Monday, January 14, 2013

TUNDURU NA UTEKELEZAJI WA CHANJO YA KUZUIA MAGONJWA VICHOMI NA KUHARA


Na Steven Augustino, 
Tunduru.

WILAYA ya Tunduru mkoani Ruvuma imeanza kutekeleza mpango wa kuwapatia chanjo mpya ya kuzuia ugonjwa vichomi na kuharisha kwa kuwapatia chanjo hiyo jumla ya watoto 12,372 walio chini ya umri wa mwaka mmoja ikiwa ni juhudi ya serikali kupambana na vifo vitokanavyo na magonjwa hayo.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho alisema hayo alipokuwa akizundua chanjo hizo katika ukumbi wa kutolea huduma ya mama na mtoto   hospitali ya serikali ya wilaya hiyo iliyopo mjini hapa.
 
Katika hilo Nalicho aliwahimiza wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao bila kukosa, ili wapatiwe chanjo hizo zikiwa ni juhudi za mapambano dhidi ya magonjwa hayo.

Alisema endapo kutatokea wazazi na walezi kuzembea katika kuzingatia kupeleka watoto wao kupatiwa chanjo ya magonjwa hayo kunaweza kusababisha vifo vingi visivyo vya lazima.


Sunday, January 13, 2013

NAIBU WAZIRI WA MAJI AKIBADILISHANA MAWAZO NA MKUU WA MKOA WA RUVUMA MARA BAADA YA KUMALIZA ZIARA YAKE YA SIKU TANO MKOANI HUMO

Naibu waziri wa maji mhandisi Dkt. Bilinith Mahenge upande wa kulia, akimsikiliza mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu alipokwenda kumtembelea ofisini kwake mara baada ya kumaliza ziara yake ya siku tano mkoani humo.(Picha na Muhidin Amri)


NAIBU WAZIRI WA MAJI AKIKAGUA MASHINE ZA KUSUKUMIA MAJI KATIKA KIJIJI CHA PERAMIHO

Naibu waziri wa maji mhandisi Dkt. Bilinith Mahenge akiangalia mashine za kusukumia maji katika kijiji cha Peramiho.(Picha na Muhidin Amri)

KIONGOZI AKITOA NENO MARA BAADA YA KUKAGUA MRADI WA MAJI

Naibu waziri wa maji mhandisi Dkt. Bilinith Mahenge akizungumza mara baada ya kuona mradi wa maji katika kijiji cha Peramiho A  wilayani Songea mkoani Ruvuma.(Picha na Muhidin Amri)

MKIRIKITI AKITOA TAARIFA YA MAENDELEO KATIKA KIKAO CHA MAJUMUISHO YA ZIARA YA NAIBU WAZIRI WA MAJI



Mkuu wa wilaya ya Songea Josepph Mkirikiti kushoto akitoa taarifa ya maendeleo ya wilaya yake kwa Naibu waziri wa maji mhandisi Dkt. Billinith Mahenge aliyekaa katikati wakati wa majumuisho ya ziara ya waziri huyo mkoani Ruvuma.(Picha na Muhidin Amri)

KIONGOZI AKIELEKEZA JAMBO



Naibu waziri wa maji mhandisi Dkt.  Bilinith Mahenge akielekeza jambo kwa viongozi wa wilaya ya Namtumbo mara baada ya kutembelea chanzo kimojawapo cha maji mjini Namtumbo hivi karibuni.(Picha na Muhidin Amri)

NAMTUMBO WATAKIWA KUWA WABUNIFU KATIKA UJENZI WA MIRADI YA MAJI

Naibu waziri wa maji mhandisi Dkt. Bilinith Mahenge akizungumza na viongozi wa wilaya ya Namtumbo, ambapo aliwataka kuwa wabunifu wa miradi ya maendeleo ikiwemo ya maji badala ya kusubiri misaada kutoka serikalini hali inayozidisha kuongezeka kwa umasikini wa wilaya hiyo. Kushoto ni mkuu wa wilaya hiyo Abdul Lutavi na kulia mkurugenzi wa wilaya  Mohamed Maje.(Picha na Muhidin Amri)

KARIBU NAIBU WAZIRI UZUNGUMZE NA VIONGOZI WA WILAYA YA NAMTUMBO



Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Abdul Lutavi akimkaribisha Naibu waziri wa maji mhandisi Bilinith Mahenge aliyekaa katikati, kwa lengo la kuzungumza na viongozi wa wilaya hiyo. Kulia ni mkurugenzi wa wilaya hiyo Mohamed Maje.(Picha na Muhidin Amri)

NAIBU WAZIRI AKIZUNGUMZA NA WATAALAMU WA MAJI

Naibu waziri wa maji mhandisi Bilinith Mahenge wa kwanza kushoto, akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mji wa mbinga(MBIUWASA) hivi karibuni alipokuwa katika ziara yake wilayani humo.(Picha na Muhidin Amri)

VIONGOZI WA WILAYA YA MBINGA WATAKIWA KUFUATILIA KWA KARIBU UJENZI WA MIRADI YA MAJI AMBAYO INAENDELEA KUJENGWA WILAYANI HUMO



Mkuu wa wilaya Mbinga Senyi Ngaga aliyekaa upande wa kulia, akimsikiliza Naibu waziri wa maji mhandisi Bilinith Mahenge wakati akitoa maagizo kwake juu ya ufuatiliaji wa miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa katika wilaya hiyo.(Picha na Muhidin Amri)

MAHENGE: JENGENI MIRADI YA MAJI KWA VIWANGO VINAVYOKUBALIKA


Naibu waziri wa maji mhandisi Bilinith Mahenge kulia, akisisitiza juu ya wataalamu wa maji kuhakikisha wanajenga miradi hiyo ya maji kwa kiwango bora. Anayeshuhudia upande wa kushoto ni Mbunge wa viti maalum mkoani Ruvuma, Injinia Stella Manyanya.(Picha na Muhidin Amri)

STELLA MANYANYA AKISISITIZA JAMBO KWA NAIBU WAZIRI



Mbunge wa viti maalum mkoani Ruvuma mhandisi Stella Manyanya kushoto akisisitiza jambo kwa Naibu waziri wa maji mhandisi Bilinith Mahenge, wakati waziri huyo alipokuwa katika ziara yake wilayani Nyasa.(Picha na Muhidin Amri)

KIONGOZI AKIPOKEA MAELEZO

Mhandisi wa maji wilaya ya Mbinga Evaristo Ngole kushoto akimfafanulia jambo Naibu waziri wa maji Mhandisi Dkt. Bilinith Mahenge juu ya kukamilika kwa   ujenzi wa tangi la maji na huduma ya   maji katika kijiji cha Ng'ombo wilayani Nyasa, Ruvuma ulivyokamilika ambapo utasaidia kupunguza tatizo kubwa la upatikanaji wa maji katika kijiji hicho.(Picha na Muhidin Amri)

NAIBU WAZIRI WA MAJI AKIKAGUA TANKI LA MAJI AMBALO LIMEJENGWA NA UNDP

Naibu waziri wa maji mhandisi Dkt. Bilinith Mahenge akipanda kukagua tanki la maji safi na salama katika kijiji cha Ng'ombo wilayani Nyasa Ruvuma hivi karibuni akiwa katika ziara yake wilayani humo ya kukagua miradi ya maji ambayo imejengwa kwa msaada wa fedha kutoka shirika la maendeleo la kimataifa UNDP. Tanki hilo limejengwa kwa thamani ya shilingi milioni 298. (Picha na Muhidin Amri)




Saturday, January 12, 2013

AFARIKI DUNIA KUTOKANA NA KUGONGANA NA GARI USO KWA USO

Na Steven Augustino, 
Songea.
 
Mwendesha Pikipiki mkazi wa kijiji cha Lipokela Songea vijijini Issack Gillas(31) amefariki dunia katika ajali mbaya ya kugongana  Pikipiki aliyokuwa akiiendesha na gari lililokuwa likipita barabarani.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Ruvuma Deusdedith Nsemeki alisema, tukio hilo lilitokea Januari 8 mwaka huu katika Barabara ya Songea kwenda Mbinga mkoani humo.
Nsemeki alisema kuwa katika tukio hilo pikipiki hiyo yenye namba za usajiri T. 937 CCA  iligongana uso kwa uso na gari aina ya Toyota Hilux lenye namba za usajili T. 730 AXZ.

Tuesday, January 8, 2013

AUAWA NA MWILI WAKE KUTUPWA MASHAMBANI KUTOKANA NA UGOMVI WA KIMAPENZI


Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKAZI mmoja wa kijiji cha Tinginya tarafa ya Nakapanya wilayani Tunduru, Ruvuma amekutwa mwili wake ukiwa umetupwa katika mashamba ya kijiji hicho, baada ya kuuawa kikatili na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake.

Marehemu ametambuliwa kwa jina la Abdallah Kingunge(35) ambapo kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo walisema, tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Januari 4 mwaka huu.

Walifafanua  kuwa mkasa huo umewasikitisha wengi na kuleta gumzo katika kijiji hicho na kutajwa kuwa huu ni mwanzo mbaya kwao kwa mwaka huu ni sawa na kutia nuksi kwa wanakijiji wa Tinginya ambao daima huishi kwa amani na upendo.

WATOTO MKOANI RUVUMA KUPATIWA CHANJO YA VICHOMI NA KUHARISHA

Na Steven Augustino,
Songea.

ZAIDI ya watoto 53,000 wenye umri chini ya miaka mitano mkoani Ruvuma, wanatarajiwa kupata chanjo mpya ya ugonjwa wa kichomi na kuharisha mkoani humo.

Wakati taarifa za takwimu za magonjwa hayo zikitolewa, zinaonesha  kusababisha watoto takribani 6000 kupoteza maisha kila mwaka na kushika nafasi ya pili na ya tatu kwa kusababisha vifo vingi vya watoto yakitanguliwa na ugonjwa wa Malaria.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu alisema hayo wakati wa uzinduzi wa chanjo hizo za kuzuia ugonjwa wa kichomi na kuharisha, kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ambao umekuwa ukisababisha vifo vingi kwa watoto hao.

Friday, January 4, 2013

TANESCO MBINGA MASWALI MENGI KULIKO MAJIBU

Kassian Nyandindi



















Na Kassian Nyandindi,                                         Uchambuzi.

TATIZO la upatikanaji wa umeme wa uhakika katika mji wa Mbinga, hivi sasa imekuwa ni kero kiasi ambacho wakazi wa mji huo wameanza kulalamikia hali hiyo.

Binafsi nimelichunguza tatizo hili na kubaini  TANESCO kuanzia ngazi ya wilaya hadi huko juu, ni muhimu kuchukua hatua za haraka kunusuru hali hiyo ili isiweze kuendelea na kuleta malalamiko yasiyo ya lazima miongoni mwa jamii.

Ukosefu wa umeme wa uhakika katika mji huu wa Mbinga unatokana na Transfoma yenye ukubwa wa KVA 100 – 11KV kushindwa kufanya kazi yake ipasavyo kwa sababu ya kubebeshwa mzigo mkubwa nje ya uwezo wake.

Transfoma hiyo ndio kiini kikuu ambacho hutegemewa kusambaza nishati hiyo muhimu katika maeneo ya viwanda, mashine za kukobolea nafaka na maeneo mengine ya nyumba za kuishi watu.

WAJUMBE WA ALAT RUVUMA WAKIANGALIA MTARO WA KUPELEKA MAJI SHAMBANI KWA AJILI YA KILIMO CHA MPUNGA



Baadhi ya wajumbe wa ALAT mkoa wa Ruvuma, wakiangalia mtaro mmojawapo katika mradi wa shamba la mpunga Mbamba bay wilayani Nyasa hivi karibuni walipokuwa katika kikao chao kilichofanyika katika mji wa Mbamba bay.(Picha na Muhidin Amri)

AKIFAFANUA JAMBO KWA WAJUMBE WA ALAT MKOA



Mwenyekiti wa kikundi cha  Lwika wilaya ya Nyasa, Mputa Kumburu (kulia) akifafanua jambo hivi karibuni kwa wajumbe wa ALAT mkoa wa Ruvuma, wakati wajumbe hao walipotembelea eneo la kilimo cha Mpunga katika kijiji cha Lundo wilayani humo.(Picha na Muhidin Amri)

ODDO MWISHO AWATAKA WATENDAJI WA SERIKALI KUZINGATIA TARATIBU ZILIZOWEKWA

Mwenyekiti wa Jumuiya ya serikali za mitaa(ALAT) mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho, akizungumza na wajumbe wa jumuiya hiyo hivi karibuni katika  eneo la mradi wa kilimo cha mpunga kijiji cha Lundo wilayani Nyasa, wa pili kulia Mstahiki Meya wa manispaa ya Songea Charles Mhagama wakiwa na wajumbe wengine. Hata hivyo Mwisho alisisitiza kwa kuwataka watendaji wa serikali kuzingatia taratibu zilizowekwa ili miradi ya wananchi iweze kusonga mbele.(Picha na Muhidin Amri)

MKIRIKITI AKIMPA ZAWADI WAKATI WA KUMUAGA MPEMBELE

Mkuu wa wilaya Songea Joseph Mkirikiti kulia akimpa zawadi Mpembele.

RUIMBE AKIZUNGUMZA KATIKA HAFLA YA KUMUAGA MPEMBELE


Mkuu wa chuo cha Veta Songea Gidion Ole Ruimbe akizungumza wakati wa tafrija ya kumuaga aliyekuwa mkuu wa mafunzo wa chuo hicho Timoth Mpembele hayupo pichani, kati kati ni mkuu wa wilaya ya Songea Josepph Mkirikiti na kulia ni mama Mkirikiti.(Picha Muhidin Amri)

MPEMBELE AKIZUNGUMZA KATIKA HAFLA YA KUMUAGA ILIYOFANYIKA MJINI SONGEA

Aliyekuwa mkuu wa mafunzo chuo cha VETA Songea ambaye sasa amehamishiwa mkoa wa Singida Timoth Mpembele, akizungumza wakati wa tafrija fupi ya kumuaga iliyoandaliwa na uongozi wa veta Songea katika ukumbi wa Serengeti Pub mjini Songea, wa pili kushoto mkuu wa chuo hicho Gidion OleRuimbe na wa pili kulia mkuu wa wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti na kulia mama Mkirikiti.(Picha na Muhidin Amri)

ANGUKO LA ELIMU WILAYANI TUNDURU LACHANGIWA NA WAZAZI KUTOZINGATIA MALEZI BORA YA WATOTO WAO


Na Steven Augustino,
Tunduru.
WAZAZI na walezi wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameaswa kushirikiana na serikali kusimamia na kufuatilia   kwa karibu mienendo na maendeleo ya watoto wao hasa wa kike, ikiwa ni juhudi ya kuhakikisha  kuwa  watoto hao wanafanya  vizuri katika masomo yao na kujiletea maendeleo yao.
Ofisa mtendaji wa kata ya Muhuwesi  Shijabu Ngoronje alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa Wadau wa elimu uliofanyika katika Kijiji cha Mhuwesi, ukiwa ni mwendelezo wa juhudi za mradi  wa usimamizi na utetezi wa haki ya mtoto wa kike kupata elimu .
Akifafanua taarifa hiyo Ngoronje alisema, ili kufanikisha adhima hiyo serikali imejipanga kutoa elimu kwa kuwaomba wazazi na walezi kujitoa kuchangia chakula  cha mchana kama kivutio kwa watoto wao na kuwafanya wapende masomo.

Thursday, January 3, 2013

TANESCO MBINGA LAWAMANI


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WAKAZI wa mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wamelilalamikia shirika la ugavi wa umeme Tanzania(TANESCO) tawi  la wilaya ya Mbinga mkoani  humo, kwa kutochukua hatua za haraka kutatua tatizo la upatikanaji wa umeme katika maeneo ya viwanda na mashine ya kukobolea nafaka.

Kero hiyo imekuwa ikijitokeza hata katika majumba ya kuishi watu, ambapo nishati hiyo muhimu imekuwa ikipatikana kwa mgawo na kusababisha adha kubwa kwa watumiaji.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, wakazi wa mji huo walisema kuwa tatizo hilo lilianza kujitokeza Desemba 31 mwaka huu majira ya mchana, huku wakiomba uongozi husika wa shirika hilo kuchukua hatua za makusudi kunusuru hali hiyo.

Thursday, December 20, 2012

KELVIN MAPUNDA: ZINGATIENI ELIMU MNAYOPEWA NA WALIMU WENU

Diwani wa Kata ya Mbinga mjini Kelvin Mapunda(Aliyevaa koti jeusi) akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Mbambi, Mbinga na Nyerere zilizopo katika kata hiyo wakati akiwa katika ziara yake ya kutembelea vituo vya masomo wakati wa likizo vilivyopo katika kata hiyo. Lengo la wanafunzi hao kuwa pamoja katika kituo hicho ni kuwaongezea ujuzi na maarifa katika masomo yao, na huu ni mpango ambao umwekwa na uongozi wa wilaya ya Mbinga, ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi kwa mitihani ya darasa la nne na la saba. Hata hivyo Diwani huyo aliwataka wanafunzi hao kuzingatia masomo yao. Vilevile katika ziara hiyo alitembelea vituo vinne vinavyotumika kufundishia watoto hao katika kata hiyo, ambavyo vipo shule ya msingi Mbinga, Makita sekondari, Lupilisi english medium school na shule ya msingi Mahela.(Picha na Kassian Nyandindi)

AKUTWA NA MAUTI BAADA YA KUIBA MATITA YA NYASI


Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKAZI  wa kijiji cha Tingunya  wilayani Tunduru Ruvuma, anayefahamika kwa jina la Matatizo Mohamedi(27) anashikiliwa na Jeshi la polisi kwa tuhuma za mauaji ya kukusudia katika tukio lililotokea kijijini hapo Desemba 12 mwaka huu.

Kamanda wa polisi wa mkoa huo Deusidedith Nsemeki alisema

kuwa mtuhumiwa huyo  anashikiliwa kwa tuhuma za kumuua kwa kumpiga kichwani kwa kutumia mguu(Tendegu) la kitanda baada ya kutokea ugomvi kati yao.

Kamanda Nsemeki alimtaja aliyefariki dunia katika
  tukio hilo kuwa ni mtu aliyefahamika kwa jina la Maulio Tikiri(14) aliyedaiwa kupigwa na Tendegu hilo Kichwani, na kupoteza maisha muda mfupi baada ya kufikishwa katika kituo cha afya cha Nakapanya kwa matibabu wilayani Tunduru.

KATIBU WA JUMUIYA YA WAZAZI RUVUMA NUSURA AZICHAPE NA KATIBU WAKE WA WILAYA


Na Steven Augustino,
Songea.

KATIBU wa Jumuiya ya wazazi mkoa wa Ruvuma na wa wilaya ya Tunduru mkoani humo, wamenusurika kuchapana makonde, kwa kile kinachodaiwa kutokana na katibu wa jumuiya hiyo kutoka Tunduru, kumpelekea barua ya uhamisho katibu wa jumuiya hiyo mkoani humo.

Katibu wa jumuiya hiyo mkoani humo Lotali Mbawala na katibu huyo wa Tunduru Deogratias Lweyemamu ndio waliotaka kuzua kizaa zaa hicho, baada ya Lweyemamu kudaiwa kumpelekea barua ya uhamisho  Mbawala, kwenda makao makuu ya jumuia ya wazazi taifa.

Kizaa zaa hicho pia kilichoonesha kuwashitua wajumbe wa kamati ya utendaji  ya mkoa, ilifikia hatua kumtaka Mbawala atii taratibu zilizoamriwa na ngazi husika na kumtaka akabidhi ofisi hiyo kwa Lweyemamu ambaye alionesha barua ya uteuzi wake kuwa Kaimu katibu wa jumuiya ya wazazi wa mkoa wa Ruvuma.

Saturday, December 15, 2012

MCB YASISITIZA WATEJA WAKE KUNUNUA HISA KWA WINGI, LENGO KUKUZA MTAJI WA BENKI



 Baadhi ya Wanahisa wa Benki ya wananchi Mbinga (MCB) wakiwa katika picha ya pamoja leo, mara baada ya kufanya mkutano wao maalum wa kujadili namna ya kukuza mtaji wao wa benki, uliofanyika kwenye ukumbi wa Mbiku hoteli Mbinga mjini. (Picha na Kassian Nyandindi)





Na Kassian Nyandindi,


Mbinga.

MWENYEKITI wa bodi ya Benki ya Wananchi Mbinga mkoani Ruvuma(MCB) Altemius Millinga, amewataka wateja wa benki hiyo, kuendelea kununua hisa kwa wingi ili kukuza mtaji wa ndani wa benki.

Hivi sasa benki hiyo tokea ianzishwe mwaka 2003 imeweza kujiendesha na kufikia kuwa na mtaji wa shilingi milioni 347,238.

Rai hiyo ilitolewa leo na Mwenyekiti huyo katika mkutano maalum wa wanahisa wa MCB, ulioketi kwenye ukumbi wa Mbiku hoteli uliopo mjini hapa.

“Ndugu zangu hisa zilizonunuliwa hadi sasa ni 32,555 tu, hizi ni kidogo tunaomba tuongeze juhudi ya kuendelea kuzinunua kwa wingi, ili tufikie malengo yetu tuliyojiwekea na benki iweze kusonga mbele”, alisisitiza.

Millinga alisema mafanikio ya kimaendeleo ya benki ya wananchi Mbinga hayawezi kusonga mbele, kama Wanahisa hawatakuwa tayari kununua hisa kwa wingi ambazo zitaifanya benki iweze kukuza mtaji wake wa ndani.

Thursday, December 13, 2012

KUSHINDWA KUTOA TAARIFA YA MAENDELEO YA WANANCHI NI ISHARA GANI ?

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu.




















Na Kassian Nyandindi,                         Uchambuzi.              

NIMEKUWA nikitafakari kwa kina juu ya tukio lililojitokeza siku kadhaa zilizopita katika ziara ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, iliyofanyika hapa wilayani Mbinga na Nyasa mkoani humo.

Tafakari zangu zinaenda sambamba na mkuu wa mkoa huo Said Mwambungu kuwajia juu viongozi wa wilaya hizo, baada ya kushindwa kumuandalia taarifa iliyo katika misingi ya upembuzi yakinifu.

Binafsi namuunga mkono Mwambungu, kwa kuligundua hili mapema na sitakosea nikisema hivi sasa Taifa hili linahitaji viongozi walio makini kama yeye na wenye kupembua mambo kwa haraka, ili tuweze kusonga mbele kimaendeleo.

Tuesday, December 11, 2012

UONGOZI WA WILAYA YA MBINGA NA NYASA LAWAMANI, NI BAADA YA MKUU WA MKOA WA RUVUMA KUIKATAA TAARIFA YA MAENDELEO YA WILAYA HIZO

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma(Kushoto) Said Mwambungu, akiwa katika ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga leo, majira ya saa 3:15 asubuhi wakati alipokuwa akiikataa taarifa ya maendeleo ya wilaya ya Nyasa na Mbinga kutokana na kutoandaliwa kwa misingi ya upembuzi yakinifu. Upande wa kulia aliyevaa suti nyeusi ni mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga na kati kati ni mkuu wa wilaya ya Nyasa Ernest Kahindi.(Picha na Kassian Nyandindi)

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.


MKUU wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, amewajia juu viongozi wa wilaya ya Nyasa na Mbinga kwa kushindwa kuandaa taarifa sahihi za maendeleo ya wilaya hizo.



Sambamba na hilo mkuu huyo wa mkoa amekataa kupokea taarifa ya maendeleo ya wilaya hizo leo, wakati alipokuwa katika ziara yake ya siku nne ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kitendo cha mkuu huyo wa mkoa kukataa taarifa hizo kilijitokeza katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Mbinga, baada ya kusomewa na ofisa mipango wa wilaya hiyo, Seleman Mwamba na kuwapa muda wa nusu saa kuandaa taarifa nyingine kabla hajaanza ziara yake rasmi.

Sunday, December 9, 2012

MATANKI HAYA YANATUMIKA KUSAFIRISHIA UDONGO WENYE URANI

Baadhi ya waandishi wa habari wa mkoa wa Ruvuma(Pichani) wakimsikiliza Mjiolojia mkuu wa Mantra Tanzania, Emmanuely Nyamsika, wakati alipokuwa akitoa maelezo juu ya matanki yanayotumika kusafirishia udongo wenye madini ya Uran kwa kutumia ndege aina ya Helkopta kwa ajili ya kwenda kufanyiwa utafiti katika maabara zilizopo Mwanza hapa nchini na nje ya nchi za Australia, Afrika Kusini na Uingereza. Baada ya kufanyiwa utafiti udongo huo wenye madini hurejeshwa tena katika eneo hilo la utafiti wilayani Namtumbo. (Picha na Kassian Nyandindi)

HII NI RAMANI HALISI INAYOONESHA ENEO LA MRADI



Waandishi wa habari wa mkoa wa Ruvuma na wataalamu wa Mantra Tanzania, wakiwa wameizunguka ramani(Iliyowekwa chini) ambayo inaonesha eneo halisi linalofanyiwa utafiti na litakalochimbwa madini hayo mara baada ya serikali kutoa kibali chake.(Picha na Kassian Nyandindi)

HIVI NDIVYO TUNAVYOCHORONGA MADINI YA URANI



Waandishi wa habari wakipokea maelezo kutoka kwa mjiolojia mkuu wa Mantra Tanzania Emmanuely Nyamsika, namna madini ya Urani yanavyochorongwa na kuhidhiwa katika mifuko maalum.(Picha na Kassian Nyandindi)

MADINI YA URANI NAMTUMBO BADO HAYAJAANZA KUCHIMBWA WATANZANIA TUSIPOTOSHWE

Madini ya Urani yakionekana kujitokeza juu ya ardhi katika eneo la mto Mkuju hifadhi ya Selous, wilayani Namtumbo.(Picha na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.

UVUMI na kauli zilizokuwa zikielezwa na watu mbalimbali kwamba kazi ya uchimbaji wa madini aina ya Urani katika mto Mkuju uliopo pori la hifadhi ya Selous, wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma kwamba umeanza sio kweli, badala yake kinachofanyika ni kukamilisha kazi ya utafiti wa madini hayo.

Waandishi wa habari wa wa mkoa huo wamefanya ziara maalumu ya kutembelea mradi wa mto huo ambako kampuni ya Mantra Tanzania inatarajia kuanza ujenzi wa mgodi wa madini hayo.

Kauli zinazotolewa na watu mbalimbali ambapo wamekua wakidai mradi huo haufai kwa kuwa unahatarisha maisha ya binadamu kutokana na athari za mionzi na uharibifu wa mazingira.

MJIOLOJIA: ENEO MOJAWAPO LILILOFANYIWA UTAFITI HILI HAPA

 


Waandishi wa habari wa mkoa wa Ruvuma, wakiwa pamoja na baadhi ya wataalamu wa kampuni ya Mantra Tanzania, katika eneo mojawapo ambalo utafiti unafanyika kwa kuchukuliwa udongo wenye madini ya Urani.(Picha na Kassian Nyandindi)

NYAMSIKA: ENEO LILE NDILO LITAKALOCHIMBWA URANI

Waandishi wa habari wa mkoa wa Ruvuma, wakioneshwa eneo la mto Mkuju ambalo hapo baadaye mara baada ya serikali kutoa kibali cha kuruhusu kuchimba madini hayo, yataanza kuchimbwa. Anayeonesha kwa mkono ni Mjiolojia mkuu wa kampuni ya Mantra Tanzania, Emmanuel Nyamsika. Waandishi hao walifanya ziara hiyo leo ili kujiridhisha juu ya uvumi uliojitokeza kuwa madini hayo yameanza kuchimbwa lakini imebainika kwamba kazi ya uchimbaji bado haijaanza kutokana na serikali bado haijatoa kibali cha kuruhusu kazi hiyo kuanza kufanyika.

WAANDISHI WA HABARI RUVUMA NA UTAFITI WA MADINI YA URANI NAMTUMBO

Mjiolojia mkuu wa kampuni ya Mantra Tanzania, upande wa kushoto anayezungumza, Emmanuely Nyamsika akiwapa maelezo waandishi wa habari wa mkoa wa Ruvuma juu ya mapipa yanayotumika kusafirishia URANI kwenda katika maabara za kufanyia utafiti zilizopo Jijini Mwanza na nchi za Afrika Kusini, Australia na Uingereza.Waandishi hao walitembelea leo katika eneo ambalo utafiti huo unafanyika mto Mkuju wilayani Namtumbo mkoani humo. (Picha na Kassian Nyandindi).

MTUHUMIWA WA MAUAJI AACHIWA HURU



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MAHAKAMA Kuu kanda ya Songea mkoani Ruvuma kupitia vikao vyake vinavyoendelea wilayani Tunduru, imemuachilia huru Suzana Kapinga(28) aliyekuwa anakabiliwa na shauri  namba Rm11/2012 la mauaji ya kukusudia, kinyume cha sheria kifungu namba 196 sura ya 16 cha kanuni ya adhabu.

Pamoja na kumuachilia huru pia mahakama hiyo imetoa masharti ya kuomba mtuhumiwa huyo kuwa chini ya uangalizi wa maafisa tabibu wa magonjwa ya akili katika hospitali iliyopo Gereza la ISANGA mjini Dodoma.

Akifafanua hukumu hiyo msajili wa mahakama Kuu mwenye mamlaka ya kijaji Wilifred Peter Ndyansobera alisema kuwa, maamuzi hayo yaliyofanyika na mahakama hiyo imebaini na kuzingatia taarifa iliyotolewa na Daktari wa hospitali ya Milembe, alikopelekwa kwa ajili ya uchunguzi kubaini kuwa pamoja na  mtuhumiwa huyo kutenda kosa hilo la mauaji hayo lakini mtuhumiwa huyo hakuwa amedhamiria kufanya kosa hilo.

ACHOMWA MOTO NA KUFARIKI DUNIA BAADA YA KUIBA SIMU

 






Picha ya marahemu aliyeiba simu na mwili wake kuchomwa moto na kutupwa porini kijiji cha Mbesa wilayani Tunduru.(Picha na Steven Augustino)










Na Steven Augustino,
Tunduru.

Mkazi wa Kijiji cha Mbesa wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, aliyejulikana kwa jina la Seif Jaffari(18) ameuawa kikatili na wananchi wenye hasira kali baada ya kumtuhumu ameiba simu.

Mauaji hayo ya kinyama yalifuatia na kipigo kikali alichokipata na wananchi hao walimchoma moto na mwili wake kuteketezwa kwa porini.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa kabla ya kifo hicho marehemu akiwa na wenzake waliiba simu 6 ambazo zilikuwa zikichajiwa katika nyumba ya Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Chikomo aliyefahamika kwa jina moja la Mwl. Komba iliyopo kijijini humo.

Thursday, December 6, 2012

TUACHENI TUPATE MVINYO, TUKIFURAHIA NDOA YETU





Pascal Mwabesa na mkewe wakinyweshana kinywaji, wakati wakiwa ukumbini (UVIKAMBI) kusherehekea ndoa yao.(Picha na Muhidin Amri)

TUPO KATIKA POZI TUKIFURAHIA NDOA YETU


 
 
 
 
 
Pascal Mwabesa akiwa na mkewe katika pozi mara baada ya kufunga pingu zao za maisha. (Picha na Muhidin Amri)

TUPO NA WAPAMBE WETU


 
 
 
Pascal Mwabesa na mkewe wakiwa katika viwanja vya kanisa la mtakatifu Alois Gonzaga, mara baada ya kufunga ndoa yao huku wakisindikizwa na wapambe wao.(Picha na Muhidin Amri)

TUNAONESHA PETE ZETU, HII NI ISHARA YA UPENDO




Maharusi Pascal Mwabesa na mkewe Gonzalva Lupogo wakionesha pete zao za ndoa kwa ndugu na jamaa waliofika kushuhudia ndoa yao katika kanisa la Mtakatifu Alois Gonzaga mjini Mbinga.(Picha na Muhidin Amri)

WAKIVISHANA PETE KATIKA TUKIO LA KUFUNGA NDOA





Pascal Mwabesa akimvalisha pete ya ndoa mkewe Gonzolva Lupogo wakati wa ndoa yao katika kanisa la Mtakatifu Alois Gonzaga mjini Mbinga juzi.(Picha na Muhidin Amri)

ZIARA YA WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA


Waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa Shamshi Vuai Nahodha akiangalia vyakula vinavyopikwa na askari wakiwa vitani, wakati alipotembelea kambi ya mazoezi ya vikosi vya jeshi kutoka brigedi ya 401 kv Songea juzi wilayani Namtumbo. Kulia ni mkuu wa kikosi cha 411 Meja Yahaya Chausi.(Picha na Muhidin Amri)

Wednesday, December 5, 2012

MBINGA: SHULE YAFUNDISHA WANAFUNZI BILA KUSAJILIWA

Wanafunzi wa shule ya msingi Twiga Mbinga, wakipata kifungua kinywa.


















Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WATOTO hawa(Pichani) ni wanafunzi wa shule ya msingi Twiga iliyopo mtaa wa Mapera, kata ya Mbinga mjini mkoani Ruvuma, kama walivyokutwa na kamera yetu. 

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa shule hiyo inafundisha watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu. Lakini shule haijasajiliwa rasmi na kupewa kibali na serikali kuendesha masomo ya shule ya msingi.

Pamoja na serikali kupitia wizara yake husika kukemea shule kama hizi ziache kutoa huduma mpaka zipewe usajili, hali hiyo imekuwa kinyume katika shule hiyo na hii inaonesha ni ukiukwaji wa taratibu na sheria zilizowekwa. 

Hivyo tunashauri viongozi husika wa wilaya ya Mbinga, kuchukua hatua za haraka kunusuru hali hiyo kabla viongozi wengine kutoka ngazi ya taifa wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi, kuchukua hatua juu ya tatizo hili. 

Ofisi ya Mkurugenzi mtendaji na Mkuu wa wilaya ya Mbinga tunahitaji suala hili lifanyiwe kazi ili kusaidia watoto hawa waweze kupata elimu bora na sio kama ilivyo sasa, ukizingatia kwamba shule hiyo hata haina vifaa vya kutosha katika kukidhi mahitaji muhimu ya mwanafunzi anapokuwa darasani.

Cha kushangaza shule hii ina miaka mitano sasa, ikiendelea kutoa huduma hiyo bila kusajiliwa, Je viongozi tupo makini hapo katika kutekeleza majukumu yetu?


WANAOWAPA MIMBA WANAFUNZI KUKIONA CHA MOTO

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu.
















Na Steven Augustino,
Songea.

SERIKALI mkoani Ruvuma imeamua kuanzisha kampeni maalumu ya kukabiliana na wahusika wa vitendo vya kuwapa mamba wanafunzi kwa kutoa agizo kwa viongozi wa wilaya na halmashauri zote zilizopo mkoani humo.

Hizo ni juhudi zake kuhakikisha kuwa inakomesha wimbi kubwa la upataji wa mimba kwa watoto wakike wanaosoma katika shule za msingi na sekondari.

Kampeni hiyo inawahamasisha wananchi kuwabaini wanaume ambao wamekuwa wakiwashawishi watoto wa kike  na kuwaharibia mfumo wa masomo na maisha   yao.

Hayo yalisemwa na mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu alipokuwa akizungumza katika kikao cha kamati ya ushauri cha mkoa wa Ruvuma, kilichoketi hivi karibuni katika ukumbi wa Songea Club mjini hapa, ambapo pamoja na mambo mengine aliwaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi watendaji wa halmashauri pamoja na viongozi wengine kuhakikisha wanaweka mikakati ya kukabiliana na tatizo hilo ambalo linazidi kuongezeka siku hadi siku mkoani humo.

ATEKETEZWA KWA MOTO AKITUHUMIWA KUIBA SIMU


Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKAZI mmoja wa kijiji cha Mbesa wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma ameuwawa kikatili, na wananchi wenye hasira kali na mwili wake kuuteketeza kwa kuchomwa moto.

Aliyefanyiwa kitendo hicho cha kinyama ni Seif Jafari(18) baada ya kumtuhumu ameiba simu.
Kabla ya mauaji hayo wananchi hao walimuangushia kipigo kikali  na kwamba
akiwa na wenzake wanadaiwa kuiba simu 6 ambazo zilikuwa zikichajiwa katika nyumba ya mwalimu mkuu wa shule ya msingi Chikomo aliyefahamika kwa jina moja la Mwl. Komba.

AFARIKI DUNIA BAADA YA KUNYWA GONGO


Na Mwandishi maalum,
Tunduru.

MTU mmoja mkazi wa Tunduru mjini mkoani Ruvuma, amefariki dunia wakati akiendesha mkokoteni ambao huutumia kubebea mizigo ya aina mbalimbali ya wateja wake, baada ya kunywa pombe haramu aina ya gongo.

Aliyefariki hufahamika kwa jina la Rashid Mpembu kwa jina maarufu “Wamunyama”(43) ambapo kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mashuhuda wa tukio hilo, walisema kuwa Mpembu alianguka ghafla na kupoteza maisha wakati akisukuma mkokoteni huo.

Walisema tukio hilo lilitokea wakati akiwa amebeba viroba viwili vya mahindi ambayo inadaiwa kuwa alikuwa akiwapelekea wateja wake, kukoboa na kusaga katika mashine mojawapo mjini Tunduru.

ASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA MAUAJI


Na Mwandishi wetu,
Tunduru.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma limechukua hatua ya kumshikilia dereva wa kampuni “Progressive Higleig Jv Contractors”, inayojenga mradi wa barabara ambao kwa sasa unaosuasua wa kwa kiwango cha lami Kutoka wilaya ya Namtumbo hadi Tunduru, anayefahamika kwa jina la Philip Chigana kwa tuhuma za kusababisha mauaji.
Kamanda wa polisi wa mkoa huo Deusdedith Nsemeki alisema hayo kwa waandishi wa habari na kuongeza kuwa katika tukio hilo pia dereva huyo alimgonga mtoto wa miaka 12 na kumjeruhi vibaya.
Akifafanua taarifa hiyo alisema kuwa ajali hiyo ilitokea katika kijiji cha Mletele Manispaa ya Songea na kuongeza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi.

Monday, December 3, 2012

POLISI RUVUMA KUFUKUA KABURI ALILOZIKWA KICHANGA


Na Steven Augustino,
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma limeahidi kuomba Kibali cha Mahakama ili waweze kufukua kaburi linalodaiwa kuzikwa kitoto kichanga kwa kile kinachoelezwa, kunyimwa na kuzikwa na mama yake Jenister Mapunda (24).

Kuwepo kwa mkanganyiko wa hapa na pale unaoendelea kuzua maneno na taarifa tofauti na kuwachanganya wananchi, ndiko kunakolifanya jeshi hilo kufikia hatua hiyo.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Deusdedith Nsemeki alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika mahojiano maalumu, na kuongeza kuwa uchunguzi huo pekee ndio utakao ondoa utata na maneno yalityopo sasa.

KAHINDI: JENGENI MIUNDO MBINU RAFIKI YA WALEMAVU

 Mkuu wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma Ernest Kahindi, akihutubia wananchi(Hawapo pichani) waliohudhuria siku ya maadhimisho ya walemavu duniani yaliyoadhimishwa kiwilaya, wilayani Mbinga, Mbinga mjini. Katikati ni Mwenyekiti wa walemavu wa wilaya hiyo Martin Mbawala na kulia kwake ni Diwani wa kata ya Mbinga mjini Kelvin Mapunda. Katika hotuba yake Kahindi aliwataka wataalamu wa serikali na jamii kwa ujumla kujenga(majengo) miundo mbinu rafiki na mazingira ya walemavu ili waweze kuitumia kwa urahisi kulingana na maumbile yao. (Picha na Kassian Nyandindi)

NAKABIDHI SHAIRI LANGU KWA KIONGOZI

Mlemavu wa ngozi(Albino) Dada Shukrani Ndunguru (kulia) akikabidhi shairi lake alilomaliza kuimba siku ya walemavu iliyoadhimishwa kiwilaya Mbinga mjini, kwa mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya ya Nyasa Ernest Kahindi. Anayeshuhudia kulia kwa mgeni rasmi ni mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga. Shairi hilo lilisheheni ujumbe ambao ukiitaka jamii na serikali kwa ujumla kuwajali watu wenye ulemavu na sio kuwabagua katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.(Picha na Kassian Nyandindi)

VIONGOZI WAKIBADILISHANA MAWAZO




 Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga(aliyenyosha mkono) na wa Nyasa Ernest Kahindi (Katikati) wakibadilishana mawazo katika sherehe za maadhimisho siku ya walemavu duniani, zilizofanyika kiwilaya Mbinga mjini. (Picha na Kassian Nyandindi)

AKINA MAMA NA SIKU YA WALEMAVU MBINGA



 Akina mama wa mtaa wa Matarawe Mbinga mjini mkoani Ruvuma, wakicheza kwa pamoja na kufurahia sherehe za maadhimisho ya walemavu zilizofanyika kiwilaya wilayani Mbinga, mjini hapa mbele ya mgeni rasmi Ernest Kahindi (Hayupo pichani, Picha na Kassian Nyandindi)

WAKUBWA WAKITAFAKARI



Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga na wa Nyasa Ernest Kahindi, wakifuatilia kwa pamoja matukio ya michezo mbalimbali(Haipo pichani) iliyokuwa ikichezwa katika siku ya maadhimisho ya walemavu yaliyofanyika Kiwilaya Mbinga mjini. (Picha Kassian Nyandindi)

WATOTO NA SIKU YA WALEMAVU



Watoto walemavu(Albino) na wasiokuwa walemavu, wakicheza kwa pamoja kusherehekea sherehe za maadhimisho ya siku ya walemavu zilizofanyika Mbinga mjini, mkoani Ruvuma mbele ya mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Nyasa Ernest Kahindi. (Hayupo pichani). (Picha na Kassian Nyandindi)

DIWANI AKIFURAHIA SIKU YA WALEMAVU




Diwani wa Kata ya Mbinga mjini mkoani Ruvuma, Kelvin Mapunda (kulia) akisakata dansi wakati wa sherehe za maadhimisho ya siku ya walemavu duniani yaliyoadhimishwa kiwilaya mjini hapa. (Picha na Kassian Nyandindi)

SHEREHE YA WALEMAVU MBINGA

 Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Senyi Ngaga, (kushoto) akimkaribisha Mkuu wa wilaya ya Nyasa Ernest Kahindi aliyekaa ambaye amevaa taji, katika sherehe za kilele cha maadhimisho siku ya walemavu duniani kwa wilaya ya Mbinga yalifanyika mjini hapa na mgeni rasmi alikuwa mkuu wa wilaya hiyo ya Nyasa. Kulia ni Mwenyekiti wa Walemavu wa wilaya ya Mbinga Martin Mbawala. (Picha na Kassian Nyandindi)

UCHAFU: TASWIRA KATIKA JAMII


 Watoto hawa huku hawajui wakihatarisha afya zao, walikutwa na kamera yetukatika mtaa wa KKKT Mbinga mjini mkoani Ruvuma, wakiwa wanacheza na kuzunguka katika ghuba ambalo taka na uchafu wa aina mbalimbali humwagwa hapo. Ni vyema wazazi tuwaelimishe watoto wetu waache kucheza katika maeneo machafu kama haya.