Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa Polisi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Ramia
Mganga amewataka madereva wanaoendesha pikipiki wilayani humo, maarufu kwa jina
la Yebo yebo kuacha kutumiwa vibaya na wanasiasa, jambo ambalo linahatarisha
usalama wao na kusababisha malumbano yasiyokuwa ya lazima.
Aidha alikemea kitendo cha madereva hao baadhi yao kuleta
vurugu, kuchoma moto bendera za vyama na kubandua mabango ya wagombea hao katika
kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi, ambayo yamebandikwa katika maeneo
mbalimbali jambo ambalo amewasihi kwa kuwaeleza kitendo hicho waachane nacho,
kwani husababisha na kuleta mifarakano au mipasuko katika jamii.
Mganga alisema hayo alipokuwa akizungumza na baadhi ya
waendesha pikipiki wa wilaya hiyo, katika viwanja vya eneo la stendi kuu ya
magari ya abiria mjini hapa.
Kadhalika aliwataka kutii sheria za nchi bila shuruti, ambapo
kwa yule atakayeonekana anakiuka atachukuliwa hatua, ili kuweza kudhibiti hali
hiyo na kutoweza leta madhara kwa wengine.
“Nawataka tujenge ushirikiano, itikadi zenu za vyama vya
siasa isiwe chanzo cha vurugu na kuhatarisha usalama wa wengine tufanye kazi
zetu kwa amani, tusikubali kutumiwa na wagombea wa chama fulani ambao wamekuwa
wakiwatuma mfanye jambo, kwa maslahi yao na kutaka kuleta machafuko”, alisema
Mganga.
Kadhalika kwa upande wao madereva hao wa pikipiki, nao kwa
nyakati tofauti walimhakikishia Mkuu huyo wa Polisi wilaya ya Mbinga kwamba
wapo tayari kujenga ushirikiano wa pamoja na Jeshi la Polisi wilayani humo, kwa
kutoa taarifa pale itakapoonekana kuna tatizo au uhalifu wa aina fulani ili
hatua ziweze kuchukuliwa kwa haraka, kabla ya kutokea madhara.
No comments:
Post a Comment