Na Mwandishi wetu,
Tunduru.
VIONGOZI wa vyama mbalimbali vya siasa hapa Tanzania, wameendelea
kushauriwa kufanya mikutano yao ya kampeni za siasa kiustaarabu, katika kipindi
hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, bila
kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu uliopo hapa nchini.
Mkurugenzi wa shirika la maendeleo, mikoa na matawi ya
Tanzania Red cross Society, Julius Kejo alitoa wito huo alipokuwa akizungumza
na wadau wa shirika hilo kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo, jinsi ya
kukabiliana na majanga wakati wa kampeni hizo.
Aidha aliwakumbusha viongozi wa dini, kuongeza juhudi na
kutoa mahubiri yanayolenga kusisitiza amani na utulivu katika nchi yetu, ili isiweze
kujitokeza machafuko yanayoweza kuliangamiza taifa hili.
Kejo alisema endapo kampeni hizo zitafanyika bila kuathiri
ubinadamu au utu wa mtu, upo uwezekano wa kutotokea matendo ambayo yanaweza
kusababisha madhara katika jamii.
Alifafanua kwamba shirika lake litaendelea kuimba wimbo wa
amani na utulivu kwa watanzania, na kuongeza kuwa mafunzo hayo yamekwisha
tolewa kwa wadau wengine wa maeneo ya Mtwara, Dar es Salaam, Iringa na Songea
kwa lengo la kuwaweka tayari ili waweze kukabiliana na matukio ya uchaguzi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya viongozi wa vyama
vya siasa, Katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani
Tunduru, Nyenje Undi aliwatupia viongozi wa chama tawala CCM, akidai kuwa ndiyo
wamekuwa wakivitumia vibaya vyombo vya dola likiwemo jeshi la Polisi ambalo
badala ya kutenda haki limekuwa likivikandamiza vyama vya upinzani, kwa kutumia
mabavu na vipigo kwa raia wasiokuwa na makosa kitendo ambacho kinasababisha
uvunjifu wa amani.
Akijibu juu ya hilo, mwakilishi wa Kamanda wa Polisi wilayani
Tunduru mkoa wa Ruvuma, SP. Nico Mwakasanga alisema kuna kila sababu jamii
kutii sheria bila shuruti pale amri inapotolewa na vyombo vya ulinzi na
usalama, ili kulisaidia shirika la Red cross kutofanya shughuli za uokoaji wa
majanga ambayo yamekuwa yakisababishwa na vipigo vya Polisi.
Mwakasanga alibainisha kuwa tayari Jeshi hilo limekwisha
fanya kazi ya kutoa elimu kwa askari wake, juu ya matumizi ya nguvu kwa
wananchi hasa wakati huu kuelekea uchaguzi mkuu huku akiongeza kuwa, askari
atakayekikuka maelekezo husika atachukuliwa hatua za kisheria.
Upande wa viongozi wa madhehebu ya dini ambao waliwakilishwa
na mchungaji Myiya Kashimito wa kanisa la Biblia Tunduru na Shekh Abdalah Mdidu,
waliahidi kuongeza juhudi katika kutimiza wajibu wao na kwamba wakati wote
wataendelea kuhubiri amani na utulivu.
Awali akifungua mafunzo hayo Mwenyekiti wa shirika hilo wilayani
humo, Rashid Mchileka aliwataka Wadau wake kuwa wajumbe wazuri katika kusambaza
elimu watakayoipata, ili kuweza kuepusha jamii isiweze kujiingiza kwenye
makundi mabaya yatakayoweza kusababisha vurugu.
No comments:
Post a Comment