Na Steven Augustino,
Ruvuma.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) katika wilaya ya Tunduru na Songea
mkoani Ruvuma, kimeendelea kung’ang’ania majimbo yake na kata kwa ujumla baada
ya wagombea wake kwa nafasi ya diwani, ubunge na rais kuongoza kwa kura nyingi.
Wakitangaza kwa nyakati tofauti wasimamizi wa uchaguzi katika
majimbo ya Tunduru Kusini, Kaskazini na Songea walisema kuwa wagombea wa chama
hicho ndio walioibuka kidedea katika matokeo ya uchaguzi huo, uliofanyika
Oktoba 25 mwaka huu.
Wilayani Tunduru msimamizi wa uchaguzi, Mkurugenzi mtendaji wa
Halmashauri ya wilaya hiyo, Tinna Sekambo aliwatangaza Daimu Mpakate kupitia
Chama Cha Mapinduzi kuwa mshindi wa nafasi ya ubunge, jimbo la Tunduru Kusini
baada ya kupata kura 27,486.
Alisema katika matokeo hayo, Mpakate aliwashinda wapinzani
wake Sadick Songoni wa Chama Cha Wananchi (CUF) kupitia muungano wa vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) aliyepata kura 16, 620 na Ally Abdallah,
ACT Wazalendo aliyepata kura 1,026.
Kwa upande wa jimbo la Tunduru Kaskazini, Sekambo alimtangaza
Mhandisi Ramo Makani (CCM) kuwa mshindi kwa kupata kura 29,841 na kuwashinda
Manjoro Kambili (CUF) aliyepata kura 29,102 na Mohammed Alifa, ACT wazalendo
aliyepata kura 856.
Katika jimbo la Songea mjini msimamizi wa uchaguzi, Lahari
Kimari alimtangaza Leonidas Gama (CCM) kuwa mshindi baada ya kupata kura 40,886
na kuwashinda Fuime Joseph (CHADEMA) aliyepata kura 37,012 na kwamba upande wa
matokeo ya udiwani Chama Cha Mapinduzi, kimeibuka na ushindi katika kata 16
kati ya 21 zilizopo kwenye jimbo hilo ambapo kata 5 zimechukuliwa na vyama vya
upinzani.
No comments:
Post a Comment