiwa na mwekezaji wa kampuni ya Intra Energy.
No comments:
Post a Comment