Katibu mkuu Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi Taifa (UVCCM), Sixtus Mapunda. |
Na Steven
Augustino,
Tunduru.
JUMUIYA ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM)
wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, imewataka wanachama wake na wananchi kwa
ujumla kujitokeza kwa wingi na kwenda kupiga kura bila uoga wala hofu ya aina
yoyote, kwa lengo la kumchagua kiongozi wanayemtaka Oktoba 25 mwaka huu.
Katibu wa UVCCM wilayani humo, Juma Khatibu alisema hayo
alipokuwa akizungumza na wananchi waliohudhuria kwenye mkutano wa kampeni wa
kuwanadi wagombea udiwani, katika kata za Masonya, Majengo na Mlingoti
Mashariki mjini hapa.
Alisema kuwa umoja huo umechukua hatua hiyo, kufuatia kuwepo
kwa taarifa za vitisho ambavyo husambazwa kwa njia ya vipeperushi wilayani
humo, zenye nia ya kuwatia hofu wananchi wasipige kura.
Khatibu alieleza kuwa watu walio katika makundi maalumu kama
vile wazee na walemavu, wamekuwa wakitishwa kwamba siku hiyo ya uchaguzi
kutakuwa na makundi ya vijana ambayo yameandaliwa kuleta fujo, zitakazowazuia
wasipige kura za wagombea waliosimamishwa na CCM.
Alibainisha kuwa katika kuwahakikishia ulinzi na usalama siku
hiyo, umoja huo umekwisha andaa makamanda 11,876 ambao watasambazwa kama
wasimamizi na walinzi wa kura za chama hicho tawala, katika vituo vyote vya
kupigia kura.
No comments:
Post a Comment