Friday, October 9, 2015

POLISI WATOA ONYO SIKU YA UCHAGUZI MKUU

Na Muhidin Amri,
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma limesema kwamba, halitakuwa tayari kuona amani na utulivu vikivurugwa hasa katika kipindi hiki cha kampeni na kuelekea siku ya kupiga kura, kutokana na sababu za itikadi za kisiasa.

Kauli  hiyo  imetolewa jana na Kaimu Kamanda wa  Polisi wa mkoa huo, Revocatus Malimi alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na hali ya usalama ya wananchi, kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika oktoba 25 mwaka huu.

Malimi alisema Jeshi hilo limejiandaa vya kutosha kuhakikisha kwamba, uchaguzi wa mwaka huu unaendeshwa kwa amani na utulivu, katika maeneo mbalimbali mkoani humo mpaka siku ya mwisho ya upigaji  kura.


“Tutahakikisha ndani ya mkoa wetu amani na utulivu vinaendelea kutawala, ili kutoa nafasi kwa wananchi mara baada kumaliza kuwachagua viongozi wao waendelee na shughuli nyingine za uzalishaji mali, katika maeneo yao wakiwa salama”, alisema Malimi.

Alisema kuwa ni vyema kila mmoja, kuanzia wagombea  wenyewe na wafuasi wao waheshimu sheria na taratibu zilizowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kuepusha uwezekano wa kutokea vurugu, ambazo itakuwa kero kwa watu wengine.

Mbali na hilo Malimi amewataka  watu wote kuwa watulivu, kipindi  chote cha kampeni na siku ya kupiga kura kwa kile alichoeleza kuwa kumekuwa na baadhi ya watu wachache, wanaweza kutumia nafasi hiyo kuona kama wana uhuru wa kufanya kila jambo wanalolitaka huku wakijua wanavunja sheria.

Aliongeza kuwa vurugu katika uchaguzi wa mwaka huu, hazina nafasi hivyo anawakumbusha wananchi kufuata maelekezo yanayotolewa na vyombo husika vya serikali, pale watakapobaini kuna kasoro  na ukiukwaji wa kanuni na taratibu za uchaguzi, na sio kufanya vurugu.


Pia ametoa mwito kwa vyombo vya habari katika mkoa huo, kuacha uchochezi badala yake viwe sehemu ya kufanikisha uchaguzi huo huku akionya kwamba Jeshi la Polisi  halitakuwa na huruma kwa mwandishi yeyote, ambaye atakuwa chanzo cha  kuvuruga uchaguzi huo na kuhatarisha amani iliyopo kwa maslahi yake binafsi.

No comments: