Na Steven Augustino,
Tunduru.
MKAZI mmoja wa kitongoji cha Makombe kijiji cha Milonde kata
ya Matemanga wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, Mohamed Mawazo (43) anashikiliwa
na Polisi kwa tuhuma ya mauaji.
Taarifa za tukio hilo, zinasema kuwa mtuhumiwa huyo
anashikiliwa akidaiwa kumuua Zuberi Issa kutokana na kipigo alichokipata kutoka
kwa mtuhumiwa huyo ambaye alimpiga kwa kutumia mchi wa kutwangia, kutokana na wivu
wa kimapenzi.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Revocatus Malimi. |
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mtuhumiwa huyo alifanya kosa hilo
kwa kumtwanga nao kichwani kitendo ambacho kilimsababishia kufikwa na mauti.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Revocatus Malimi alisema
kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa Oktoba 16 mwaka huu.
Alisema baada ya mtuhumiwa huyo kufanya shambulizi hilo,
alikwenda kuripoti kwa Mwenyekiti wa kitongoji cha Makombe, Said Mussa huku
akitamba kuwa tayari amekwisha mpiga mtu aliyekuwa anamtuhumu kwamba anatembea
na mke wake, ambaye ni miongoni mwa wake zake watatu.
Baada ya kiongozi huyo kupewa taarifa hizo, alichukua jukumu
la kwenda kufuatilia tukio hilo kwa kushirikiana na ndugu wa jirani na marehemu
huyo ambapo walimkimbiza Hospitali ya Kanisa la Upendo wa Kristu Kiuma, ambako baadaye
alifariki akiwa anapatiwa matibabu.
Alisema baada ya kifo hicho, Mwenyekiti huyo wa kitongoji
alitoa taarifa Polisi ambapo jitihada za kumtafuta mtuhumiwa zilifanikiwa, ambaye
awali alikuwa amekimbia lakini alikamatwa.
Kamanda huyo wa Polisi, amewaasa wananchi kuachana na tabia
za kuchukua sheria mkononi, kwani kufanya hivyo ni kosa la jinai.
Mganga aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, Zuberi Issa (36),
Dokta Gaofrid Mvile alisema chanzo cha kifo hicho kilisababishwa na
kuchanganyika kwa damu na ubongo, kulikosababishwa na kupasuka kwa fuvu
la kichwa chake.
Alisema katika tukio hilo marehemu, aliumia vibaya sehemu ya
nyuma katika kichwa chake.
No comments:
Post a Comment