Na Muhidin
Amri,
Namtumbo.
SERIKALI imelipa kiasi cha shilingi milioni 257,004,000 kwa
kaya maskini 56 ambazo ziliibuliwa wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, kupitia
mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) awamu ya tatu ili ziweze
kuwasaidia kugharimia mahitaji yao muhimu, ikiwemo matibabu, chakula na kulipa
karo za watoto wao shuleni.
Ofisa ushauri na ufuatiliaji kutoka katika mfuko huo wilayani
humo, Edson Kagaruki alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari mjini hapa, huku akiwataka walengwa walioibuliwa kwenye mpango huo
kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na sio kunywea pombe au kuongeza
idadi ya wake majumbani kwao.
Kagaruki alisema, baada ya zoezi la uandikishaji na usajili
waliweza kuibua kaya hizo kutoka katika vijiji 42, ambavyo viliingizwa kwenye
mpango huo wa awamu ya tatu.
Alisema kuwa serikali kupitia mpango wa TASAF, imekuwa ikitoa
ruzuku ya msingi na ile ya masharti nafuu kwa kaya hizo na familia zinazoishi
katika mazingira hatarishi, ili ziweze kumudu kupata mahitaji yao ya kila siku
na kwamba mpango huo ni wa miaka mitatu ambapo kila kaya, italipwa fedha kwa
miezi miwili miwili.
Ruzuku ya msingi imekuwa ikitolewa kwa kila kaya, ambayo
imeandikishwa kwenye mpango huo na ile yenye masharti nafuu hutolewa kwa kaya
maskini ambazo zina watoto wanaohitajika kwenda shule na wale wanaohitaji
kupata huduma ya matibabu, ambao wana umri chini ya miaka mitano.
Kadhalika kwa kila kaya au familia kupitia mpango huo, huweza
kuboresha maisha yao kwa kuweka akiba, uanzishwaji wa shughuli ndogo ndogo za
kiuchumi ambapo kwa kipindi hicho cha miaka miwili hupatiwa ruzuku ya shilingi
36,000 hadi 65,000 ambazo hutolewa kila baada ya miezi miwili.
Hata hivyo aliongeza kuwa kazi ya uzinduzi wa malipo kwa kaya
hizo ulitekelezwa rasmi Agosti 18 mwaka huu, katika kijiji cha Namtumbo na Mkuu
wa wilaya hiyo Chande Nalicho.
No comments:
Post a Comment