Na Steven Augustino,
Tunduru.
WAKATI kampeni za Uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba
25 mwaka huu zikiendelea kushika kasi sehemu mbalimbali hapa nchini, mgombea
ubunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini kupitia tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF)
na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) Manjoro Kambili, amesema
ataendelea kujiwekea mikakati ya kuhakikisha kwamba anajipatia ushindi mnono na
kujinyakulia jimbo hilo, ili aweze kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Jimbo hilo kwa sasa mgombea huyo, anapambana na Mhandisi Ramo
Makani ambaye anapeperusha bendera kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hayo yamebainika kufuatia uchunguzi uliofanywa na mwandishi
wa habari hizi, ambapo taarifa zinaonesha kuwa Kambili amechukua maamuzi
hayo kutokana na kuwepo kwa mgogoro mkubwa miongoni mwa wanachama wa CCM ambao
unafukuta chini kwa chini, huku kukiwa na kundi kubwa lililoanza kujitokeza na
kumuunga mkono mgombea huyo wa UKAWA.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mgombea huyo wa Ukawa ameanza
kuyaita makundi hayo na kuzungumza nayo katika vikao vyake mbalimbali na
kufanya makubaliano, ambayo yatamhakikishia kuibuka na ushindi huo.
Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao, baadhi ya
viongozi wa makundi hayo ya Chama cha mapinduzi, walikiri hilo kufanyika na
kwamba wao wapo tayari kuzungumza na mgombea huyo huku wakiongeza kuwa wanachohitaji
awamu hii ni mabadiliko ya uongozi.
Walifafanua kuwa wapo tayari kuzungumza na mgombea
huyo wa upinzani kwa kile walichoeleza kuwa viongozi wa chama chao (CCM) wamekuwa
hawasikilizi na kutatua kero mbalimbali za wananchi wa Jimbo hilo, jambo ambalo
chama hicho kimetumia mabavu kumteua Mhandisi, Ramo Makani kuwa mgombea Tunduru
Kaskazini.
Kutokana hali hiyo hivi sasa mgombea huyo wa CCM, ameshindwa
kumaliza tofauti hizo ambazo zinaendelea kumtafuna kila kukicha, na sasa wanachama
wake wanasema wataendelea kumpuuza.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyoleta dhahama hiyo, ndani ya Chama
cha mapinduzi Mhandisi Ramo alitangazwa kuwa mshindi wa kwanza katika matokeo ya
uteuzi wa kuwania nafasi ya ubunge katika Jimbo la Tunduru Kaskazini, kwa
kupata kura 5,286 jambo ambalo liliwafanya wagombea wenzake kususia na
kutosaini, matokeo hayo yaliyompatia ushindi huo kwa madai kuwa aliyachakachua.
Wagombea wengine ambao walichuana na Mhandisi huyo ni Omary
Ajili Kalolo alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 3,957, Issa
Mohamed Mtuwa alishika nafasi ya tatu kwa kura 2,025, Rashid Mohamed Mandoa
kura 1,719, Athuman Salehe Nkinde kura 1,296, Shaban Richard Uronu kura
942, Hassan Zidadu Kungu kura 687, Michael Augustino Matomora kura 480, Moses
Ally Kaluwayo alishika nafasi ya mwisho kwa kupata kura 353.
No comments:
Post a Comment