Na Muhidin Amri,
Namtumbo.
KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyefanikiwa kwenye
kinyang’anyiro cha uchaguzi kura za maoni, kuomba ridhaa ya kugombea nafasi ya
ubunge kupitia tiketi ya chama hicho Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma, Edwin
Ngonyani amewasihi wanachama wenzake walioshindwa kwenye mchakato huo kuacha
kupakana matope au kufikiria kukihama chama hicho, bali waungane pamoja ili
kukipa nguvu na hatimaye kiweze kufanya vizuri katika uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Tabia na mawazo ya namna hiyo alieleza kuwa hayana mantiki
yoyote ile, kwa kile alichodai kuwa hata kama watakimbilia kwenye vyama vingine
vya siasa kwa lengo la kutafuta uongozi, bado nafsi zao zitawasuta.
Ngonyani aliyasema hayo muda mfupi mara baada ya msimamizi wa
uchaguzi kura za maoni wilayani humo, Oscar Msigwa kumtangaza kuwa ndiye
aliyeshinda kugombea nafasi hiyo ya ubunge katika jimbo hilo.
Aidha aliwashukuru wanaccm kwa kumchagua kwenye
kinyang’anyiro hicho, ambapo hii ni mara ya pili kwake kugombea nafasi hiyo ya
ubunge katika jimbo la Namtumbo, na kwamba mara ya kwanza aliwahi kugombea
mwaka 2010 ambapo kura hazikutosha.
Katika uchaguzi huo wa kura za maoni mwaka huu, alieleza
amejifunza kwamba jambo kubwa aliloliona ambalo linapaswa kuchukuliwa hatua na
kukemewa ni pale wagombea wanapotumia nguvu kubwa ya kifedha kusaka madaraka,
jambo ambalo linahatarisha kuwanyima haki wagombea ambao wanasifa ya kuongoza
wananchi lakini hawana fedha ya kufanya hivyo.
Mchakato wa kura za maoni kwa nafasi ya ubunge kwenye jimbo
hilo umelazimika kurudiwa mara tatu, ambapo kwa mara ya kwanza Vita Kawawa
aliibuka mshindi ambapo matokeo yake yalipingwa na wagombea wenzake 11 kwa kile
kilichodaiwa kuwa kuwepo kwa kasoro ya kuzidi kura zilizopigwa tofauti na idadi
ya wanachama, ambao walistahili kupiga kura husika.
Kutokana na kasoro hiyo, Katibu Mkuu taifa wa CCM Abdulrhaman
Kinana aliamuru kurudiwa kwa uchaguzi huo ambapo Ediwn Ngonyani aliibuka
mshindi kwa kupata kura 12,606 huku nafasi ya pili, ikichukuliwa na Salome
Sijaona kwa kupata kura 7,002 na Vita Kawawa akishika nafasi ya tatu kwa
kuambulia kura 2,749.
Hata hivyo matokeo hayo yalilalamikiwa tena na wagombea
wengine akiwemo, Kawawa ambapo hata uliporudiwa kwa mara ya tatu bado Ngonyani
aliweza kuwashinda wagombea wenzake, kwa kupata kura 13,573 huku mpinzani wake
wa karibu, Kawawa akipata kura 10,068 na Salome Sijaona kura 6,015.
No comments:
Post a Comment