Ziwa Nyasa lililopo wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma. |
Na Kassian
Nyandindi,
Nyasa.
BAADHI ya wananchi wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wamepongeza
jitihada zinazofanywa na Benki ya NMB kwa kuanzisha na kutoa huduma za kifedha
wilayani humo, jambo ambalo limekuwa ni mkombozi kwao katika kuendeleza
biashara zao.
Walisema kitendo cha benki hiyo kutoa huduma ya kufungua
akaunti, kulipa hundi, kuweka na kutoa fedha kwa kutumia mfumo wa Benki jamii
(Bank on Wheel) kumeweza kuwapunguzia umbali mrefu wa kufuata huduma hiyo
ambapo awali walikuwa wakilazimika kwenda wilaya ya Mbinga, ili waweze kupata
mahitaji ya kifedha katika taasisi hiyo ya kifedha.
Aidha walifafanua kuwa wilaya ya Nyasa ni wilaya mpya, ambayo
tokea kuanzishwa kwake sasa ni faraja kwa wananchi wa wilaya hiyo, kusogezewa
karibu huduma hiyo muhimu kwa faida ya maendeleo yao.
Hayo yalisemwa na wananchi wa wilaya hiyo, walipokuwa
wakizungumza na mwandishi wetu na kuongeza kuwa kutokana na wilaya kuwa na watu
wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali, kama vile uvuvi wa samaki na
wakulima wa zao la kahawa sasa wataweza kufanya biashara zao kwa ufanisi zaidi
kutokana na kusogezewa karibu huduma za kifedha.
“Tunawapongeza watu hawa wa NMB kwa kuwa na wazo la kuanzisha
huduma hii muhimu hapa kwetu, hata uchumi wa wilaya yetu ya Nyasa utaweza kukua
na kusonga mbele kimaendeleo”, alisema Aden Komba.
Komba ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kilosa kata ya kilosa
wilayani humo, alibainisha kuwa jitihada hizo zinazofanywa na benki hiyo ili ziweze kuleta mafanikio, kuna kila
sababu NMB ikafanya mpango wa kujenga ofisi za kudumu za kutolea huduma za
kifedha katika wilaya hiyo, ili wananchi waweze kupata hata huduma za mikopo
kwa karibu zaidi.
Vilevile kwa upande wa wafanyakazi ambao wameajiriwa na
serikali kwenda kufanya kazi katika wilaya hiyo ya Nyasa, nao walipongeza jitihada
hizo na kueleza kuwa kila mwishoni mwa mwezi walikuwa wakilazimika kufuata
huduma za mishahara wilayani Mbinga, ambako ni mbali kutoka wilayani humo
lakini sasa imekuwa kwao ni rahisi kupata huduma hiyo.
No comments:
Post a Comment