Na Kassian
Nyandindi,
Ruvuma.
HALI ya uchaguzi katika Jimbo la Mbinga mjini na vijijini
mkoani Ruvuma, limeendeshwa kwa amani na utulivu, huku wananchi ambao ni wapiga
kura wakijitokeza kwa wingi kupiga kura.
Mwandishi wetu ambaye ametembelea katika maeneo mbalimbali ya
vituo vya kupigia kura, ameshuhudia hali ikiwa shwari licha ya kuwepo kwa changamoto
ndogo ndogo wakati zoezi hilo linaendeshwa.
Changamoto hizo ni kwamba baadhi ya wafuasi wa vyama vya
siasa, ambao wanadaiwa kutoka vyama vya upinzani, walikuwa wakionekana katika
vituo wakifanya kampeni na kupiga kelele.
Hali hiyo imeshuhudiwa katika kata ya Mpepai na Mbangamao jimbo la Mbinga mjini,
ambapo askari wa kikosi cha kutuliza ghasia, walikwenda huko na kufanikiwa
kuzima kelele hizo.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela amethibitisha
juu ya tukio hilo na kuongeza kuwa katika kata hizo kulikuwa na zomea zomea
zenye kuashiria vurugu, lakini walifanikiwa kudhibiti na kuwatawanya wafuasi
hao.
Uchunguzi uliofanywa na mtandao huu, kwa mujibu wa sensa ya
idadi ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2012 wilaya ya Mbinga inakadiriwa
kuwa na jumla ya watu 385,354.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, Jimbo la Mbinga mjini lina idadi
ya watu 129,537 na vijijini kuna watu 255,817.
Mbinga mjini kuna idadi ya wapiga kura 61,833 likiwa na kata
19 na vituo vya kupigia kura 165 na kwamba kwa vijijini, kuna idadi ya wapiga
kura 110,468 kata 29 vituo vya kupigia kura 312.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotufikia hivi punde, katika
majimbo hayo mpaka sasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaongoza katika majimbo hayo,
kwa ngazi ya diwani, ubunge na rais vikifuatiwa na vyama vingine.
Hata hivyo, Tume ya uchaguzi inaendelea na taratibu za
kujumlisha kura husika ambapo imeweka kambi na kufanya kazi hiyo, katika kituo
cha utafiti wa kahawa TaCRI – Ugano Mbinga mjini na matokeo yanatarajiwa kutangazwa
muda wowote kuanzia sasa, baada ya taratibu husika kukamilika.
No comments:
Post a Comment