Friday, December 12, 2014

MKURUGENZI MBINGA AENDELEA KUKALIA KUTI KAVU, WADAU WASEMA UMEFIKA WAKATI KWA SERIKALI KUMCHUKULIA HATUA ZA KINIDHAMU


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

BARUA iliyoandikwa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga juu ya kuifutia usajili asasi ya Waratibu elimu kata wilayani humo (UWEKAMBI) kwa madai kwamba imeshindwa kutimiza masharti na taratibu husika, imezua gumzo huku wakisema kuwa mkurugenzi huyo, amekosa kazi ya kufanya badala yake ajikite katika kufikiria maendeleo ya wanambinga na sio kuendekeza migogoro ambayo haina tija katika jamii.

Barua hiyo yenye kumbukumbu namba MDCC/F.10/20/64 ya Novemba 30 mwaka huu ambayo imesainiwa na mkurugenzi huyo, ambapo waratibu hao walipozungumza kwa nyakati tofauti walisema kuwa kitendo hicho kilichofanywa na mkurugenzi huyo, si cha kiungwana bali ana mambo yake binafsi ambayo hawatakii mema wananchi wa wilaya hiyo.

Walisema UWEKAMBI ilianzishwa kwa nia njema na kwa kufuata taratibu husika za usajili kupitia ofisi yake ya idara ya maendeleo ya jamii, hivyo yeye anavyosema leo kwamba umoja huo unakiuka sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza misingi ya utendaji kazi wa asasi za kiraia, sio kweli bali anachuki binafsi huku wakimtaka asitumie vibaya cheo chake alichonacho na kuingiza mambo binafsi katika utendaji kazi wa maendeleo ya wananchi.

Wednesday, December 10, 2014

ACHENI TUME IFANYE KAZI ZAKE KWA UHURU BILA KUINGILIWA

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HATIMAYE serikali, imechukua hatua ya kuunda tume na kuileta katika halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu juu ya tuhuma anazotuhumiwa Afisa elimu msingi wa wilaya hiyo Mathias Mkali.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Hussein Ngaga ndiye aliyeibua hoja kadhaa za kumtuhumu afisa elimu wake, na kufikia hatua ya kumsimamisha kazi kwa muda, hadi tume hii leo inaripoti hapa Mbinga kwa ajili ya kuja kuchunguza tuhuma hizo kwa lengo la kupata ukweli na kutoa ushauri nini kifanyike.

Kwa ujumla tunapenda kuipongeza serikali kwa jitihada hizi ilizozifanya, na kwamba tunashauri tu kwa kuiomba tume hiyo isimame kidete katika kutenda haki kwa pande zote mbili yaani aliyetuhumu na mtuhumiwa, ili wananchi siku ya mwisho tuweze kutambua ukweli wa jambo hili upo wapi, ambapo kila kukicha limekuwa likikera na kuleta mgogoro ambao umedumu kwa muda mrefu sasa.

Tuesday, December 9, 2014

DED MBINGA ALALAMIKIWA WAMTAKA AZINGATIE MAKUBALIANO YALIYOFANYWA NA WAZAZI

Hussein Ngaga, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.










Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

AGIZO lililotolewa hivi karibuni na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga juu ya michango wanayochanga wazazi kwa ajili ya watoto wao kujisomea wakati wa likizo (Makambi) wilayani humo, na kuingizwa kwenye akaunti ya fedha za ruzuku kutoka serikalini kwa ajili ya kuendeshea mitihani mashuleni (Capitation) limezua mapya, kufuatia kamati husika zinazojishughulisha na uendeshaji wa makambi hayo kulalamika wakidai kwamba, kufanya hivyo ni ukiukaji wa taratibu na makubaliano yaliyofanywa na wazazi kupitia vikao husika.
 
Imeelezwa kuwa ni vyema mkurugenzi huyo, akazingatia mawazo na makubaliano yaliyofanywa na wazazi hao na sio vinginevyo, hivyo kutozingatia hilo ni kukosa utawala bora katika jamii na kuleta migogoro isiyokuwa ya lazima.

Kwa nyakati tofauti walipozungumza na mwandishi wa habari hizi wajumbe wa kamati hizo walieleza kuwa, michango inayokusanywa kutoka kwa kila mzazi ambaye ana mtoto anayesoma katika shule husika, hukabidhiwa mkuu wa kambi na kamati hufanya kazi ya kupanga mapato na matumizi na sio utaratibu huo ambao mkurugenzi huyo ameutoa.

Walidai kuwa michango hiyo kuingizwa kwenye akaunti ya Capitation hivi sasa kunaleta kikwazo kikubwa kwao, hasa pale wanapohitaji kufanya matumizi husika kwani wanapokwenda kwa mkurugenzi huyo ili waweze kupata fedha hizo kwa ajili ya kuendeshea shughuli za watoto hao katika kambi, hukumbana na vikwazo vingi.

Walifafanua kuwa uendeshaji wa makambi hayo ni mfumo ambao wazazi wa wilaya hiyo walijiwekea mikakati yao wenyewe na kujenga makubaliano juu ya namna ya kuinua kiwango cha taaluma, kupitia vikao vya Mabaraza ya kata (WDC) ambapo makubaliano yao yalikuwa kila mchango unapokusanywa akabidhiwe mkuu wa kambi husika, kwa ajili ya kupanga matumizi na baadaye mwisho wa kambi taarifa ya mapato na matumizi itolewe kwenye kikao hicho cha WDC kwa eneo husika.

Saturday, December 6, 2014

WAFANYABIASHARA TUNDURU WALIA NA SERIKALI


Na Steven Augustino,

Tunduru.

WAFANYABIASHARA na walipa kodi wanaotakiwa kutumia mashine za kielektroniki (EFD'S) wilayani Tunduru mkoani hapa, wameiomba serikali inunue mashine hizo na kuzigawa bure kwa wafayabiashara hao, ili ziweze kusaidia serikali kukusanya kodi husika.

Ombi hilo limetolewa na wafanyabiashara hao wakati walipokuwa wakizungumza na maafisa waandamizi wanaosimamia ukusanyaji wa kodi, katika mkutano uliofanyika kwenye Ukumbi wa New generation uliopo mjini hapa.

Mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Kazembe Said ndiye aliyeanza kufanya uchokonozi wa kupenyeza ombi hilo, na kuongeza kuwa pamoja na mambo mengine wao hawapingani na taratibu za ulipaji wa kodi, isipokuwa kinacho wakwaza ni kutokuwa na mitaji ya kutosheleza kununua mashine hizo.

Wakati wafanyabiashara hao wakionekana kuunga mkono ombi hilo naye Leonsi Kimario akaja na hoja ya kuisihi serikali, kuandaa utaratibu mzuri wa matumizi na mapato ambayo yamekuwa yakitokana na kodi za wananchi tofauti na sasa, ambapo kumekuwa kukitokea kashfa za matumizi mabaya ya fedha yakiwa yanazungumzwa mara kwa mara Bungeni.

AFARIKI DUNIA BAADA YA PIKIPIKI ALIYOKUWA AKIENDESHA KUGONGA POWER TILLER



Na Mwandishi wetu,

Tunduru.

STAMILI Mohamed (42) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Namiungo wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, amekutwa na mauti baada ya pikipiki aliyokuwa akiiendesha kupata nayo ajali, akiwa katika mwendo kasi.

Taarifa zinaeleza kuwa pikipiki hiyo aliyopata nayo ajali, ni aina ya SUNLG yenye namba za usajili T 339 na kwamba ajali hiyo, ilitokana pia na kuligonga trekta dogo ambalo hutumika kufanyia shughuli za kilimo shambani (Power tiller) na kusababisha kifo chake papo hapo.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma  Mihayo Msikhela amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo, akieleza kwamba ajali hiyo ilitokea Disemba 4 mwaka huu majira ya usiku.

CUF YATAMBA, YASEMA CCM UMEFIKA WAKATI WA KUFUNGA VIRAGO


Na Steven Augustino,

Tunduru.

CHAMA Cha wananchi (CUF) Taifa kimetangaza sera ya kutoa gawiwo kwa wananchi wake, endapo kitapatiwa ridhaa ya kuongoza nchi katika uchaguzi mkuu ujao ikiwemo wananchi watanufaika na rasilimali za taifa, katika kipindi chake cha uongozi.

Aidha kitafungua akaunti maalumu tatu ambapo baadhi ya mapato yake  ndiyo yatakayokuwa yakigawiwa kwa wananchi hao.

Katibu Mkuu wa CUF makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim seif Sharifu alisema hayo alipokuwa akihutubia wananchi wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhamasisha wananchi kujiunga na chama hicho.

Friday, December 5, 2014

TAARIFA ILIYOSOMWA NA MKAGUZI WA NDANI NA MADIWANI KUNYANG'ANYWA HII HAPA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

NDUGU wasomaji wa mtandao huu, sasa tunawaletea taarifa ya Mkaguzi wa ndani juu ya hoja zilizojitokeza katika kikao cha fedha, mipango na uongozi kilichoketi Septemba 25 mwaka huu wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, na kuwasilishwa katika kikao cha baraza la madiwani la wilaya hiyo Oktoba 27 mwaka huu, kama tulivyosema kuwa katika toleo lililopita kwamba Madiwani walinyang'anywa mara baada ya kusomwa katika baraza hilo.

Taarifa hiyo ambayo imesainiwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Hussein Ngaga ina hoja saba za kumtuhumu Afisa elimu wake wa idara ya elimu msingi wilayani humo, Mathias Mkali kwamba amefanya ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na taratibu za fedha za utumishi wa umma, jambo ambalo baadhi ya Madiwani wengi wao walipinga hoja hizo na kusema kuwa jambo hilo halina kweli badala yake ni mambo ambayo yalikwisha kubaliwa na kupitishwa kwenye vikao halali na baraza la madiwani kwa ujumla. (nakala tunazo) 

Katika hali ya kushangaza, taarifa hiyo iligawiwa kwa madiwani katika baraza hilo, ghafla wajumbe husika (Madiwani) baada ya taarifa hiyo kumaliza kuisoma mkaguzi wake wa  ndani, Laston Kilembe na madiwani hao kuipinga, ghafla madiwani walinyang’anywa huku mkurugenzi akisimama mbele ya kikao na kueleza kuwa haijakamilika watapatiwa tena katika kikao kijacho cha baraza hilo.

Sasa taarifa yenyewe ni hii hapa.............................



Wednesday, December 3, 2014

KILELE CHA MAADHIMISHO YA WALEMAVU IRINGA: SERIKALI YAPIGA MARUFUKU UJENZI WA MAJENGO YASIYO RAFIKI KWA WALEMAVU


Waziri  wa nchi  ofisi ya  waziri  mkuu (sera na uratibu wa bunge) William Lukuvi akihutubia katika kilele  cha siku ya  walemavu duniani, maadhimisho  yaliyofanyika katika viwanja vya kichangani mjini Iringa Kitaifa,  na Lukuvi kumwakilisha  Waziri mkuu Mizengo Pinda ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.


Waziri  wa nchi  ofisi ya  waziri mkuu  sera  na uratibu wa bunge, William Lukuvi akimkabidhi cheti cha ushiriki mlemavu, Tumaini  Mdegella kwa  niaba ya ofisi za Neema Crafti mjini Iringa  wakati wa kilele  cha maadhimisho ya  siku ya  walemavu duniani, yaliyofanyika kitaifa  mjini humo.
Na Mwandishi wetu,
Iringa.

SERIKALI  imeziagiza  Mamlaka  za  usafiri  wa majini na nchi kavu (SUMATRA )  nchini,  kuanza mchakato  wa  kukaa na  wamiliki wa  vyombo  hivyo  ili kuanza  uagizaji  wa vyombo  vya usafiri yakiwemo mabasi ambayo ni  rafiki na walemavu nchini, huku ikipiga marufuku  majengo ya   serikali kujengwa bila kuwepo kwa  mchoro  unaoonyesha mazingira yanayozingatia makundi  yote ya jamii  likiwemo la walemavu wa viungo.

Agizo   hilo  limetolewa na  Waziri  mkuu Mizengo  Pinda, wakati  wa maadhimisho ya  siku ya  walemavu  duniani yaliyofanyika   kitaifa  katika  viwanja  vya kichangani mkoani  Iringa.

Akiwahutubia   walemavu hao na  wananchi  waliofika katika  viwanja   hivyo waziri  mkuu, aliyewakilishwa na Waziri  wa nchi  ofisi ya  waziri mkuu (sera na uratibu wa bunge) Wiliam Lukuvi ambaye ni mbunge wa  jimbo la Isimani mkoani Iringa, alisema kimekuwepo kilio  cha muda  mrefu kutoka kwa  walemavu  juu ya kusahulika katika ujenzi  wa  majengo mbalimbali, ambayo yamekuwa  yakijengwa  bila kuzingatia  kundi la  watu  wenye  ulemavu jambo ambalo ni sawa na  kuwabagua watu  hao.

Aidha alisema  katika  kuona kilio  hicho  cha  walemavu  kinafanyiwa  kazi  kuanzia  sasa, majengo  yote ya  serikali  zikiwemo  shule na taasisi nyingine  kabla ya  kuanza  ujenzi  wake lazima  wasimamizi wa  ujenzi  huo kujiridhisha kwa  mchoro ambao  utaonyesha  mazingira  yatakayomuwezesha  mlemavu,   kutumia jengo  husika bila usumbufu  wowote tofauti na  ilivyo sasa ambapo  idadi kubwa ya majengo mazingira  yake  si rafiki kwa  mlemavu.

"Ni  siku  nyingi  watu  wenye ulemavu  wamekuwa  wakilalamika juu ya mazingira  yasiyo rafiki    katika majengo  mbalimbali............ sasa  leo naomba  kuagiza  kuwa michoro yote inayochorwa katika majengo ya  huduma za  kijamii,  ni marufuku  kupitishwa ama  wasimamizi  wa  ujenzi  husika  kuruhusu ujenzi  iwapo mchoro hauonyeshi  kama utajali makundi  yote wakiwemo  walemavu,

“Wasimamizi  wote msikubali  kusimamia  wala  kutangaza  tenda  ya ujenzi kama ramani  yake  si rafiki kwa  mlemavu, lakini  pia  hata  kwenye mabasi hivi unamtegemea mtu mwenye ulemavu wa miguu ataingia vipi na baiskeli  yake  katika gari iwapo hakuna mazingira  yanayomwezesha  kuingia, hivi  sasa  teknlojia  imezidi kukua na baadhi ya nchi  wameanza muda mrefu kuwajali walemavu kwa kuwa na mabasi ambayo mlemavu anaingia na baiskeli  yake  na  kushuka nayo   bila usumbufu, ni vyema hata Sumatra mkaangalia uwezekano wa  kuwajali  walemavu hawa”, alisema  Lukuvi.

WAZIRI MKUU PINDA MBINGA KUNA HAJA YA SERIKALI KUINGILIA KATI KUMALIZA TATIZO HILI

Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

TAARIFA ya Mkaguzi wa ndani juu ya hoja zilizojitokeza katika kikao cha fedha, mipango na uongozi kilichoketi Septemba 25 mwaka huu wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, na kuwasilishwa katika kikao cha baraza la madiwani la wilaya hiyo Oktoba 27 mwaka huu, imeendelea kukosolewa na wadau mbalimbali wa elimu wilayani humo wakisema kwamba ni mpango mbovu ambao ulisukwa na watu wachache wenye ni mbaya ya kurudisha nyuma maendeleo katika sekta ya elimu, licha ya kila kilichoelezwa kwenye taarifa hiyo kilikwishapitishwa kwenye vikao halali vya halmashauri ya wilaya hiyo.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo Hussein Ngaga ndiye anayenyoshewa kidole akidaiwa kuwa na kundi la watu wachache, ambao wanaelezwa ndiyo vinara wa kusuka mpango huo ambao sasa umefikia katika hatua ambayo inaleta mgogoro ambao hauna tija kwa wanambinga.

Ngaga katika taarifa hiyo ametoa hoja saba za kumtuhumu Afisa elimu wake wa idara ya elimu msingi Mathias Mkali kwamba, amefanya ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na taratibu za fedha za utumishi wa umma, jambo ambalo tumelifanyia utafiti na kubaini sio kweli badala yake ni mambo ambayo yalikwisha kubaliwa na kupitishwa kwenye vikao halali. (nakala tunazo) 

Katika hali ya kushangaza, taarifa hiyo iligawiwa kwa madiwani katika baraza hilo ambayo imesainiwa na mkurugenzi huyo, ghafla Wajumbe husika (Madiwani) baada ya taarifa hiyo kumaliza kusoma mkaguzi wa ndani, Laston Kilembe walinyang’anywa huku mkurugenzi akisimama mbele ya kikao na kueleza kuwa haijakamilika watapatiwa tena katika kikao kijacho cha baraza hilo.

Hali hiyo iliyojitokeza wengi wao walikuwa wakihoji inakuwaje baraza linaletewa taarifa ambayo haijakamilika, huku wengine wakisema huenda ndio ulikuwa mpango wenye kubeba matakwa binafsi ambayo hayana tija kwa jamii.

Tuesday, December 2, 2014

SONGEA WALALAMIKIA UBOVU WA DALADALA WAZITAKA MAMLAKA HUSIKA KUCHUKUA HATUA



Na Gideon Mwakanosya,
Songea.

BAADHI ya wakazi wa halmashauri ya Manispaa ya songea mkoa wa Ruvuma, wamezilalamikia  mamlaka husika zikiwemo kikosi cha usalama barabarani mkoani humo na  Sumatra kwa kushindwa kudhibiti daladala mbovu, zinazofanya kazi ya kubeba abiria katika manispaa hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi hao wameeleza kuwa kwa muda mrefu sasa, daladala ambazo zinaonyesha kuwa ni mbovu lakini zimekuwa zikiendela kubeba abiria zimekuwa zikihatarisha maisha ya abiria wanaotumia daladala hizo.

Felix Komba mkazi wa Mahenge alisema kuwa daladala zinazotoka Songea mjini mtaa wa Delux, kwenda Matogoro na Songea Boys zinaonekana hata kwa macho kuwa ni mbovu.

Monday, December 1, 2014

MBINGA WANASHUGHULIKA KUKOMOA WANANCHI BADALA YA KUSIMAMIA MAENDELEO, AGIZO LA RAIS KIKWETE UJENZI WA MAABARA UTATA MTUPU

Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Na Kassian Nyandindi,


SIKU zote misingi ya taifa linalojali maisha ya wananchi wake ni ujenzi bora wa elimu, afya na miundombinu inayokuza uchumi huku viongozi wake katika eneo husika hutakiwa kuwa makini, kujenga mshikamano na kuacha migogoro ya hapa na pale.

Wahenga wetu husema, ukiona kiongozi muda mwingi amekuwa akiendekeza migogoro basi tambua kwamba, mahali pale ameshindwa kutawala na maendeleo hayawezi kupatikana badala yake serikali, inashauriwa kuchukua hatua za haraka katika kunusuru hali hiyo ili wananchi wake wasipate mateso.

Kinyume chake kukosekana kwa kiongozi wa kweli na asiyejali utawala bora au maslahi ya wananchi, kunanyima watu fursa ya kufanya maamuzi sahihi kuhusu rasilimali zao, ikiwemo hata kujiondoa katika lindi la umasikini unaonuka.

Popote pale kiongozi wa namna hii, ni sawa na kusema ni kiongozi muflisi ambaye hutambulika muda mwingi kupenda kuruhusu mianya ya rushwa kutawala kila kona, hasa wakati wa utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi anaowaongoza.

Katika makala haya napenda kuelezea juu ya kilio cha baadhi ya wananchi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, dhidi ya Mkuu wao wa wilaya Senyi Ngaga na Mkurugenzi wake Hussein Ngaga, jinsi gani wanavyoiyumbisha wilaya hiyo na kufikia hatua wananchi kukosa imani nao.

Nimefikia hatua ya kuliweka jambo hili hadharani kutokana na mambo kadhaa yanayokera wananchi ambayo viongozi hawa, wamefikia sasa kuchukiwa na watu wanaowaongoza kutokana na kile kinachoelezwa kuwa kupenda kufanya mambo ambayo hayana msingi katika mustakabali mzima, wa maendeleo ya wananchi wa wilaya hiyo.

Jambo la kwanza, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali ambavyo vimetoa ushirikiano wa karibu kwa mwandishi wa makala haya, vimeeleza kuwa mkuu wa wilaya hiyo ameshindwa kukemea mgogoro ambao unaendelea kufukuta kwa muda mrefu kati ya mkurugenzi huyo na afisa elimu msingi wa wilaya hiyo, Mathias Mkali.

Aidha wanaongeza kuwa licha ya afisa elimu huyo kuonekana kufanya kazi zake vizuri katika kuboresha kiwango cha taaluma wilayani humo, cha kushangaza viongozi hao wamekuwa wakimpiga vita pasipo sababu yoyote ya msingi na kusababisha kuwepo kwa tabaka kubwa, ambalo linaitafuna wilaya kwa kurudisha nyuma maendeleo katika sekta hiyo muhimu.

Wanasema mkuu wa wilaya Ngaga, kukaa kwake kimya pamoja na serikali kukemea migogoro kazini huenda akawa amejenga maslahi yake binafsi, na kusahau jukumu alilopewa na Rais Jakaya Kikwete, wakati anamteua kwenda kutumikia wananchi wa wilaya hiyo kwa kuzingatia kuepuka misingi ya itikadi, rangi au dini na mambo mengine ambayo hayana tija katika jamii.

Wengi kwa nyakati tofauti wanasema, vitendo vinavyofanywa na mkurugenzi huyu huku mkuu huyo wa wilaya kutoingilia kati na kukemea, ni sawa na kushughulika kukomoa wananchi badala ya kubuni na kusimamia maendeleo kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Senyi Ngaga namfahamu vizuri, ni dada yetu ambaye wananchi wa Mbinga tulikuwa na imani naye katika kujenga mshikamano wa kuweza kusukuma mbele gurudumu la maendeleo, lakini kwa haya yanayoendelea sasa anakatisha tamaa wananchi anaowaongoza. 

Saturday, November 29, 2014

WANACCM RUVUMA WATAKIWA KUACHA MAJUNGU NA FITINA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM) Sixtus Mapunda, aliyevaa skafu shingoni akiangalia mganda ngoma ya asili, wakati alipowasili juzi katika ofisi kuu za Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Songea mkoa wa Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,
Songea.

VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma, wametakiwa kujenga ushirikiano na kuacha vitendo vya majungu na fitina ndani ya chama, huku ikielezwa kuwa endapo kama wataendeleza mambo hayo yatawafanya wagawanyike katika makundi na kusababisha hata wanachama wa chama hicho wakose imani nao.

Aidha walielezwa kuwa CCM ni chama ambacho kipo madarakani kwa miaka mingi tokea nchi hii ipate uhuru, mikononi mwa Baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere, hivyo wanapaswa kuzingatia taratibu na sheria zilizowekwa kwa mujibu wa katiba husika ili wananchi wasiweze kujengeka na dhana potofu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM) Sixtus Mapunda alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa CCM, kwenye ukumbi wa Songea Club uliopo mjini hapa.

Sunday, November 23, 2014

AFISA USALAMA WA TAIFA WILAYA YA MBINGA AMTISHIA MWANDISHI WA HABARI KWA BASTOLA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Na Gideon Mwakanosya,


Mbinga.

MWANDISHI wa habari Kampuni ya Businesstimes Limited, Kassian Nyandindi anayeandikia gazeti la Majira wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, ameshushiwa kipigo na kutishiwa kuuawa kwa silaha na Afisa usalama wa taifa (DSO) wa wilaya hiyo (Jina tunalo) katika hoteli ya Gold Farm ya Mbinga mjini.

Habari zilizopatikana mjini hapa, zimeeleza kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 22 mwaka huu, majira ya saa 5 usiku kwenye hoteli hiyo wakati mwandishi huyo alipokuwa anaaga kurudi nyumbani kwake.

Taarifa zaidi za tukio hilo zilifafanua kuwa, Nyandindi ambaye alikuwa kwenye ziara ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (UVCCM) Sixtus Mapunda, alishushiwa kipigo na kigogo huyo wa usalama wa taifa ambapo baadhi ya wajumbe wa UVCCM wakiwemo maafisa wa umoja huo toka makao makuu ya chama hicho, walishuhudia tukio hilo.

Aidha wajumbe hao walipoona hali inazidi kuwa mbaya, walishitushwa na kufikia hatua ya kwenda karibu na tukio hilo na kuingilia kati ili kuweza kumnusuru mwandishi huyo asiweze kudhurika, licha ya kuwa wakati huo tayari alikuwa anapigwa mateke na ngumi huku kigogo huyo akiporomosha lugha chafu akimtukana mwandishi huyo.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida inadaiwa kwamba afisa usalama huyo wa taifa, baada ya kuona mwandishi Nyandindi amebebwa na kuingizwa kwenye gari ili apelekwe nyumbani kwake, ghafla alitoka kwenye eneo la tukio na kwenda kuchukua silaha aina ya bastola, aliyokuwa ameihifadhi kwenye gari lake ambalo alikuwa ameliegesha  nje ya hoteli hiyo.

Habari zaidi za tukio hilo zilifafanua kuwa wakati silaha hiyo akiwa ameishika mkononi tayari kwa kutaka kumfyatulia risasi mwandishi wa habari, baadhi ya wajumbe wa UVCCM waliokuwepo kwenye eneo hilo la tukio walimdhibiti afisa usalama huyo na kufanikiwa kumnyang’anya silaha hiyo, ambayo baadae ilidondoka chini na kuokotwa na mmoja wa viongozi hao wa chama huku wakimuuliza kwa nini unataka kufanya mauaji kwa mwandishi wa habari huyu, ambapo alishindwa kuwa na majibu zaidi aliendelea kufoka kwa hasira huku akiporomosha matusi.

Saturday, November 22, 2014

KATIBU MKUU UVCCM TAIFA AENDELEA NA ZIARA YAKE WILAYANI MBINGA, SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA VIONGOZI WENYE MATENDO YA HOVYO

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM) Sixtus Mapunda, akipokelewa na Vijana wakiwemo pia wanachama wa Chama Cha Mapinduzi leo asubuhi, katika eneo la Tanki la maji mjini hapa wakati anawasili wilayani Mbinga akitokea wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.

Katibu Mkuu UVCCM Taifa, Sixtus Mapunda akiwasili katika ofisi kuu ya CCM wilayani Mbinga.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM) Sixtus Mapunda akizungumza na wananchi wa kata ya Mpepai wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KATIBU wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM) Sixtus Mapunda amesema, serikali nchini ipo tayari kumchukulia hatua za kinidhamu kiongozi yeyote aliyekuwa madarakani, ambaye anaonesha kuwa na matendo ya hovyo kwa wananchi wake na yenye  kurudisha nyuma maendeleo husika.

“Ndugu zangu wananchi hatupo tayari mahali popote pale, kumvumilia Mkuu wa wilaya au Mkurugenzi mtendaji mwenye matendo ya hovyo na yenye kukatisha tama wananchi, tukisikia tunamwondoa haraka tunahitaji kiongozi mwenye kujali maisha na maendeleo ya watu wake”, alisema.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu huyo leo, alipokuwa akihutubia wananchi wa kata ya Mpepai wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Mpepai wilayani humo.   

Mapunda alisema kuwa itakuwa ni ajabu kwa chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumkalia kimya bila kumwajibisha kiongozi ambaye hana nia njema na taifa hili, huku akiwaacha wananchi wakiteseka kutokana na mambo yake binafsi ambayo hayana tija katika jamii.

Friday, November 21, 2014

KATIBU MKUU UVCCM TAIFA KUFANYA ZIARA MBINGA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM) Sixtus Mapunda.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KATIKA kuhakikisha kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) hapa nchini kinaendelea kuwa imara na kuwajali wananchi wake, Katibu mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) wa chama hicho, Sixtus Mapunda atafanya ziara yake ya kikazi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kwa lengo la kuzungumza na wananchi wa wilaya hiyo ikiwemo pia na taratibu za kuimarisha chama na umoja huo kwa ujumla.

Habari zilizotufikia hivi punde zinaeleza kuwa Katibu huyo atapokelewa mjini hapa kesho, Novemba 22 mwaka huu majira ya saa 3:00 asubuhi na kuwasili kwenye viwanja vya ofisi kuu ya CCM wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, akitokea wilaya ya Nyasa mkoani humo.

Wananchi wa wilaya hiyo wameombwa kujitokeza kwa wingi, katika kushiriki zoezi hilo muhimu  la mapokezi.

Aidha Mapunda katika ziara yake baada ya kuwasili kwenye ofisi za chama hicho, atafanya ziara fupi akielekea kata ya mpepai kwa ajili ya kuzungumza na kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wa kata hiyo.

Baadaye atarudi Mbinga mjini kwa lengo pia la kuzungumza na wananchi mnamo majira ya mchana, hivyo wadau wanaombwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano wa hadhara ambao atahutubia kwenye viwanja vya soko kuu vilivyopo mjini hapa.

Kwa ujumla Mapunda sio mtu mgeni kwa wananchi wa wilaya ya Mbinga, wengi wao wamekuwa wakimfahamu akiwa mzaliwa wa wilaya hii, hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kumsikiliza.

Pamoja na mambo mengine, Katibu huyo wa vijana mnamo Novema 23 mwaka huu wakati anamaliza ziara yake ya kikazi wilayani humo, atazungumza na wakazi wa kijiji cha Kigonsera hatimaye kuelekea Songea mjini.


Monday, November 17, 2014

KWA MAMBO HAYA YANAYOFANYWA NA MKURUGENZI HUYU WA MBINGA, HAKIKA SEKTA YA ELIMU HUENDA IKADOROLA WILAYANI HUMO


Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, akisisitiza jambo wakati akiwa katika vikao wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, katikati ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Allanus Ngahy na Mkurugenzi wake Hussein Ngaga.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

JINAMIZI linalodaiwa kutengenezwa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga katika kuhakikisha linaendelea kumsakama Afisa elimu msingi Mathias Mkali na walimu wake, imeelezwa kuwa ni dalili tosha zinazoashiria kurudisha nyuma maendeleo katika sekta ya elimu msingi wilayani humo, ambapo hivi sasa limeingia katika sura mpya kwa walimu wakuu wa shule hizo likitaka taarifa ya mapato na matumizi ya fedha za TSM. 9 na Capitation zinazopelekwa mashuleni.

Mkurugenzi huyo amewaandikia barua walimu hao ambayo nakala yake tunayo, yenye kumbukumbu namba MDCC/F. 10/20/43 ya Novemba 10 mwaka huu, ikiwataka waandae taarifa hiyo ya kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2011 hadi sasa 2014/2015.

Baadhi ya walimu waliokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti walisema, wanamshangaa Mkurugenzi huyo kuwaandikia barua hiyo ambayo ameichelewesha kuwafikia walimu hao, ikiwataka kufanya kazi hiyo   jambo ambalo ni vigumu huku wengine wakibeza na kusema huenda anatafuta sababu kwa mwalimu atakayekosea na kushindwa kukamilisha kwa wakati apate cha kusemea.

Walisema wamechoshwa na mambo yake tokea aingie katika wilaya ya Mbinga, amekuwa ni mtu wa kuongoza wenzake kwa njia ya migogoro na kuwatafutia sababu zisizo na msingi badala ya kukaa na kubuni mipango ya kimaendeleo, huku wakiongeza kuwa kazi hiyo ilibidi aikamilishe Mkaguzi wake wa ndani, Laston Kilembe alipokuwa akipita hivi karibuni kuhoji mashuleni kwa walimu wakati anafanya ukaguzi wake juu ya fedha hizo, lakini mkaguzi huyo hakufanya hivyo ndio maana hivi sasa walimu hao wanasumbuliwa akiwataka watekeleze hilo.

Sunday, November 16, 2014

CHEMBA YA WAFANYABIASHARA MBINGA YAITAKA SERIKALI ULIPAJI KODI UFANYIKE MAHALI BIDHAA INAPOZALISHWA, GAUDENCE KAYOMBO LAWAMANI


Gaudence Kayombo, Mbunge wa Jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

UMOJA wa Chemba ya Wafanyabiashara Tanzania (TCCIA) tawi la Mbinga mkoa wa Ruvuma, umepanga mikakati na kuitaka serikali iweke taratibu zake ambazo zitahakikisha kwamba, kila jambo la ulipaji wa kodi lifanyike pale mahali ambapo bidhaa inazalishwa kwa lengo la kukuza uchumi wa eneo husika na Taifa kwa ujumla. 

Aidha kodi za makampuni yanayofanya kazi au biashara yoyote wilayani humo, malipo yafanyike Mbinga ikiwa ni lengo la kumfanya mfanyabiashara mkubwa na mdogo, asiweze kuumizwa kwa kutozwa kodi kubwa.

Hayo yalisemwa katika kikao cha Wafanyabiashara hao kilichoketi ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) mjini hapa, ambapo walieleza kwamba wafanyabiashara wa wilaya hiyo hutozwa kodi kubwa ya mapato kutokana na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa, ambapo walitolea mfano kwa wale ambao hujishughulisha na ununuzi wa zao la kahawa wilayani humo, kwenda makao makuu ya kampuni zao yaliyopo nje ya Mbinga kulipia kodi zao. 

Vilevile mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Menlick Sanga, aliongeza kuwa licha ya wilaya hiyo kuwa na mwekezaji mkubwa wa mgodi wa makaa ya mawe Ngaka, ambayo uchimbaji wake hufanyika katika kijiji cha Ntunduaro kata ya Rwanda wilayani humo, bado amekuwa halipi kodi hapa wilayani na wilaya kutonufaika na chochote hivyo ni vyema serikali ikaliangalia hilo ili malipo husika kwa mwekezaji huyo aweze kuyafanya hapa hapa wilayani.

Saturday, November 15, 2014

MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA MBINGA KATIKA HILI UMEKENGEUKA



Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WASOMAJI wetu wa mtandao huu mara ya mwisho tuliwaeleza kwamba tutaendelea kuwaletea tuhuma zingine ambazo zinaonesha kuleta mashaka dhidi ya Afisa elimu msingi Mathias Mkali wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, ambazo Mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo Hussein Ngaga anamtuhumu huku akijua fika kwamba anamuonea na hazina ukweli wowote ambapo binafsi haziningii akilini kwa mtu mwenye akili zake timamu, endelea kufuatilia sakata hili kupitia mtandao huu.............

Awali tuliwafafanulia juu ya chanzo cha mgogoro huu kwamba kuhusiana na tuhuma inayojieleza kwamba Afisa elimu huyo ameunda NGO yake inayofahamika kwa jina la UWEKAMBI ambapo kirefu chake ni Umoja wa Waratibu Elimu Kata wilaya ya Mbinga.

Sasa nachukua safu hii kutaka kuelezea tuhuma zingine ambazo Mkurugenzi huyo amemtuhumu Afisa elimu huyo na inanilazimu niziweke bayana juu ya ukweli wake.

Nikiachana na tuhuma hiyo ya Umoja wa Waratibu Elimu Kata wilaya ya Mbinga, naingia katika tuhuma ya Ununuzi na matumizi ya mafuta ambapo Hussein Ngaga anamtuhumu Mkali kwamba ameiba mafuta na kuyatumia yenye thamani ya shilingi milioni 25,547,500 yakiwemo Petroli lita 5,500 na Diesel lita 5,500 yaliyoagizwa Mei 26 mwaka huu na mafuta ya nyongeza Petroli lita 4,500 na Diesel lita 4,500 ikiwemo na vilainisho vyenye thamani ya shilingi milioni 22,250,000 yaliyoagizwa Agosti 12 mwaka huu ambapo ukweli ni kwamba;

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa mafuta haya yote yaliombwa kwa Mkurugenzi huyo, ili kuwezesha uendeshaji wa mitihani 11 ya Mock kata, Mock mkoa ambapo ulifanyika mtihani mmoja na shughuli za kujisomea watoto wakati wa likizo yaani Makambi kwa darasa la saba.

Aidha mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa darasa la saba, mtihani wa ufundi na matumizi ya ofisi kama dharula za misiba na uhamisho kwa shule 227 na kata za kielimu 38 ikiwemo pia na vituo vya makambi 42 mafuta hayo yalitumika katika shughuli hizo.

Katika mahitaji hayo ni mtihani pekee wa kumaliza elimu ya msingi ndio Mkurugenzi Hussein Ngaga, alinunua mafuta Petroli lita 1,000 na Diesel lita 5,000 mnamo mwezi Septemba mwaka huu, ambapo mafuta hayo yalitumika kusambaza mtihani wa kumaliza elimu ya msingi na yalitumika ndani ya siku tatu na yakaisha.

Mahitaji ya mafuta hayo hapo juu yaliombwa kwa kuzingatia kuwa toka mwezi Machi 2014, idara ya elimu msingi wilayani Mbinga haikupewa mafuta ya uendeshaji mitihani ya mock kata, wilaya na mock mkoa ambapo pamoja na idara kutopewa mafuta haikusimamisha utekelezaji wa shughuli zake za kila siku yaani matokeo makubwa sasa (BRN).

NGAGA KIBULI HIKI KWA MAMBO UNAYOYAFANYA UNAKIPATA WAPI, MBINGA UNAIPELEKA WAPI?


Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

TAARIFA zilizotufikia hivi punde Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga ameitisha kikao na Waratibu elimu kata wakiwemo pia Watendaji wa kata wa wilaya hiyo kwa lengo la kujadili mikakati mbalimbali ya maendeleo husika, ikiwemo suala la waratibu hao na watendaji kwa lengo la kutaka kuwarubuni kwa namna moja au nyingine juu ya kukubalina naye katika mgogoro ambao unaendelea sasa kati yake na Afisa elimu msingi wa wilaya hiyo Mathias Mkali. 

Kikao hicho ambacho kinafanyika katika ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa, vyanzo mbalimbali vya habari vimeeleza kuwa kukutana na watu hao kunatokana na Mkurugenzi huyo kuendelea kupanga njama na kutangaza kwamba Afisa elimu huyo ni mwizi, ili watendaji hao na waratibu wamkubali kwa kile anachokitaka yeye jambo ambalo wengi wao wamekuwa wakishangazwa nalo, huku wengine wakieleza kuwa ni vyema Ngaga akaachana na mambo hayo badala yake awe mbunifu wa mambo ya kimaendeleo na sio kuendekeza migogoro isiyokuwa na tija kwa jamii.

Walisema, Mkurugenzi huyo tokea afike wilayani hapa ni mtu wa kuendekeza majungu na migogoro isiyokuwa na msingi kwa wananchi wa Mbinga, huku wakihofia kwamba endapo ataendeleza mambo hayo huenda wilaya hiyo ikarudi nyuma kimaendeleo.

Katika hatua nyingine wengi wao walieleza kuwa tokea afike katika wilaya hii ni mwaka mmoja sasa umepita, lakini amekuwa ni mtu wa kupenda migogoro na kupanga safu katika idara mbalimbali kwa lengo la kutaka kuweka wakuu wa idara ambao yeye anawataka kwa maslahi yake binafsi.