Na Steven Augustino,
Tunduru.
WAPENZI na wakereketwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la
Tunduru Kusini mkoani Ruvuma, wamemfananisha mgombea ubunge wa jimbo hilo, Daimu
Mpakate kuwa ni sawa na jembe na pembejeo za kilimo, ambavyo
wamekuwa wakivitabikia kwa muda mrefu jimboni mwao.
Wananchi wenye bendera za chama hicho, walikuwa na
mabango yenye kubeba ujumbe wa aina mbalimbali ambao ulikuwa
ukimuunga mkono mgombea huyo, huku wakiimba nyimbo za
kumpongeza kuchaguliwa kwake, kuwa mgombea wa ubunge kwa tiketi ya chama hicho.
Hayo yalibainishwa kwa vitendo kutokana na wananchi hao, pale
walipojitokeza kwa wingi huku wakiwa wameinua mabango hayo ambayo yalikuwa
na ujumbe wakumpa moyo mgombea, kwamba watamchagua kwa kumpatia kura zaidi ya asilimia
zaidi ya 80.
Baadhi yake yalikuwa na ujumbe yakisema, “Mpakate umethubutu,
unaweza, tunakukubali, tunakuamini, ukitaka mabadiliko chagua CCM,
tunaimani na Mpakate kero yetu ya zao la korosho itakwisha, Mpakate
wewe ni jembe, pembejeo za kilimo zitafika kwa wakati”.
Aidha toka kampeni za kuwania nafasi hiyo, tokea zianze
kutimua vumbi katika jimbo hilo kwa mara ya kwanza Mpakate
alipata mapokezi makubwa yaliyoweza kufananishwa na gharika, kutokana na
idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza kumlaki na kumsikiliza kwanye
mkutano wake wa kampeni, uliofanyika kwenye viwanja vya mikutano
vya makaoni vilivyopo katika kijji cha Lukumbule wilayani Tunduru mkoani hapa.
Katika mkutano huo mgombea huyo, aliwashukuru wananchi waliojitokeza
na kuvunja rekodi ya vyama vingine vya siasa wilayani humo, kwamba havijawahi
kupata umati mkubwa wa watu katika kampeni zao na kwamba hizo ni salamu kuwa jimbo
lake halihitaji viongozi wa upinzani.
Kufuatia hali hiyo Mpakate aliwataka wanchi wa jimbo la
Tunduru Kusini, kupuuza kelele za wapinzani na akawataka kujitokeza kwa wingi
kumchagua mgombea urais wa CCM, mbunge na diwani ili waweze
kuwaletea maendeleo ya kweli na kwamba yeye ni mtetezi wa wanyonge, na
anazifahamu kero zinanazo wakabili wananchi wa jimbo hilo.
Mpakate alitamba kuwa Chama cha mapinduzi, endapo kitachukua
nafasi ya ushindi ya kuongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo
kitajikita zaidi katika kuimarisha miundombinu ya elimu, kilimo, afya,
maji na michezo ambavyo vimeainishwa kusimamiwa katika ilani ya chama
chake katika kipindi hicho.
Naye Mwenyekiti wa Chama hicho wilaya ya Tunduru, Hamis
Kaesa aliwaomba wananchi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi siku ya
kupiga kura na kuwachagua wagombea waliosimamishwa na chama chake, kwa
kuwapatia kura nyingi za ndiyo ili waweze kuwaongoza katika kipindi cha
serikali ya awamu ya tano chini ya Dokta John Magufuli.
Kadhalika Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi ya CCM wilayani
humo, Said Mkandu aliwaasa wananchi wajimbo hilo wasiwachague viongozi wa UKAWA kwa
kile alichodai kuwa wamesambaratika na hawawezi kuleta maendeleo
wilayani humo na Taifa kwa ujumla.
Vilevile kiongozi kimila wa makabila ya Wayao kutoka kijji
cha Lukumbule, Mwenye Kanyinda alimhakikishia
mgombea ubunge katika jimbo hilo, Mpakate kuwa wananchi watampigia kura nyingi.
Aidha Mwenye Kanyinda alimuomba mgombea huyo, atakapoingia
madarakani ahakikishe katika tarafa ya
Lukumbule anawajengea kituo kidogo cha Polisi ili waweze
kuishi kwa amani, tofauti na ilivyo sasa ambapo wamekuwa wakiishi kwa mashaka
kutokana na kuwa mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.
No comments:
Post a Comment