Na Kassian Nyandindi,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma limesema, limefanikiwa
kumkamata mtuhumiwa mmoja kati ya watano ambao walihusika katika tukio la kurushia
mawe msafara wa kampeni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kijiji cha Mtua,
kata ya Mpepai wilayani Mbinga mkoani humo na kuharibu magari mawili.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Revocatus Malimi alisema
hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu na kuongeza kuwa katika tukio hilo
wengine watano, wametokomea kusikojulikana ambapo wanaendelea kuwasaka ili
waweze kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria, kujibu tuhuma inayowakabili.
Malimi alisema usiku wa kuamkia Septemba 22 mwaka huu, askari
wake walifanya msako mkali katika kata hiyo na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja
kati ya hao, aliyemtaja kwa jina la Christopher Mapunda (32) ambaye ni mkazi wa
kijiji hicho.
Magari mawili yameharibiwa vibaya, baada ya watu wanaodaiwa
kuwa ni wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuvamia msafara
huo na kurusha mawe huku watu waliokuwemo ndani ya magari hayo nao wakinusurika
kujeruhiwa.
Alifafanua kuwa mtuhumiwa huyo aliyekamatwa, ndiye aliyekuwa
kiongozi wa kuwahamasisha watuhumiwa wenzake warushie mawe msafara huo wa
kampeni za CCM, katika kata hiyo ya Mpepai na kwamba wakati wowote kuanzia sasa
atafikishwa Mahakamani.
Hata hivyo, magari ambayo yaliharibiwa ni pamoja na gari la
Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Mbinga lenye namba za usajili T 545 BEW aina ya
Landcruiser Hardtop limevunjwa kioo cha ubavuni upande wa kushoto na lingine
aina ya Landrover Discover, lenye namba T 797 AEN nalo limevunjwa vunjwa vioo
kwa mawe ambayo yalikuwa yakirushwa.
No comments:
Post a Comment