Na Mwandishi wetu,
Tunduru.
KUFUATIA kuendelea kuwepo kwa matukio ya wagonjwa wanaolazwa
katika Hospitali ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, kuwapiga waganga na
wauguzi wa hospitali hiyo Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo,
ameuagiza uongozi husika kuhakikisha kwamba, vitendo hivyo vinadhibitiwa mara
moja.
Sekambo alitoa agizo hilo akiwataka wafanyakazi wa hospitali
hiyo, kuzingatia maadili ya kazi zao za kila siku ili waweze kuepukana na migongano
isiyokuwa ya lazima kati yao na wagonjwa, wanaokwenda kupatiwa matibabu
hospitalini hapo.
“Nimekwisha waagiza viongozi wa hospitali hii, wakae pamoja
na kuona wapi kuna tatizo, yawezekana baadhi yao wamekuwa hawatimizi majukumu
yao ya kazi ipasavyo ndio maana kumekuwa na matatizo ya kutoelewana, kati ya
wafanyakazi wa hospitali na wagonjwa”, alisema Sekambo.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa katika hali ya kawaida,
haiwezekani mgonjwa achukue hatua ya kumpiga muuguzi wake, bila kuwepo kwa
sababu yoyote ile hivyo, lazima kuwepo na jambo ambalo limejitokeza miongoni
mwao.
Pamoja na mambo mengine, uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa
habari hizi umebaini kuwa matatizo hayo katika hospitali ya Tunduru yanatokana pia
na baadhi ya wafanyakazi wake kutotimiza majukumu ya kazi zao ipasavyo, ndio
maana kumekuwa na migongano kati yao na wagonjwa.
Nimezungumza kwa nyakati tofauti na baadhi ya wagonjwa
wanaokwenda kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo, walidai kuwa jambo hilo
limekuwa ni tatizo sugu linaloendelea kuwatesa pale wanapohitaji matibabu
hospitalini hapo, na kwamba wanaiomba serikali kuingilia kati ili kuweza
kunusuru hali hiyo.
Hata hivyo Mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Tunduru,
Dokta Zabron Mmari juu ya madai hayo alithibisha hilo na kusema kuwa hatua
zitachukuliwa kwa mganga au muuguzi, atakayekiuka maadili ya kazi ili iwe
fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
No comments:
Post a Comment