Na Mwandishi wetu,
Tunduru.
WANANCHI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameaswa kujiepusha
na vishawishi vinavyosababisha kuuza ardhi yao kwa wageni bila kufuata taratibu
za nchi, ikiwa ni lengo la kuwafanya waweze kuepukana na vitendo vya uporaji vinavyofanywa
na watu wajanja, hatimaye kuwa maskini na watumwa katika nchi yao.
Badala yake wametakiwa kutumia utajiri wa ardhi waliyonayo,
kuzalisha kwa wingi mazao mbalimbali ili wajikwamue na waondokane na umaskini.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mohamed Lawa alisema hayo
alipokuwa akizungumza na wanachama wa chama hicho, katika kijiji cha Nandembo
kwenye ziara yake ya kikazi ya kuhamasisha wananchi kushiriki katika mikutano
ya kampeni ya wagombea wa chama hicho, inayoendelea sasa hapa nchini.
Lawa alisema kuwa mipaka ya Tunduru na maeneo mengine ya
nchi, imeanza kufunguka hivyo anaimani wilaya itapokea wageni wengi kutoka
ndani na nje ya nchi, ambao watahitaji maeneo kwa ajili ya shughuli za kiuchumi
hivyo wanaowajibu wa kutunza ardhi yao kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye.
Alisema kuingia kwa wageni hao ni jambo zuri ambalo
litasaidia kukua kwa uchumi wa wilaya hiyo, lakini itakuwa sio jambo la busara
kuona wananchi wanauza maeneo yao kiholela bila kufuata taratibu na ushauri
kutoka kwa wataalamu husika, na kubaki mwisho wa siku wanahangaika kutokana na
kuuza kwa bei ndogo ambayo hailingani na thamani halisi.
“Nawataka wananchi watumie ardhi yao kwa shughuli za
maendeleo yao na sio kukimbilia kuwauzia wageni, wakati sisi wenyewe tukiendelea
kubaki maskini”, alisema Lawa.
Kadhalika aliipongeza serikali ya chama tawala kwa
utekelezaji wa ahadi zake kwa wananchi wa wilaya ya Tunduru, kwani kumekuwa na
dalili tosha za kuvutia wageni kwenda kuwekeza huko ambapo wilaya hiyo ni kati
ya wilaya chache ambazo zimebahatika kuzungukwa na madini ya aina mbalimbali,
misitu, ardhi na wanyama.
Mbali na hilo alisema kujengwa kwa barabara ya lami kutoka
Namtumbo, kwenda Tunduru hadi Masasi na kuanza utekelezaji wa mradi wa umeme
vijijini (REA) ni ishara kubwa kwamba serikali imedhamiria kumaliza kero
zilizokuwa zinakwamisha maendeleo ya wananchi wake.
No comments:
Post a Comment