Monday, September 21, 2015

TUNDURU YAJIVUNIA RASILIMALI ZAKE

Mnara wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.
Na Muhidin Amri,
Tunduru.

IMEELEZWA kwamba kuwepo kwa rasilimali nyingi, katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, ni moja kati ya sifa zinazoifanya wilaya hiyo kuwa miongoni mwa wilaya zinazofaa kwa shughuli za uwekezaji miradi mbalimbali ya maendeleo na kuifanya wilaya hiyo, iweze kukua kiuchumi.

Tina Sekambo ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu kuhusiana na mkakati uliopo wa kuitoa wilaya, katika umaskini na kuwa wilaya tajiri kwa kutumia rasilimali zake zilizopo.

Kwa mujibu wa Sekambo alisema kwamba, wilaya yake imebarikiwa kuwa na fursa nyingi kama vile ardhi inayofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali, mabonde na mito inayotiririsha maji mwaka mzima, ambayo kama itaendelezwa vizuri itaweza kusaidia hata katika shughuli za kilimo cha umwagiliaji.


Mkurugenzi huyo alizitaja shughuli nyingine kuwa ni za uvuvi katika mto Ruvuma, utalii katika hifadhi ya Taifa ya Selou, misitu na madini ya kila aina ambayo yakitumika vizuri yataweza kuibadili wilaya na wananchi wake waweze kukua kiuchumi.


Mbali na hayo wilaya ya Tunduru, ndiyo inayoongoza kwa uzalishaji mkubwa wa zao la korosho katika ukanda wa pwani wa Tanzania, na kwamba ni zao pekee linalotegemewa wilayani humo katika kuongeza mapato ya wilaya hiyo.

No comments: