Na Steven
Augustino,
Tunduru.
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, mgonjwa ambaye alikuwa
amelazwa Hospitali ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Mariam Njaidi amezua
jambo baada ya kumshambulia kwa kipigo Muuguzi mmoja wa kitengo cha maabara
katika hospitali hiyo, kutokana na kucheleweshewa majibu ya vipimo vyake vya
magonjwa ya taifodi na sukari.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Thabit Mwambungu. |
Mgonjwa huyo ambaye alikuwa amelazwa wodi namba tatu,
aliwashangaza wagonjwa wenzake waliolazwa hospitalini hapo baada ya kuamka
kitandani alipokuwa amelala na kwenda kumfuata muuguzi, Hiren Msokwa katika
chumba cha maabara na kuanzisha mapigano kati yao ambaye baadaye alimkuta akiwa
na majibu yake mikononi mwake.
Hali hiyo inadaiwa ilitokana na Njaidi kucheleweshewa majibu
ya vipimo vya magonjwa hayo kwa zaidi ya siku tatu, ambayo yamekuwa yakimsumbua
kwa muda mrefu.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema, awali mabishano yalianza
kutokea kati ya wauguzi waliokuwa zamu katika wodi hiyo na mgonjwa huyo ndipo
alipochukua maamuzi ya kwenda mwenyewe, kufuata majibu ya vipimo vyake maabara
ambako alikutana na muuguzi huyo na kuanza kupigana naye.
Pamoja na mambo mengine, uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa
habari hizi umebaini kuwa matatizo hayo katika hospitali ya Tunduru yanatokana pia
na baadhi ya wafanyakazi wake kutotimiza majukumu ya kazi zao ipasavyo, ndio
maana kumekuwa na migongano kati yao na wagonjwa.
Nimezungumza kwa nyakati tofauti na baadhi ya wagonjwa
wanaokwenda kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo, walidai kuwa jambo hilo limekuwa
ni tatizo sugu linaloendelea kuwatesa pale wanapohitaji matibabu hospitalini
hapo, na kwamba wanaiomba serikali kuingilia kati ili kuweza kunusuru hali
hiyo.
Kwa upande wake Mganga
mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Tunduru, Dokta Zabron Mmari alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa mapigano hayo yalisababisha, Msokwa kupatwa na majeraha ya kawaida mwilini.
Alisema hali hiyo inatokana na kujirudia matukio ya aina
hiyo, ambapo Septemba 16 mwaka huu mlinzi wa hospitali hiyo, Chande Bakari naye
alivamiwa na ndugu ya mtunza mgonjwa aliyekuwa hospitalini hapo ambaye
alifahamika kwa jina la, Jobe Khatibu.
No comments:
Post a Comment