Na Muhidin
Amri,
Ruvuma.
OFISA ushauri na ufuatiliaji, Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii (TASAF) hapa nchini wilaya ya Namtumbo mkoani
Ruvuma, Edson Kagaruki amekanusha taarifa
za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa wilayani humo, kwamba mfuko
huo unafanya kazi ya kuhawilisha fedha kwenda kaya maskini, kwa lengo la
kukisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kiweze kushinda katika uchaguzi mkuu
utakaofanyika, Oktoba 25 mwaka huu.
Kufuatia maneno hayo, Ofisa huyo wa TASAF wilayani humo amewataka wanasiasa hao kuacha
porojo hizo na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali, katika
kupambana na umaskini hapa nchini.
Aidha amewakumbusha kutumia majukwaa ya kisiasa, kueleza sera
zao na sio kuwapotosha wananchi kwa mambo ambayo hayana msingi, jambo ambalo linaweza
kuchochea uhasama katika jamii.
Kagaruki alisema kuwa amechukua jukumu la kutoa ufafanuzi huo,
baada ya kuwepo kauli kutoka kwa baadhi ya wanasiasa wilayani Namtumbo
wanaodai kuwa, Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF III) ni njama na ujanja
wa Chama cha Mapinduzi kutaka kujiweka karibu na wapiga kura, ili wakichague
katika uchaguzi huo.
Alifafanua kuwa madai hayo hayana ukweli wowote, kwani mpango
huo unalenga kunusuru kaya maskini na tokea uanzishwe hapa Tanzania una zaidi
ya miaka mitatu, na baadhi ya wananchi kupitia Halmashauri husika wamewezeshwa
kupitia mpango huo.
Kwa mujibu wa Kagaruki alieleza kuwa TASAF, ilianza kazi zake
siku nyingi katika maeneo mbalimbali hapa nchini katika awamu tatu na haina
uhusiano wowote na chama cha siasa, zaidi ya kuboresha maisha ya Watanzania
waliowengi ambao wanakabiliwa na matatizo mbalimbali.
Alifafanua kuwa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo, ina vijiji
42 ambavyo vipo kwenye mpango wa uhawilishaji fedha na tayari malipo ya awamu
ya pili yameshafanyika, Septemba 28 mwaka huu.
Mbali na hilo, alisema katika vijiji hivyo jumla ya kaya 5,652
ambazo zilikidhi vigezo na kuingizwa katika mpango wa kunusuru kaya maskini, vilipewa
fedha ambazo zitawawezesha kupunguza ukali wa maisha katika familia zao.
Alisema kuwa Halmashauri hiyo, itatumia kiasi cha
shilingi milioni 237,577,500.00 ili kufanikisha zoezi zima, la
malipo kwa walengwa.
Kwa upande wake Mratibu wa TASAF wilaya ya Namtumbo,
Raphael Mponda alisema kupitia mpango huo walengwa, hupata ruzuku ya msingi na
wengine ya kutimiza masharti.
Alifafanua kuwa ili kaya yenye watoto iweze kupata ruzuku,
lazima watoto waliochini ya miaka mitano wapelekwe Kliniki na kupata huduma za
afya kwa asilimia mia moja, na wale walio na umri wa kwenda shule wanatakiwa
kuhudhuria masomo yao kwa kiwango kisichopungua asilimia 80 ya siku zote za
masomo.
Fedha hizo za malipo kwa kaya masikini, hufanyika kila baada
ya miezi miwili na kwamba matumaini yake kupitia mpango huo walengwa wataweza
kuboresha maisha yao, kuweka akiba na kuanzisha shughuli mbalimbali za kuinua
uchumi katika kaya zao.
No comments:
Post a Comment