Na Mwandishi wetu,
Ruvuma.
SERIKALI wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, imewaonya
watumishi wake na kuwataka kutojiingiza katika vitendo vya kushabikia na
kuzungumzia mambo siasa wakiwa ofisini, kwani kufanya hivyo ni kinyume cha
taratibu na maadili mahali pa kazi.
Imeelezwa kuwa kufanya hivyo kunapunguza muda wa kuwatumikia
wananchi, badala yake waongeze juhudi kutekeleza majukumu yao waliyopewa na
serikali ili kuweza kuleta tija katika jamii, ikiwemo upatikanaji wa huduma
muhimu kwa faida ya maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Mkurugenzi mtendaji Halmashauri ya wilaya hiyo, Ally Mpenye
alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi juu ya taratibu
za maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika, oktoba 25 mwaka huu kwa
nafasi ya Rais, diwani na mbunge ambapo kwa mamlaka aliyonayo yeye ndiye
msimamizi mkuu wa uchaguzi huo ndani ya wilaya.
Mbali na hilo, Mpenye pia amepiga marufuku tabia ya baadhi ya
watumishi wa serikali kutumia ofisi za umma kuzungumzia mambo ya kisiasa huku
wakisahau jukumu lao la kuwatumikia wananchi bila kujali itikadi ya vyama, dini
au kabila ambao hufika katika ofisi zao wakihitaji kupatiwa huduma kwa njia ya
ushauri, utaalamu na mawazo mbalimbali ili waweze kutatua na kuondoa kero zao
kwa namna moja au nyingine.
“Mimi ndiye kiranja mkuu ndani ya halmashauri, nimekwisha
keti na watumishi wenzangu wanaonihusu kwa idara zote hapa wilayani na kuwaeleza
wasitumie ofisi za walipa kodi kuzungumzia siasa, siwakatazi kuwa na itikadi za
vyama isipokuwa wanatakiwa kufanya hivyo pale wanapotoka nje ya ofisi zao”,
alisema Mpenye.
Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, alisema kuwa
licha kupiga marufuku mtumishi kushabikia siasa katika eneo la kazi, kadhalika
hakuna ruhusa kwa mtumishi yeyote kuingia ndani ya jengo la halmashauri akiwa
amevaa sare ya chama chochote cha siasa.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo alisema kuwa ofisi yoyote ya
serikali ni ya kila mwananchi, ukizingatia kwamba wao ndiyo walipa kodi
wanaoiwezesha ofisi hiyo iweze kufanya kazi hivyo ni kosa kwa mtumishi
aliyepewa dhamana na serikali kumtumikia mwananchi, kuvaa sare ya chama fulani
wakati anapokuwa ofisini kwa atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua
kwa mujibu wa sheria na kanuni za utumishi wa umma.
Alisema kwa mtumishi wa umma, hakatazwi kuwa na mapenzi kwa
chama cha siasa anachokitaka isipokuwa mapenzi yake anatakiwa akayaonyeshe mara
baada ya kutoka nje ya ofisi hizo, ili kuepuka mifarakano inayoweza kutokea
kati yao na wananchi pale wanapohitaji huduma mbalimbali kutoka kwenye ofisi
hizo.
No comments:
Post a Comment