Na Julius
Konala,
Mbinga.
MGOMBEA udiwani
kupitia tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kata ya Mkako wilaya
ya Mbinga mkoani Ruvuma, Gabriel Mwinuka amesema kuwa endapo wananchi wa kata
hiyo watampa ridhaa ya kuwa mwakilishi wao, atahakikisha anapambana kutatua
matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii katika kata hiyo, ikiwemo ukosefu wa
maji safi na salama.
Mwinuka aliyasema
hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu, akielezea mipango na
mikakati yake mbalimbali, atakayoitekeleza katika kuwatumikia
wananchi pindi atakapochaguliwa kuwa Diwani wa kata hiyo.
Alisema kuwa kata
hiyo kwa muda mrefu imekuwa na tatizo la ukosefu wa huduma hiyo muhimu, katika
vijiji vya Mkako, Lihale na Kihuruku hali ambayo inawalazimu akina mama kutembea
umbali mrefu kufuata maji pamoja na kusababisha wananchi kuugua homa za
matumbo.
Alieleza kuwa,
yeye kwa kushirikiana na wananchi pamoja na viongozi wanaounda Umoja wa katiba
ya wananchi (UKAWA) watatatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa
kata hiyo, ikiwemo kuboresha miundombinu yote ya maji, barabara, ujenzi wa
nyumba za wahudumu wa afya na walimu.
Kadhalika alisema
katika uongozi wake, atahakikisha anaunganisha nguvu za wananchi na Halmashauri
katika kujenga kituo cha afya kwenye kata hiyo kwa madai kuwa wananchi wanapata
tabu ya kutembea umbali mrefu, kufuata huduma kwenye gereza la kitai pindi
wanapougua ambapo alisema wakati mwingine matatizo yanapotokea usiku hasa kwa
akina mama wajawazito inakuwa ni vigumu kupata huduma muhimu ya matibabu.
Mgombea huyo pia
alidai kuwa katika kipindi atakachokuwepo madarakani atahakikisha anajitahidi
kutatua changamoto ya muda mrefu, ya ujenzi wa daraja la mto
Ruvuma linalounganisha kijiji cha Lihale wilayani Mbinga na kijiji cha Lusonga
kilichopo katika wilaya ya Songea, kwa madai kuwa kukosekana kwa daraja hilo
kunawakwamisha wananchi kusafirisha mazao yao ya mahindi, kwa ajili ya kupeleka
kusaga unga kwenye kiwanda cha masista wa Chipole.
Mwinuka amewaomba
wananchi hao wamchague siku ya uchaguzi mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais
ifikapo Oktoba 25 mwaka huu ili akashirikiane na viongozi wanaounda Umoja wa
katiba ya wananchi (UKAWA) kwa malengo ya kuwatatulia matatizo yanayowakabili, ikiwa
pamoja na kufuta michango ya shule isiyo ya lazima pamoja na kuondoa vizuizi
ambavyo vimekuwa kero kwa wakulima wakati wa kusafirisha mazao yao kutoka
shambani.
No comments:
Post a Comment