Tuesday, June 24, 2014

MGOGORO WA MIPAKA NA ARDHI: MKUU WA WILAYA YA NYASA MKOANI RUVUMA ALALAMIKIWA NA WANANCHI WAKE


 
Mkuu wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma Ernest Kahindi, akiwa ofisini kwake wilayani humo. (Picha na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

SAKATA la mgogoro wa kugombea ardhi na mipaka katika kitongoji cha Mshangano kijiji cha Liparamba tarafa ya Mpepo wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, limechukua sura mpya kufuatia Wakazi wa maeneo hayo kumlalamikia Mkuu wa wilaya hiyo Ernest Kahindi huku wakimnyoshea kidole kwamba ameshindwa kumaliza mgogoro huo kwa kufuata taratibu husika  ikiwemo ridhaa ya wananchi, badala yake  anatumia nguvu kubwa  kunyanyasa viongozi wa kijiji hicho.  

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati  tofauti kijijini hapo, wakazi hao walisema Kahindi amefikia hata hatua ya kumweka mahabusu kwa siku tatu katika kituo kikuu cha polisi wilaya ya Nyasa, Mwenyekiti wa kijiji Joseph Komba bila kosa lolote huku akizuia dhamana.

Uchunguzi umebaini kuwa Mwenyekiti huyo aliwekwa mahabusu kuanzia siku ya Ijumaa Juni 20 na kudhaminiwa Juni 23 mwaka huu majira ya jioni, ambapo kufikia saa 11 jioni siku hiyo ndipo alichukuliwa maelezo na kuambiwa atafute mtu wa kumdhamini huku akipewa usumbufu wa kuendelea kuripoti kila siku katika kituo hicho cha polisi.

Wednesday, June 11, 2014

KASI YA UPIMAJI VVU MBINGA NI NDOGO BULEMBO AUTAKA UONGOZI WA WILAYA KUHAMASISHA WANANCHI


Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Alhaj Abdallah Bulembo, akipokea vazi na kadi ya chama cha upinzani kutoka kwa mama Maria Ndimbo ambaye alikuwa mfuasi wa Chama Cha Wananchi (CUF) na kuhamia CCM. Tukio hilo lilifanyika katika uwanja wa soko kuu mjini hapa.

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Alhaj Abdallah Bulembo, amemwagiza Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga kuhakikisha kwamba wilaya hiyo inaweka mikakati madhubuti ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao.

Agizo hilo lilifuatia baada ya kusomewa taarifa ya maendeleo ya wilaya hiyo katika ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, ambayo ilionesha kwamba watu 300,000 tu ndio waliopima afya zao katika kipindi cha mwaka 2013 hadi mwaka huu, ili waweze kujitambua kama wana maambukizi ya virusi vya ukimwi kiasi ambacho ni kidogo kutokana na wilaya hiyo kuwa na watu wengi.

“Nimegundua hapa hamasa ya upimaji VVU ni ndogo ukizingatia kwamba Mbinga kuna watu wengi sana, kuanzia sasa tengenezeni hili liwe kama agenda katika vikao vyenu sio tuna kaa kimya tuweke mazingira ambayo yenye programu ya muda mrefu na endelevu”, alisema Bulembo.

Tuesday, June 10, 2014

CHADEMA YAPATA PIGO MBINGA WASEMA NI CHAMA AMBACHO HAKINA MWELEKEO

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Alhaj Abdallah Bullembo akihutubia leo mamia ya wakazi wa Mbinga mjini katika uwanja wa soko kuu mjini hapa.

Alhaj Abdallah Bulembo akimkabidhi kadi ya CCM aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Desderius Haulle katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini hapa, baada ya kurejesha kadi ya CHADEMA.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Desderius Haulle akiwa amebebwa na Wafuasi wa CCM baada ya kurejesha kadi ya chama hicho pinzani na kuhamia chama tawala. (Picha zote na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepata pigo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kufuatia aliyekuwa Mwenyekiti wake wa chama hicho wilayani humo Desderius Haulle kujitoa uanachama na kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tukio hilo limejitokeza leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa soko kuu uliopo mjini hapa, ambao ulikuwa ukihutubiwa na Mwenyekiti wa taifa wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi Alhaj Abdallah Bulembo.

Sambamba na hilo katika mkutano huo pia alijitokeza mwanachama mmoja wa Chama Cha wananchi CUF, Maria Ndimbo naye alirejesha kadi yake ya chama hicho na kuhamia CCM.

Haulle alirudisha kadi ya CHADEMA na kukabidhiwa ya CCM, ambapo alipopewa nafasi ya kuzungumza alisema amechoshwa na sera za chama hicho pinzani ambazo hazina utekelezaji.

“Leo nimeamua kurejesha kadi hii na kuhamia katika chama hiki tawala kwa sababu nafahamu mambo mengi yanayofanywa na CHADEMA, hivyo nilivumilia kwa muda mrefu lakini leo imefikia mwisho wake naomba tuungane pamoja tujenge taifa letu”, alisema Haulle.

UNYAMA WA KUTISHA: WATOTO WATEKETEA KWA MOTO BAADA YA KUFUNGIWA NDANI


Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

SIMANZI na majonzi vilitawala katika mji mdogo wa Mbamba bay wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, kufuatia wanafunzi wawili wakazi wa mji huo wanaosoma shule ya msingi Mbamba bay wilayani humo kufariki dunia, baada ya kuteketea kwa moto katika chumba walichokuwa wamelala ambacho inadaiwa kuwa walifungiwa nje kwa kufuli na kuwafanya washindwe kujiokoa.

Kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika vya habari vimeeleza kuwa tukio hilo lilitokea Mei 23 mwaka huu majira ya usiku, ambapo chanzo cha moto huo hadi sasa hakijulikana na kwamba watoto hao walifungiwa kwenye chumba ambacho ni duka la bidhaa mbalimbali ambalo vitu vilivyokuwa ndani yake navyo viliteketea kabisa.

Watoto waliokumbwa na mkasa huo ni Sharifa Nurudin (13) ambaye anasoma darasa la saba na Ismail Nurudin (11) wa darasa la tano katika shule hiyo, imedaiwa kuwa walikuwa wakifungiwa mara kwa mara kwenye duka hilo lenye jina maarufu ‘Kwa mjomba Nuru’ nyakati za usiku, kwa lengo la kulinda  mali zilizomo ndani yake.

“Watoto hawa walikuwa siku zote wanafungiwa nje na kufuli na baba yao mzazi Nurudin Mohamed, licha ya watu kumweleza acha kuwatumikisha watoto hawa kwa mtindo huu alikuwa hataki kusikia na leo watoto wamepoteza maisha kwa sababu ya ujinga wa huyu baba”, alisema mama mmoja mkazi wa mji mdogo wa Mbamba bay ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

Sunday, June 8, 2014

ASASI ZISIZO ZA SERIKALI WILAYANI MBINGA LAWAMANI

Ofisa maendeleo ya jamii Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Paschal Ndunguru akisisitiza jambo alipokuwa akifungua mkutano wa Wadau mapambano dhidi ya UKIMWI uliofanyika kwenye ukumbi wa shule ya sekondari Kigonsera uliopo wilayani humo. Katikati ni Mwenyekiti wa Mamlaka ya mji mdogo wa Mbinga Steven Matesso na upande wa kulia ni Ofisa maendeleo ya jamii Henry Digongwa, anayeshughulikia kitengo cha UKIMWI na tiba. (Picha na gwiji la matukio mkoani Ruvuma)



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

IDARA ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imezinyoshea kidole baadhi ya asasi zisizo za kiserikali wilayani humo kwamba, hazitekelezi majukumu yake ya kazi ipasavyo.

Sambamba na hilo imeelezwa kuwa taarifa za kazi inazofanya hazitolewi kabisa juu ya nini asasi husika inafanya, jambo ambalo ni kinyume na taratibu zilizowekwa wakati zinasajiliwa na kupewa majukumu ya kwenda kuyafanya.

Kauli hiyo ilitolewa na Ofisa maendeleo ya jamii Henry Digongwa anayeshughulikia kitengo cha UKIMWI na tiba, katika halmashauri hiyo alipokuwa kwenye mkutano wa siku mbili na Wadau wa mapambano dhidi ya ugonjwa huo, uliofanyika ukumbi wa shule ya sekondari Kigonsera iliyopo wilayani humo.

Saturday, June 7, 2014

MALUMBANO YA VIGOGO MBINGA YAENDELEA KUIBUA MAPYA

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

























Na Mwandishi wetu,

Mbinga.

IMEBAINIKA kwamba kumekuwa na mgogoro mzito unaoendelea kufukuta wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kufuatia kuwepo kwa malumbano yasiyokuwa na ulazima, kati ya baadhi ya vigogo ngazi ya wilaya hiyo, askari polisi na madereva wa pikipiki.  

Hali hiyo imefikia hatua kwa baadhi yao kudaiwa kunyanyasa madereva wa pikipiki wa wilaya hiyo huku uongozi wa umoja wa madereva hao (UWAMBI) uliopo wilayani hapa, ukijipanga kwenda kwa mkuu wa mkoa huo Said Mwambungu ili waweze kufikisha kilio chao.

Ukweli juu ya mgogoro huo ulijitokeza hivi karibuni katika kikao kilichoketi Mei 22 mwaka huu mjini hapa, endelea kufuatilia mkasa huu kama ifuatavyo;

UWAMBI wanena kwenye kikao hicho:

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Katibu wa umoja huo Bern Mangeni mbele ya mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, kwa niaba ya wanachama wenzake alisema wamekuwa wakinyanyaswa na Ofisa mmoja wa usalama wa taifa wilayani hapa (jina tunalo) na Mkuu wa polisi wa wilaya hiyo Justine Joseph.

“Mheshimiwa mkuu wa wilaya sisi tutaendelea kusonga mbele ngazi ya juu kwa sababu inaonesha umeshindwa kutusaidia, tumebaki kwenye hali ya sintofahamu juu ya tatizo hili”, alisema Bern Mangeni.

Wednesday, June 4, 2014

MBINGA WACHUKIZWA NA MALUMBANO YA VIGOGO WAIOMBA SERIKALI KUINGILIA KATI

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.



















Na Mwandishi wetu,

Mbinga.

BAADHI ya wakazi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wameshauri na kulitaka Jeshi la polisi mkoani humo, lijiepushe  kufanya kazi zake kwa kusikiliza majungu na maneno ya fitina katika utendaji wake wa kazi za kila siku na endapo wasipozingatia hilo, mwisho wa siku huenda jeshi hilo linaweza kujikuta likabaki na askari wachache wasiokuwa na sifa au weledi.

Ushauri huo ulitolewa kwa nyakati tofauti walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, kufuatia kuwepo kwa malumbano yasiyokuwa na ulazima ambayo yanaendelea kati ya baadhi ya vigogo ngazi ya wilaya na askari polisi.

Walieleza kuwa hali hiyo imesababisha hata baadhi yao kutoelewana ambapo kigogo mmoja ambaye ni Ofisa usalama wa taifa (jina tunalo) na Mkuu wa polisi wa wilaya ya Mbinga (OCD) Justine Joseph wanadaiwa kutoelewana na Mkuu wa kituo cha polisi wilayani humo Geofrey Ng’humbi.

Walisema malumbano ya vigogo hao hayana faida katika jamii na yanatokana na Ng’humbi kufanya kazi zake kwa kuzingatia utawala bora, hivyo kuonekana kuwa mwiba kwa wenzake.

Saturday, May 31, 2014

WATAKIWA KUONGEZA JUHUDI KATIKA MASOMO



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANAFUNZI wa shule  ya sekondari  Agustivo iliyopo katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,  wametakiwa kuongeza juhudi katika masomo yao ili waweze kutimiza malengo waliyonayo katika maisha na kuacha kujiingiza kwenye mambo yatakayowaharibia malengo yao.


Ushauri huo umetolewa na mfanyabiashara maarufu  mkoani Ruvuma Abbas Herman, alipokuwa akizungumza  na wazazi na wanafunzi kwenye mahafali ya kidato cha sita shuleni hapo huku akisisitiza umuhimu wa elimu.


Katika sherehe hizo za kuwaaga wahitimu wa kidato cha sita, mfanyabiashara huyo pia aliwazawadia wanafunzi 14  kiasi cha shilingi 25,000  kila mmoja  waliokuwa wamefanya vizuri katika masomo yao na  kiasi cha shilingi 1,000,000 kwa ajili ya shule hiyo ikiwa ni zawadi ya kufanya vizuri kitaaluma mkoani Ruvuma.

Monday, May 26, 2014

VIONGOZI CCM WANAOFANYA KAMPENI KABLA YA WAKATI KUCHUKULIWA HATUA ZA KISHERIA

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Josephat Ndulango, akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake. (Picha na Gwiji la matukio Ruvuma)

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kimewataka viongozi wake kuacha kufanya kampeni kabla ya wakati na atakayebainika hatua kali za kisheria, zitachukuliwa ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Sambamba na hilo kimewataka kuepukana na makundi, na badala yake kupitia mikutano ya wananchi waeleze utekelezaji wa ilani ya CCM ili kuweza kujenga misingi ya kukiimarisha chama, na wananchi waweze kutambua nini kimewafanyia.

Rai hiyo ilitolewa na Katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Songea, Josephat Ndulango alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya mikakati ya kukiimarisha chama hicho.

Ndulango alisema Watendaji katika maeneo mbalimbali wilayani humo baadhi yao wamekuwa kikwazo katika kusukuma mbele maendeleo ya wananchi, hivyo wamesisitizwa kuacha kujiingiza kwenye mambo ya kisiasa badala yake wazingatie majukumu yao ya kazi.

Saturday, May 24, 2014

MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA YAZITAKA HALMASHAURI ZA WILAYA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE IPASAVYO

Baadhi ya Wahariri na Waandishi wa habari wakiwa kwenye mkutano na TFDA katika ukumbi wa hospitali ya mkoa wa Mbeya.

 Mkurugenzi wa huduma za maabara kutoka Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) Charys Ugullum,(aliyesimama) akizungumza na Wahariri na Waandishi wa habari Jijini Mbeya wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.

Baadhi ya Waandishi wa habari na Wahariri wa Nyanda za juu Kusini, wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA). (Picha zote na Kassian Nyandindi)


Na Kassian Nyandindi,
Mbeya.

HALMASHAURI za wilaya hapa nchini kupitia kamati zake za udhibiti wa ubora wa chakula na dawa, zimetakiwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo ili kuweza kulinda afya za wananchi.

Rai hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa huduma za maabara kutoka Mamlaka ya chakula na dawa Tanzania (TFDA) Charys Ugullum alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa siku moja, Wahariri na Waandishi wa habari wa mikoa ya Nyanda za juu Kusini Jijini Mbeya.

Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Hospitali ya mkoa huo, ambapo ulilenga kuwaelimisha Wahariri na Waandishi wa habari  namna ya kuibua matatizo ya bidhaa feki ambazo huuzwa maeneo mbalimbali hapa nchini, kwa lengo la kuleta ufanisi na ubora wa chakula na dawa.

Sunday, May 18, 2014

ASKOFU MKUU WA JIMBO KUU LA SONGEA ASIMIKWA, AWATAKA WATANZANIA KUDUMISHA MUUNGANO

Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Songea mkoani Ruvuma, Damian Dallu.



















Na Kassian Nyandindi,

Songea.

ASKOFU mkuu wa Jimbo kuu la Songea mkoani Ruvuma, Mhashamu Damian Dallu amewataka Watanzania kuuenzi na kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao umedumu kwa miaka 50 sasa, kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

Pia alisema Watanzania waliungana kwa moyo wao wenyewe na sio kwa karatasi, hivyo wanaohangaika kutafuta karatasi zenye maelezo ya muungano huo, wanapoteza muda na kwamba mchakato wa katiba mpya usipewe nafasi ya kuuangamiza taifa hili.

Kauli hiyo aliitoa leo mara baada ya kumalizika kwa ibada ya kusimikwa kuwa Askofu mkuu wa jimbo hilo, ambalo lilikuwa wazi baada ya kujiuzulu aliyekuwa Askofu wake Norbert Mtega mwaka mmoja uliopita.

Sunday, May 11, 2014

NGAGA AWAWEKA KITIMOTO VIGOGO WA HALMASHAURI YA MBINGA

Na Muhidin Amri,

Mbinga.


MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga amegeuka mbogo na kuwaweka kiti moto baadhi ya vigogo wa wilaya hiyo kufuatia kuwepo kwa matokeo mabaya, yaliyopatikana kwenye maeneo wanayo yaongoza katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka jana. 

Ngaga alisema hali hiyo imesababisha wilaya hiyo kushika nafasi ya pili kimkoa  kinyume na maadhimio waliyojiwekea ya kushika nafasi ya kwanza  katika mtihani huo.

Hali hiyo ilijitokeza wakati wa kikao cha tathimini ya elimu ambapo Mkuu huyo wa wilaya hakuridhishwa na hali ya ufaulu katika kata zinazoongozwa na vigogo hao ambao ni Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbinga Christantus Mbunda, ambaye ni diwani wa kata ya Mbangamao.

Vilevile Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Allanus Ngahy diwani wa kata ya Kipapa na diwani wa kata  ya Ngima Winfrid Kapinga ambaye ni makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ambaye pia ni diwani wa kata ya Ngima wote kupitia tiketi ya chama hicho.

Thursday, May 8, 2014

ASKOFU ALIA NA WANASIASA AWASIHI WATIMIZE MAJUKUMU YA WANANCHI KWANZA


Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Mbinga mkoani Ruvuma John Ndimbo, amewataka Madiwani wa wilaya ya Mbinga mkoani humo kuacha itikadi za kisiasa pale wanapotekeleza mambo ya msingi ya wananchi, na endapo wasipozingatia hilo huenda wakasababisha machafuko katika jamii.

“Mwanasiasa yeyote ambaye hana kanuni na hazingatii mambo ya msingi huyo anaipoteza jamii, tuache itikadi za kisiasa tutekeleze kwanza majukumu tuliyopewa na wananchi”, alisema Ndimbo.

Kauli hiyo ilitolewa na Askofu huyo katika kikao cha tathimini ya elimu kilichoketi hivi karibuni, kwenye ukumbi wa jimbo katoliki la Mbinga ambacho kilikuwa kikiendeshwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga.

Sunday, May 4, 2014

TATIZO LA MAJI MBINGA MBIUWASA YANYOSHEWA KIDOLE

Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga.



















Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

UHABA wa maji ni tatizo ambalo limekuwa likiendelea kutesa Wakazi wa mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, na kusababisha wakazi hao kuinyoshea kidole Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (MBIUWASA) iliyopo katika mji huo, ambayo ndio tegemeo kubwa katika utoaji wa huduma hiyo muhimu.

Kufuatia hali hiyo wameitaka Mamlaka kuhakikisha kwamba inatatua kero hiyo mapema, ili wakazi hao waweze kuondokana na adha wanayoipata sasa ya mgao mkali wa maji.

Walisema ni jambo la kushangaza mji huo kukosa maji kwa kile walichoeleza kuwa, ni kipindi cha masika na maji yamekuwa mengi kiasi ambacho hawakutakiwa kukumbwa na karaha hiyo, huku wakifafanua kuwa muda mwingi maji hayo ya mgawo yamekuwa yakielekezwa katika nyumba za vigogo huku watu wa kawaida wakiendelea kuteseka.

Malalamiko hayo yalitolewa kwa nyakati tofauti walipokuwa wakizungumza na Mwandishi wa habari hizi mjini hapa, huku wakidai kuwa wakati mwingine inawalazimu kufuata maji umbali mrefu katika vijito vidogo vidogo, ambavyo huzunguka mji wa Mbinga.

Friday, May 2, 2014

TATIZO LA MIMBA LATISHIA USTAWI WA MAENDELEO KATIKA SEKTA YA ELIMU MBINGA



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

TATIZO la mimba mashuleni kwa shule za msingi na sekondari wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, lisipotafutiwa mbinu ya kudhibitiwa mapema, hakika maendeleo katika sekta ya elimu wilayani humo huenda yakadorola.

Imefafanuliwa kuwa wazazi na walimu katika shule husika ndio chanzo kikuu cha tatizo hilo ambapo kwa kiasi kikubwa, wamekuwa wakifumbia macho kwa kutowachukulia hatua za kisheria watu wanaohusika kuwapatia wanafunzi wa kike ujauzito.  

Wadau wa elimu wilayani Mbinga mkoani humo, walisema hayo mbele ya Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga ambaye alikuwa Mwenyekiti katika kikao cha tathimini ya elimu, kilichoketi katika ukumbi wa Jimboni uliopo mjini hapa.

Tuesday, April 29, 2014

BARAZA LA MADIWANI MBINGA LAMTIMUA OFISA ELIMU SEKONDARI, LASEMA LIMEZINGATIA TAMKO LA WAZIRI

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Kassim Majaliwa.

Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

HATIMAYE Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, limemaliza mzizi wa fitina kwa kumkataa aliyekuwa Ofisa elimu wa wilaya hiyo Hanji Yusuph Godigodi na kusema kuwa hawataki kumuona ndani ya wilaya hiyo, akiendelea kufanya kazi za utumishi wa umma.

Kukataliwa kwa Ofisa huyo kumefuatia baraza hilo kuketi kama kamati kwa muda wa nusu saa kujadili suala hilo, likizingatia tamko lililotolewa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Kassim Majaliwa, Februari 7 mwaka huu wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo.

Jukumu la kuketi kama kamati lilifuatia kuwepo kwa mchezo mchafu ambao ulikuwa ukisukwa chini kwa chini na baadhi ya vigogo wa ngazi ya mkoa huo na wilaya, kwa lengo la kutaka kumrejesha madarakani Ofisa huyo ili aendelee na kazi yake kama kawaida.

Majaliwa alitoa tamko la kumvua madaraka kwa kumshusha cheo Ofisa huyo wa elimu sekondari wilayani humo, na wenzake sita ambao ni walimu wakuu wa shule za sekondari, kufuatia kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kazi na kufanya ubadhirifu wa zaidi ya shilingi milioni 268 za maendeleo ya elimu ya sekondari.

NGAGA AWAPASULIA JIPU MADIWANI MBINGA



Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga amewataka Madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo wasiwe watu wa kugeuka geuka, pale wanapoweka misimamo au misingi muhimu ya maendeleo ya wananchi wa wilaya hiyo.

Ngaga alisema kuwa kumekuwa na baadhi ya Madiwani wamekuwa wakishindwa kusimamia makubaliano halali ya vikao husika, badala yake muda mwingi huishia kulumbana na kuzungumzia mambo ambayo hayana tija kwa wananchi.

Kauli hiyo ya Mkuu wa wilaya Mbinga, ilitolewa leo alipokuwa akizungumza na Madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo katika kikao cha baraza la madiwani hao kilichoketi leo, kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa.

“Hii tabia sipendi, tujenge misimamo yetu katika vikao tusiende na manufaa ya mtu mmoja mmoja, tushirikiane katika hili ili mambo yetu yaende vizuri”, alisisitiza.

Friday, April 25, 2014

HALMASHAURI ZA AGIZWA KUONGEZA VYANZO VYA MAPATO

Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Senyi Ngaga, akisisitiza jambo wakati alipokuwa akifungua mkutano wa ALAT wa mkoa huo, katikati ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Allanus Ngahy na wa mwisho ni Katibu mkuu wa ALAT wa mkoa wa Ruvuma Mohamed Maje. (Picha na Kassian Nyandindi)


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HALMASHAURI za wilaya mkoani Ruvuma zimeagizwa kuongeza vyanzo vipya vya mapato, ambavyo vitaweza kusaidia kuendesha halmashauri hizo na kuhudumia wananchi badala ya kutegemea ruzuku kutoka kwa wafadhili au serikali kuu.

Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga alipokuwa akifungua mkutano wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT)  ambao ulifanyika juzi katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani humo.

Ngaga alisema viongozi wa Halmashauri wasipokuwa wabunifu katika kuongeza mapato, hawataweza kwenda mbele na kutimiza malengo ya kuhudumia jamii ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama vile barabara na miradi ya kilimo.

Wednesday, April 23, 2014

ALAT RUVUMA YALALAMIKIA MWENENDO WA BUNGE MAALUM LA KATIBA

Mwenyekiti wa ALAT mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho. akisisitiza jambo kwenye kikao chao walichoketi leo Mbinga mjini. Anayefuatia ni mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Allanus Ngahy na Katibu mkuu wa ALAT mkoani humo Mohamed Maje.

Na Kassian Nyandindi,

Ruvuma.

WAJUMBE wa jumuiya ya Serikali za mitaa (ALAT) mkoani Ruvuma, wamesikitishwa na mwenendo wa Bunge maalum la katiba ambalo linaendelea sasa mjini Dodoma, kwa kile walichoeleza kuwa hali hiyo inawakatisha tamaa wananchi.

Walisema asilimia kubwa ya wajumbe wa bunge hilo wamekuwa wakitumia muda mwingi nafasi wanazopewa bungeni, kutetea maslahi yao binafsi na sio kuisaidia jamii ambayo iliwaamini waende huko kutetea na kuwasilisha matatizo ya wananchi.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa ALAT wa mkoa huo Oddo Mwisho alipokuwa akisoma taarifa ya maendeleo ya jumuiya hiyo mbele Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, wakati wa mkutano wao wa siku moja uliofanyika kwenye ukumbi mdogo wa Halmashauri ya wilaya hiyo mkoani humo.

“Mheshimiwa mgeni rasmi pamoja na kukushukuru wewe binafsi kukubali kuwa mgeni wetu, tunakuomba utufikishie salamu zetu kwa serikali hasa kuhusu mwenendo wa Bunge letu la katiba unaoendelea bungeni hivi sasa sisi wanajumuiya hii hatufurahishwi nao”, alisema Mwisho.

Tuesday, April 22, 2014

ALAT RUVUMA YAANZA ZIARA YAKE YA KIKAZI WILAYANI MBINGA

Wajumbe wa Jumuiya ya serikali za mitaa (ALAT) mkoani Ruvuma, wakikagua moja kati ya jengo la kusomea watoto katika shule ya wasichana Kigonsera, iliyopo wilayani Mbinga ambayo inatarajia kuanza kuchukua wanafunzi watakaosoma masomo ya sayansi.

Mwenyekiti wa ALAT mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho aliyeinama upande wa kushoto, akiangalia moja kati ya meza ambayo itatumika kusomea wanafunzi wa masomo ya sayansi kwenye shule ya sekondari ya wasichana iliyopo katika kata ya Kigonsera wilayani Mbinga.

Baadhi ya Wajumbe wakiangalia mahindi yaliyolimwa na kikundi cha Muungano kilichopo kata ya Kigonsera wilayani humo.

Upande wa kulia aliyevaa suti nyeusi, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Hussein Ngaga akitoa maelezo mafupi kwa Wajumbe wa ALAT wa mkoa huo, juu ya maendeleo ya ujenzi wa Kituo kikuu cha magari ya abiria ambacho kimejengwa Mbinga mjini. Rais Jakaya Kikwete anatarajia kukifungua mapema mwezi Mei mwaka huu. (Picha zote na Kassian Nyandindi)


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WAJUMBE wa Jumuiya ya Serikali za mitaa (ALAT) mkoani Ruvuma leo wameanza ziara ya kikazi kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Mbinga mkoani humo.

Aidha licha ya kutembelea miradi hiyo wanatarajia ifikapo Aprili 23 mwaka huu, watafanya kikao chao kujadili maendeleo ya mkoa huo na kuweka mikakati madhubuti ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo, kwa faida ya wananchi wa mkoa huo na Taifa kwa ujumla.

Leo wakiwa katika ziara ya kukagua miradi hiyo wilayani Mbinga, wameweza kujionea shule ya Sekondari ya wasichana (Mbinga girls Secondary school) iliyopo katika kata ya Kigonsera wilayani humo ambayo itaanza kuchukua wanafunzi hivi karibuni.

Shule hiyo ni ya mchepuo wa masomo ya sayansi, inauwezo wa kuchukua wanafunzi 80 watakaosoma hapo na wenye kipaji cha masomo hayo.