Na Steven Augustino,
Tunduru.
CHAMA cha Wananchi (CUF) wilaya
ya Tunduru mkoani Ruvuma, kimelaani vikali kitendo cha
kuchanwa mabango ya mgombea wake wa udiwani kata ya Mlingoti Mashariki,
Mohamed Nyoni.
Kwa mujibu wa taarifa za tukio hilo, zinaeleza kuwa zaidi ya
mabango 300 yamechanwa na vijana wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) na kwamba mabango hayo, yalikuwa yamebandikwa katika maeneo
mbalimbali ya kata hiyo.
Sambamba na kuchanwa kwa mabango hayo, pia taarifa hizo
zinasema kuwa watu hao walichana mabango ya mgombea wao wa
ubunge jimbo la Tunduru Kaskazini, anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA) Manjolo Kambili.
Madai hayo yalitolewa na Mkurugenzi wa siasa
wa Chama Cha Wananchi (CUF) wilaya ya Tunduru, Said Kiosa
wakati akiwahutubia wananchi wa kata ya Masonya kijiji cha Nakayaya Mashariki, mjini
hapa.
Alisema kuwa kumekuwa na hujuma
zinazofanyika, kwa lengo la kuwatishia wananchi wasishiriki mikutano
ya kampeni ya Ukawa huku mabango yakichanwa.
Kiosa aliwataja kwa majina baadhi ya vijana
wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi, ambao walichana mabango hayo
ni, Mohamed Kumpinduka na Shaibu Mambulu.
Kufuatia hali hiyo, aliutaka uongozi wa Jeshi la Polisi
wilayani Tunduru kuwakamata na kuwachukuria hatua ili iwe fundisho
kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Revocatus Malimi amethibitisha
kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kuwa Polisi wanaendelea na uchunguzi juu ya
tukio hilo, ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
No comments:
Post a Comment