| Hivi ndivyo ilivyo katika chanzo cha maji Kigonsera ambako maji yametegwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu, hali ni mbaya hatua husika zinapaswa kuchukuliwa mapema.(Picha na Gwiji la matukio Ruvuma) |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
AFYA
za wakazi wa kijiji cha Kigonsera kata ya Kigonsera wilayani Mbinga mkoa wa
Ruvuma, zipo mashakani kutokana na maji wanayotumia kwa ajili ya kuendeshea
maisha yao ya kila siku kuwa machafu na kutofaa kwa matumizi ya binadamu.
Hali
hiyo imesababisha wakazi hao kutoa tamko na kutishia kwamba siku ya ujio wa
Rais Jakaya Kikwete, katika ziara ambayo anatarajia kuifanya hivi karibuni katika
kipindi cha mwezi Mei mwaka huu mkoani humo hususani katika wilaya ya Mbinga,
wapo tayari kulala barabarani kwa lengo la kushinikiza msafara huo usimame ili
waweze kutoa kilio chao kwa kiongozi huyo wa kitaifa na kiweze kufanyiwa kazi
haraka.
Walisema
kufanya hivyo kunatokana na uongozi wa wilaya hiyo kuwa na kasi ndogo, ya
uchukuaji wa hatua za kuwahamisha watu waharibifu katika eneo ambako chanzo cha
maji kimejengwa na kugharimu mradi mzima wa maji uliosambazwa kijijini hapo
kufikia shilingi milioni 479 kwa ufadhili wa benki ya dunia.

