Na Steven Augustino,
Tunduru.
WANUFAIKA katika mradi wa uhawilishaji fedha, kaya maskini wilayani
Tunduru mkoa wa Ruvuma, ambao unatekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
Tanzania (TASAF) awamu ya tatu, wameishukuru serikali ya awamu ya nne kwa
kubuni na kuwapelekea mradi huo.
Aidha wanufaika hao, wametaja baadhi ya miradi ambayo
wameianzisha na kuanza kuwaletea maendeleo katika maisha yao baada ya kupokea fedha
kutoka TASAF kuwa ni ufugaji wa mbuzi, kondoo, kuku, kanga, bata, matibabu
pamoja na kununua vifaa vya ujenzi wa nyumba zao.
Wananchi hao walitoa shukrani hizo, walipokuwa kwenye
mahojiano maalum na mwandishi wetu ambaye alitembelea vijiji vya Mbesa, Nalasi,
Mchoteka, Tunduru mjini na Namasakata wilayani humo.
Wakifafanua maelezo yao kwa nyakati tofauti, wanufaika hao
walisema tangu kuanzishwa kwa mradi huo hadi sasa baadhi yao wameweza kumudu
gharama za maisha ikiwemo kujikwamua na umaskini waliokuwa nao, ikiwemo
kupeleka watoto wao shule.
Mohammed Ponera wa kijiji cha Mbesa na Sheila Salum kwa nyati
tofauti walidai kuwa, mradi huo umewawezesha kumiliki wastani wa mbuzi wanne
hadi sita kila mmoja wao na kuanza kuuaga umaskini uliokithiri miongoni mwao
kwa muda mrefu.
Wengine waliohojiwa katika ufuatiliaji wa mradi huo,
ni pamoja na Mwanahawa Daimu wa kijiji cha Mbesa, Siwema khalfan
wa kijiji cha Nalasi, Siwema Rashid wa Kijiji cha
Mchoteka na Mohammed Alifa wa Kijiji cha Nakayaya walisema kuwa
mradi huo umewanufaisha kutokana na kuanza kufuga kuku na bata ambao wameanza
kuuza mazao yatokanayo na mifugo hiyo.
Walibainisha kuwa hapo awali hawakuwa na uwezo wa kufuga hata
kifaranga kimoja cha kuku, hivyo mfuko huo umewafanya kila mmoja wao kumiliki
kati ya kuku 40 hadi 60, bata, kati ya 50 na 70 pamoja na kanga ambao walidai
kuwa na idadi tofauti jambo ambalo linawapa faraja na ni hatua nzuri kimaendeleo
katika maisha yao.
Sambamba na fedha za TASAF kuwasaidia kuanzisha ufugaji huo,
pia zimekuwa zikiwasaidia kusomesha watoto wao shule ikiwa ni pamoja na
kuwanunulia sare, daftari, kalamu na mahitaji mengine muhimu ya mtoto.
Ayesi Linyomwa wa kijiji cha Namasakata alitoa ushuhuda wake
akisema, fedha hizo zimemsaidia kujenga nyumba, anafuga kuku, pamoja na kuendeleza
shamba lake la mikorosho ambalo awali lilikuwa lina hali mbaya kutokana na kushindwa
kulihudumia.
Mkazi wa kitongoji cha Ajika kijiji cha Mbesa, Chinunga Said naye
alisema kuwa pamoja na kuanza kumiliki mbuzi na kuku lakini fedha hizo
zilimsaidia kumuuguza kijana wake, ambaye alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa
kichaa.
Wakizungumzia changamoto ambazo wamekuwa wakizipata wakati wa
ugawaji wa fedha hizo, baadhi ya wataalamu kutoka TASAF walisema kuwa awali
kulikuwa na matatizo ya wateja hao kurukwa na kompyuta jambo ambalo lilikuwa
likileta malalamiko ya hapa na pale na sasa limefanyiwa kazi na hakuna tena
usumbufu wa aina yoyote ile.
Wawezeshaji kutoka katika mfuko huo wilayani Tunduru, Muhidin Shaibu
na Twaha Nang'onde waliwaasa wanufaika hao kuanzisha vikundi vya ujasiriamali
ambavyo vitatumika kukopeshana fedha bila riba, ili fedha wanazopata ziendelee
kuwanufaisha hata baada ya mradi huo kwisha.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Ofisa mshauri na
mfuatiliaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri wilaya ya Tunduru, Christian
Amani alisema jumla ya shilingi bilioni 2,850,708,702.06 zimelipwa kwa awamu,
kwa wanufaika 60,412 waliopo katika kaya 15,012 zilizoainishwa tokea mradi huo uanzishwe.
Kwa mujibu wa takwimu za wanufaika hao, kati yao wanaume
22,412 na wanawake 38,000 ambao kati yao wanapokea ruzuku ya msingi, ruzuku ya
masharti ya elimu na afya.
Alisema malipo hayo ni miongoni mwa malengo makuu ya TASAF,
awamu ya tatu na lengo ni kuiwezesha jamii kuondokana na umaskini uliokithiri
kwa kujenga rasilimali watu, kupitia elimu na afya kwa watoto.
Pamoja na mambo mengine, Amani aliwaasa wanufaika wahakikishe
kwamba fedha wanayoipata wanaitumia katika malengo husika na endelevu, ili
mradi huo utakapofikia hatua ya mwisho walengwa waendelee kufaidi matunda.
Hata hivyo aliwahakikishia walengwa hao kuwa, mfuko
huo utawasaidia katika mchakato wa kurasimisha vikundi vyao vya uzalishaji
mali, ambavyo wamevianzisha pamoja na kuwawezesha kufikia maendeleo kwa kila
mnufaika aliyekuwa katika mradi.
No comments:
Post a Comment