Monday, October 12, 2015

AUAWA NA TEMBO AKIWA SHAMBANI

Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKAZI mmoja ambaye ni wa kijiji cha Kalulu, wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, Said Athuman (42) amefariki dunia baada ya kushambuliwa na Tembo, wakati akiwa shambani kwake.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, walisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 29 mwaka huu, majira ya jioni baada ya kundi la Tembo kujitokeza na kumvamia.

Alifa Abdalah Said ambaye ni Kaka wa marehemu huyo, alisema chanzo cha tukio hilo kilitokana na maafisa wa idara ya wanyama pori ambao wanalinda wanyama katika kituo cha hifadhi Kalulu kilichopo kwenye hifadhi ya taifa ya Selous, walikuwa wakiwafukuza Tembo hao katika maeneo waliyokuwepo, ndipo walikimbilia shambani huko na kusababisha mauaji.


Wakati tukio la kuwafukuza wanyama hao likitekelezwa, alisema kuwa walivamia pia katika maeneo ya makazi ya watu, ambapo Tembo wengine walitawanyika na kuingia katika mashamba na hatimaye kufika katika shamba la marehemu huyo na kumuua.

Akizungumzia tukio hilo, afisa ardhi na maliasili wa wilaya ya Tunduru, Japhet Mnyagala pamoja na kuthibitisha kuwepo kwa tukio hilo alisema kuwa tayari wamepeleka kikosi kazi cha askari wa kitengo hicho, kwa lengo la kuwatawanya ili kuleta usalama kwa wakazi wa kijiji hicho.

"Ni kweli kulikuwa na zoezi la maafisa wa kituo cha Kalulu, ambao wanasaidiana na askari wa Jumuiya ya ulinzi shirikishi wanyama pori vijijini (VGS) katika kuwafukuza Tembo hawa, kutoka maeneo ya makazi ya watu”, alisema.

Mnyagala alifafanua kuwa chanzo cha wanyama wengi, wakiwemo wale wakali wamekuwa wakikimbia katika mapori kutokana na maeneo yao kuvamiwa na wawindaji haramu, pamoja na uwepo wa makundi ya wafugaji.

Alisema kufutia hali hiyo, idara yake imejipanga kwa ajili ya kufanya doria za kupambana na majangiri hao pamoja na kuwahamisha wafugaji, waliovamia katika mapori ya hifadhi.
Mganga aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Athuman, Dokta Gaofrid Mvile alisema chanzo cha kifo hicho, kilisababishwa na kutokwa na damu nyingi maeneo mbalimbali ya mwili wa marehemu huyo.


Katika tukio hilo, alisema marehemu aliumia vibaya kichwani na kifuani maeneo ambayo yalipondwa pondwa na kusababisha viungo vya ndani vya mwili wake, ikiwemo kichwa kusagika kabisa.

No comments: