Na Muhidin Amri,
Songea.
KATIBU wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoani
Ruvuma, Chiku Masanja amewataka wanawake wa mkoa huo, kuwaunga mkono wanawake
wenzao waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kupitia chama
hicho.
Alisema wanawake wakipata nafasi za uongozi, itakuwa rahisi
kwao kuwatetea wanawake wenzao katika vikao mbalimbali vya maamuzi hasa vile vya
baraza la madiwani, ubunge na kupata fursa ya kushiriki kikamilifu katika shughuli
ambazo zitawawezesha wajikwamue
kiuchumi.
Chiku aliyasema hayo jana, wakati alipokuwa
akizungumza na Jumuiya ya wanawake, kata ya Misufini Manispaa ya Songea mkoani
humo kwenye ukumbi wa CCM tawi la mjini, kwa lengo la kujadili masuala
mbalimbali ya maendeleo ya umoja wao sambamba na kuwakumbusha juu ya wajibu wa
kila mwanamke kushiriki kikamilifu kupiga kura katika uchaguzi mkuu, Oktoba 25
mwaka huu katika eneo lake analoishi.
Wanawake wakiwa viongozi ni wawakilishi muhimu wa wanawake
wenzao, na wanapokuwa kwenye vikao jukumu lao kubwa ni kuhakikisha maslahi ya
wanawake yanajadiliwa kwa upana wake, hasa ikizingatiwa kuwa mwanamke ni nguzo
kuu ya maendeleo.
Alieleza kuwa UWT inategemewa katika kufanikisha ushindi wa
chama tawala, hivyo kinachotakiwa ni kuhakikisha wanapita kwenye maeneo yao na
kuitisha mikutano, ambayo wataelezea kwa kina namna ambavyo serikali
inavyotekeleza majukumu yake.
"Wanawake ni watu muhimu kwa ushindi wa Chama
chetu, tumekusanyika hapa ili tukumbushane majukumu ya kila mmoja katika eneo
lake na kuhakikisha kwamba chama chetu kinashinda katika uchaguzi kwa ngazi ya
udiwani, ubunge na rais”, alisema Masanja.
Hata hivyo alisistiza juu ya umuhimu wa wanawake, kujitokeza
kwa wingi katika mikutano ya kampeni ya vyama vya siasa ili kusikiliza sera na
ahadi za wagombea wake, kwa lengo la kuwa na maamuzi sahihi siku ya kupiga kura
na kuwachagua wanawake wenzao walioomba nafasi za uongozi kupitia CCM ili
waweze kuchaguliwa.
No comments:
Post a Comment