Injinia Stella Manyanya |
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.
TAARIFA zilizotufikia hivi punde Jimbo la Nyasa lililopo wilayani
Nyasa mkoa wa Ruvuma, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea kuongoza na
kupeperusha bendera yake kwa nafasi ya kiti cha udiwani, ubunge na rais dhidi
ya vyama vya upinzani.
Mkurugenzi msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Jabir
Shekimweri amezungumza na mwandishi wa habari hizi na kueleza kwamba kwa nafasi
ya udiwani, mpaka sasa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeweza
kuchukua kata mbili kati ya 18 zilizopo wilayani humo na matokeo kwa ngazi hiyo
ya udiwani, bado yanapokelewa kutoka katika kata mbalimbali.
Alisema jimbo la Nyasa lina idadi ya wapiga kura 70,766 na
kwamba waliojitokeza kupiga kura walikuwa 45,838.
Kwa nafasi ya ubunge, amemtangaza Injinia Stella Manyanya
kupitia tiketi ya CCM kuwa mshindi nafasi ya ubunge ambaye amepata kura 31,548.
Shekimweri alisema kuwa CHADEMA kimepata kura 12,653 kwa
nafasi hiyo ya ubunge ambapo kilimsimamisha mgombea wake, Ngwata Saulo na ACT
Wazalendo kilimsimamisha, Raymond Ndomba aliyepata kura 497.
Kwa nafasi ya mgombea urais uchunguzi wetu umebaini kuwa
jimbo la Nyasa, Chama Cha Mapinduzi kimejizolea kura nyingi na kufanya hata
baadhi ya maeneo mbalimbali jimboni humo wapiga kura wakiwa wanasherehekea juu ya
ushindi huo.
Nafasi ya rais Mkurugenzi huyo amesema yeye hana mamlaka ya
kutangaza badala yake, wanayapeleka katika ngazi husika ili yaweze kutangazwa.
Pamoja na mambo mengine, licha ya wilaya ya Nyasa kukabiliwa
na changamoto ya miundombinu ya barabara wasimamizi wa uchaguzi wameweza
kuwasilisha matokeo husika, huku ya ngazi ya udiwani yakiwa bado yanaendelea
kukusanywa kutoka katika kila kata na kwamba uchaguzi umefanyika kwa amani na
utulivu hakuna dosari yoyote iliyojitokeza.
No comments:
Post a Comment