Na Steven Augustino,
Tunduru.
TIMU ya soka, Mambo Mazuri FC ya Tunduru mjini mkoani Ruvuma,
imeibuka kidedea kupitia ligi ya Polisi Jamii, baada ya
kuwafunga mahasimu wao, Vampire FC magoli manne kwa matatu katika
mchezo mkali, uliorindima kwenye uwanja wa Chama Cha Mapinduzi mjini hapa.
Kutokana na matokeo hayo, Vampire FC imeambulia nafasi ya
pili na mshindi wa tatu katika mashindano hayo ikachukuliwa na Jobe FC.
Kulingana na maelekezo yaliyotolewa na Mratibu wa mashindano
hayo, Inspector Songelael Jwagu mshindi wa kwanza katika mashindano
hayo atazawadiwa kikombe, seti moja ya jezi na mpira mmoja wa miguu.
Inspector Jwagu alifafanua kuwa, mshindi wa pili atapata
zawadi ya seti moja ya jezi na wa tatu atajinyakulia mpira mmoja wa miguu.
Alisema jumla ya timu 12 zilishiriki katika mashindano hayo,
ambapo kati yake timu 16 zilitolewa katika ligi ya mtoano iliyochezwa na
kubakia timu nane.
Kadhalika alizitaja timu zilizoendelea na ligi hiyo katika
mzunguko wa pili kuwa ni Joker FC, Tunduru Seko Fc, Usalama FC, Mambo
mazuri FC, Veterani FC, Jobe FC, Tunduru City na Vampire FC.
Aidha katika taarifa hiyo pia alizitaja timu zilizoshiriki na
kutolewa katika mzunguko wa kwanza kuwa Frank FC, Red Scud FC, Nakayaya FC,
Mgomba FC, River Kombaini FC, Fridom FC na Joker FC.
Wakati wa makabidhiano ya zawadi hizo kwa washindi hao,
Kamanda wa Polisi wilayani Tunduru, Nicholaus Mwakasanga alisema pamoja na
mashindano hayo kutoa ujumbe wa Polisi jamii na kuwataka wananchi kushiriki
katika mpango wa ulinzi shirkishi, pia alizitaka timu hizo kucheza michezo ya
kupendana, kushirikiana kwa kile alichoeleza kuwa michezo ni furaha.
Kamanda Mwakasanga aliwataka vijana kuachana na vitendo vya
matumizi ya madawa ya kulevya, kufanya matukio ya uhalifu na kukataa kutumiwa
na wanasiasa ambao wamekuwa wakiwashawishi na kuwatumia vibaya katika kufanya
maandamano, bila kufahamu chanzo chake hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi
mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment