Na Kassian Nyandindi,
Songea.
KUNDI la watu linalodaiwa kuwa ni la wafuasi wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) limevamia eneo la soko la wakulima
lililopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma, na kung’oa kisha kuchana bendera 50 za Chama
Cha Mapinduzi (CCM) zenye thamani ya shilingi 200,000 kutokana na chuki za
kisiasa zilizopo wilayani humo.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake, Kamanda wa Polisi
mkoani humo, Mihayo Msikhela alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya
asubuhi huko wilayani Mbinga.
Alifafanua kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio, kundi hilo lilikwenda
kwenye eneo hilo na kufanya vurugu kisha kungo’a milingoti iliyowekwa bendera
na kuzichana jambo ambalo lilisababisha kuwepo kwa vurugu kubwa kati ya wafuasi
wa CHADEMA na wa CCM.
Alisema kuwa wakati vurugu hizo zinaendelea, taarifa za tukio
hilo zilikuwa tayari zimeshafika kwenye Kituo kikuu cha Polisi Mbinga na ndipo
askari walijipanga na kwenda kwenye eneo la tukio, ambako walifanikiwa
kuwatawanya watu waliokuwa wakileta vurugu.
Kadhalika baadaye Polisi walilazimika kutumia mabomu kwa
lengo la kuwatawanya watu hao waliokuwa wanaleta vurugu, ambapo hakuna madhara
yoyote yaliyotokea.
Hata hivyo Polisi walifanikiwa kuwakamata watu watatu, ambao
ndio inadaiwa walikuwa vinara wa kuanzisha vurugu hizo ambapo aliwataja kuwa ni
Meshack Komba (26) mkazi wa Matarawe Mbinga mjini, Michael Ndimbo (20) ambaye
ni dereva wa boda boda na Bushiri Mterera (30) wote wakazi wa Furaha Store.
Kamanda Msikhela alisema kuwa hivi sasa, jeshi la Polisi
mkoani humo linaendelea kuwasaka wafuasi wengine wa CHADEMA ambao inadaiwa
walishiriki kufanya uhalifu kwenye eneo la soko la wakulima, na kusababisha
kutokea kwa hasara.
No comments:
Post a Comment