Na Muhidin Amri,
Songea.
WAHITIMU kidato cha nne, shule ya sekondari Beroya iliyopo Manispaa
ya Songea mkoani Ruvuma ambao wanatarajia kufanya mitihani yao ya mwisho, Novemba
mwaka huu wametakiwa kujiepusha na udanganyifu wa kutafuta majibu ya mitihani
hiyo, badala yake watumie muda uliobaki kujisomea ili waweze kufanya vizuri na
kufaulu kwa kupata alama za juu.
Aidha wameelezwa kuwa, serikali tayari imejipanga kudhibiti
vitendo hivyo ili kuwadhibiti wanafunzi wenye tabia hiyo na kwamba wameshauriwa
kutumia muda huu mfupi uliobakia, kujikumbusha yale waliyosoma na kufundishwa
na walimu wao ili siku ya mwisho ya mitihani yao waweze kufuzu vigezo husika.
Ofisa elimu sekondari katika Manispaa hiyo, Leo Mapunda
alisema hayo alipokuwa akizungumza na wanafunzi, walimu na wazazi katika
mahafali ya saba kidato cha nne, shule ya sekondari Beroya yaliyofanyika juzi
mjini hapa.
Alisema kuwa, siri ya mwanafunzi kufanya vizuri katika masomo
na mitihani yake ni kujiandaa kwa kusoma kwa bidii anapokuwa shuleni na
nyumbani, kwa kuzingatia mambo anayofundishwa na walimu wake na sio kukaa na
kusubiri kupata majibu kwa njia haramu, jambo ambalo wengi wao linawakwamisha
kufikia ndoto yao.
Mapunda alifafanua kwamba, kitendo cha kuzingatia yale
yanayofundishwa darasani kunamwezesha mtoto kujiamini katika kujibu mitihani
yake ya mwisho kwa ubora wa hali ya juu, na wale ambao wamezoea kutumia njia za
mkato hubaki wakihangaika kutafuta majibu ya mitihani, kutoka kwa matapeli
ambao huibuka kwa wingi pale mitihani inapowadia kufanyika.
“Leo ninyi vijana wangu mnaomaliza kidato cha nne napenda
kuwaeleza kwamba, siri kubwa ya kufanya vizuri katika mitihani ni kusoma kwa
juhudi na maarifa ya hali ya juu, ili siku ya mwisho muweze kujibu mitihani yenu
vizuri pasipo shaka”, alisema Mapunda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shule hiyo Sebastian Waryuba alisema
kuwa kwa muda wa miaka minne sasa vijana hao wamefundishwa misingi muhimu ambayo
kama wataizingatia na kuyafanyia kazi, wataweza kufanya vyema katika mitihani
yao na hata katika maisha yao ya kila siku huko waendako.
Waryuba aliwataka pia watoto hao wasibweteke na elimu ya
kidato cha nne ambayo wameipata, badala yake iwe mwanzo wa kujiendeleza zaidi
jambo ambalo litaweza kukamilisha ndoto ya maisha yao.
Aliwataka kwenda kuwa mfano mzuri katika jamii, ili watu
wengine waweze kuiga mambo mazuri kutoka kwao badala ya kushiriki katika
matendo maovu ambayo hayaleti picha nzuri, kwao na jamii kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment