Wananchi wakiwa katika mikutano mbalimbali ya kisiasa wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma. |
Na Muhidin Amri,
Tunduru.
WANACHAMA 153 kutoka Chama cha wananchi CUF na CHADEMA katika
wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wamevihama vyama hivyo na kujiunga na Chama
Cha Mapinduzi (CCM) wakidai kuwa wamechoshwa na siasa zisizokuwa na malengo kwa
Watanzania, pamoja na udikteta unaofanywa na viongozi wa vyama hivyo kufanya
maamuzi mbalimbali bila kushirikisha wanachama wao.
Miongoni mwa wanachama hao, 120 ni wa kutoka CUF na 33
CHADEMA walitangaza juzi kuhama katika vyama hivyo, mbele ya katibu wa Chama
Cha Mapinduzi wa wilaya hiyo, Mohamed Lawa tukio ambalo liliambatana na
kurudisha kadi za vyama hivyo.
Walisema kuwa kwa muda mrefu sasa vyama hivyo vimekosa demokrasia
ya kweli, ambapo viongozi wake ni watu ambao wamekuwa wakifanya maamuzi ambayo
yamekuwa kinyume na matarajio ya watanzania walio wengi, wanaohitaji maendeleo.
Waliongeza kuwa hata kupokewa kwa Waziri mkuu mstaafu, Edward
Lowassa ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo na hatimaye kuwa mgombea
urais wa Ukawa, ni udhaifu alionao Freeman Mbowe, James Mbatia na Maalim Seif
Sharif kwani hapakuwa na sababu ya wao kumpokea Lowassa kwani mgombea wa kiti
hicho hajawahi kukanusha wala kuwaeleza wananchi, ukweli juu ya tuhuma za
ufisadi zilizomkabili akiwa ndani ya CCM.
Aidan Mbawala na Khalfan Wilis kutoka CHADEMA walieleza kuwa
viongozi wao wa Ukawa hawajatenda haki kwa wanachama wao, ambapo walitakiwa
kwanza kupata maoni kutoka kwao juu ya uhalali wa Lowassa kama anafaa kujiunga
na umoja huo, huku wakidai kuwa hayo ni matokeo ya ubinafsi na tamaa ya fedha
ambazo wanaimani wamepewa au kuahidiwa na mgombea huyo.
Walidai kuwa Mbowe na Mbatia ni watu ambao wanapenda sana
fedha, hivyo ujio wa Lowassa sio jambo geni kwao kwani ikumbukwe kwamba
alipoenguliwa na CCM katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi hiyo, alikwisha
tangaza kuwa hawezi kukihama chama hicho.
Nao wanachama kutoka CUF, Yasin Jafar na Ahamad Issa walisema
wamechukua jukumu la kurudisha kadi na kujiunga na chama tawala baada ya
kuchukizwa na uamuzi wa viongozi hao, kumshawishi na kumpokea Lowassa kwenda
huko jambo ambalo hata viongozi wenzao ngazi ya juu wamekuwa wakilipinga.
Mbali na hilo wanachama hao wamempongeza Dokta Wilbrod Slaa
na Profesa Haruna Lipumba kwa maamuzi mazuri waliyochukua, kuhama kwenye vyama
hivyo vinavyounda Ukawa kwani viongozi wanaounda umoja huo hakuna hata mmoja
mwenye sifa ya kuwaongoza watanzania, kutokana na tabia ya ubinafsi na tamaa ya
fedha waliyonayo.
Pia Hamad Issa amewatahadharisha wanachama wenzao, wa kutoka
vyama vya upinzani kuwa macho na viongozi wao kwa kile walichodai kuwa wanaweza
kuwapotezea muda wao, hasa baada ya kuonekana hawana nia njema kwa wananchi
bali wapo kwa maslahi yao binafsi.
Alipokuwa akiwapokea wanachama hao, Katibu wa CCM wilaya ya
Tunduru Mohamed Lawa licha ya kuwapongeza amewataka kujenga ushirikiano na
wanachama wenzao wa chama hicho tawala, kwa kuhakikisha kinapata ushindi wa
kishindo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Lawa alisema chama hicho, kimejipanga kikamilifu kuhakikisha
ushindi unapatikana kwenye uchaguzi huo kwa nafasi ya Ubunge, Diwani na Rais
huku akiwataka wagombea kujiepusha na lugha za matusi wanapokuwa jukwaani
badala yake wajenge hoja zitakazowashawishi wananchi, kuwapigia kura.
No comments:
Post a Comment