Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.
WAKATI joto la uchaguzi likiendelea kupanda kwa vyama vya
siasa na wagombea wake ndani ya vyama hivyo, imeshauriwa kuwa ni vyema wagombea
hao wajenge moyo wa subira na uvumilivu juu ya mambo yanayohusiana na maslahi
ya taifa, ikiwemo kutoa nafasi kwa wananchi kutekeleza majukumu yao ya
kimaendeleo na sio kuwa chanzo cha vurugu na uvunjifu wa amani.
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Chande Nalicho
alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na viongozi wa dini na wagombea nafasi
mbalimbali za uongozi katika vyama vya siasa, wilayani humo.
Nalicho alisema kuwa suala la maslahi ya kitaifa ni jambo
ambalo linapaswa kupewa kipaumbele, na wanasiasa kuacha kutanguliza maslahi yao
binafasi ili waweze kuwatumikia vyema Watanzania.
Aidha aliwataka viongozi wa dini wilayani Namtumbo,
kuhakikisha wanawahimiza waumini wao kushiriki vyema kwenye uchaguzi mkuu na
kujiepusha kumchagua mtu kwa misingi ya itikadi ya dini au kabila.
“Viongozi wenzangu nawaombeni sana kuelimisha waumini wetu
kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu mwaka huu, wananchi wasikose
kushiriki kwenye mikutano ya kampeni ya vyama vyote vya siasa kwani hii ndiyo
fursa pekee ya kuwapima wagombea wetu kama wanafaa au hawafai, ili baadaye
tuweze kumchagua kiongozi bora wa kuweza kuongoza taifa letu”, alisema Nalicho.
Kadhalika alisema suala la uchaguzi si la mtu mmoja au chama
fulani cha kisiasa bali ni kwa ajili ya watu wote wenye sifa ya kupiga kura,
hivyo kuna umuhimu kwa viongozi wa vyama hivyo wanapopanda majukwaani na viongozi
wa dini wanapokuwa kwenye nyumba za ibada kuhubiri amani, ili uchaguzi huo
ufanyike kwa utulivu.
Kila mtanzania kwa nafasi aliyonayo alisema, anapaswa kuimba
wimbo huo na kujiepusha kueneza maneno yanayoweza kusababisha kuleta chuki na
vurugu kwa wafuasi wa chama kimoja au kingine, kwa kile alichoeleza kuwa
watanzania wengi wanapenda kuendelea kuishi na kufanya shughuli mbalimbali za
kimaendeleo katika kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment