Anna Mghwira mgombea urais kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo, akiwa katika moja ya mikutano yake ya kampeni hapa nchini. |
Na Steven
Augustino,
Tunduru.
WANANCHI wilayani
Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameshauriwa kufanya mabadiliko kwa kuchagua wagombea
kutoka vyama vya upinzani ifikapo Oktoba 25 mwaka huu, ili waweze kuwaletea
maendeleo yenye kasi ya ajabu kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
Mgombea urais,
Jamuhuri ya muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo, Anna
Mghwira alisema hayo alipokuwa akizungumza na maelfu ya wananchi ambao
walijitokeza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Baraza la Idd
mjini hapa.
Aidha mgombea
huyo alipokuwa akizungumza na wananchi hao, aliahidi kuunda serikali ya umoja
wa kitaifa akidai kwamba lengo lake kuondoa chokochoko zilizopo, na mitafaruku
ambayo baadaye inaweza kuleta mapigano (Vita) miongoni mwa jamii.
Mghwira alisema
endapo atafanikiwa hilo, serikali yake itashirikisha viongozi wa vyama vyote
vya siasa, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, ya dini, watalaamu na sekta
mbalimbali za kijamii.
Alisema serikali
yake kwa kufanya hivyo, anaamini makundi hayo yataimarisha utendaji kazi kwa
manufaa ya jamii na kulifanya taifa kukua haraka kiuchumi kulingana na
rasilimali husika zilizopo hapa nchini, kama vile gesi na mafuta ambazo
wananchi wanapaswa kunufaika nazo.
Huku
akishangiliwa na maelfu ya wananchi ambao walijitokeza kumsikiliza katika
mkutano huo, mgombea huyo alikuwa akitamba kuwa bila kuwepo kwa vyama vya
upinzani nchi hii, isingeweza kupiga hatua kimaendeleo na kufikia hapa ilipo kwa kile
alichodai kuwa Chama tawala (CCM ) viongozi wake wamekuwa wakiandaa mikakati ya
kuwanyonya watanzania wenye hali ya chini huku matajiri wakiendelea
kujineemesha.
Mgombea huyo wa
ACT Wazalendo alisema baada ya chama chake kuyabaini hayo, ndiyo maana
kimemsimamisha yeye ili aweze kuwakomboa wananchi ikiwemo kuboresha miundombinu
ya ukusanyaji kodi ikiwa ndio msingi mkuu wa maendeleo na kuondoa vitendo vya
rushwa na ufisadi, ambavyo hudumaza maendeleo ya taifa hili.
No comments:
Post a Comment