Friday, September 18, 2015

MWAMBUNGU RUVUMA AWAPA SOMO JKT

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

VIJANA wanaomaliza mafunzo katika vikosi  mbalimbali, vya Jeshi la kujenga Taifa (JKT) wametakiwa kutojihusisha na kuwa sehemu ya mgawanyiko kwa watanzania kwa misingi ya kuendekeza itikadi ya dini, siasa na ukabila jambo ambalo linaweza kusababisha uvunjifu wa amani hapa nchini.

Aidha wameshauriwa kuwapuuza wanasiasa ambao wanalengo la kuwatumia kwa maslahi yao binafsi katika kusaka uongozi, badala yake waweke kipaumbele cha kuisaidia jamii na kudumisha upendo na umoja.

Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu alipokuwa akifunga mafunzo ya miezi mitatu kwa vijana 1,124 katika kikosi cha 842 KJ Mlale wilayani Songea, mkoa humo.


Mbali na hilo Mwambungu aliwataka vijana hao kutoyumbishwa na kundi lolote la wanasiasa, ambao kila kukicha wamekuwa wakitaka kusababisha machafuko ya hapa na pale na yenye kuhatarisha kutokuwepo utulivu na kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

“Ndugu zangu leo mmehitimu mafunzo yenu, nahitaji mkawe askari wa kwanza katika kufichua watu wanaoonesha dalili za kuanzisha mambo yanayoenda kinyume na tamaduni zetu hasa katika suala uvunjifu wa amani, endapo mtanusa kuwepo kwa dalili hizi toeni taarifa haraka katika vyombo husika ili serikali iweze kuchukua hatua kabla madhara hayajatokea”, alisema Mwambungu.

Kwa upande wake Mkuu wa brigedia 401 Songea, Jenerali John Chacha alisema kuwa mafunzo ya JKT kwa vijana wanaomaliza elimu ya juu ni muhimu sana kwao, kwa ajili ya kujifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na maadui wakati nchi inapotokea machafuko.

Chacha alifafanua kuwa mafunzo hayo, pia huwajengea uwezo wa kuwa na maadili na kiongozi imara kwa siku za usoni wakati wanapoajiriwa.


Aliongeza kuwa kutokana na umuhimu huo, ndio maana serikali imekuwa ikitenga kiasi kikubwa cha fedha ili kufanikisha mafunzo kwa vijana, katika vikosi hivyo vya JKT hapa nchini.

No comments: