Na Kassian Nyandindi,
OKTOBA 25 mwaka huu, ni siku maalum ambayo Watanzania
wataweka historia kubwa ya kuwachagua viongozi wao watakaoweza kuwaongoza
katika kipindi cha miaka mitano ambao ni diwani, mbunge na rais kwa kuvihusisha
vyama mbalimbali vya siasa ambavyo vimesajiliwa kisheria hapa nchini.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni chama ambacho kimeendelea
kuiongoza nchi hii, baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2010,
ambapo uchaguzi huo ulivishirikisha vyama vya upinzani au vyama rafiki kama
inavyoelezwa na baadhi ya makada wa chama.
Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini, Julai
2 mwaka 1992, CCM ni chama ambacho Watanzania wengi wanakiamini na kukichagua
kiendelee kushika dola kwa miaka mingi sasa.
Watanzania hao katika vipindi vyote vya chaguzi zilizopita,
waliamua kwa dhati kuwachagua wagombea waliotokana na chama hicho baada ya
kuridhishwa na sera zake, ambazo zinalenga kuwaletea maendeleo.
Katika makala haya Mwandishi wetu, anapenda kuelezea juu ya
nafasi ya Ubunge ni moja kati ya nafasi nyeti ambayo wananchi watakuwa na haki
ya kuchagua kama vile katiba ya nchi yetu inavyotaka, ambapo wakati ukifika
upigaji wa kura utafanyika katika majimbo mbalimbali ya uchaguzi na kupatikana
kiongozi ambaye atawaongoza wananchi wake katika eneo husika.
Kila chama cha siasa kimesimamisha mgombea wake, ambapo
mwananchi analojukumu moja tu la kumpigia kura yule anayemtaka wakilenga
kushirikiana naye, katika kuwaongoza na kuwaletea maendeleo.
Jimbo la Mbinga vijijini lililopo wilayani Mbinga mkoa wa
Ruvuma, ni moja kati ya majimbo ambayo yanapiganiwa kufa na kupona kwa
kuhakikisha linaongozwa na kada wake wa CCM, kwa nafasi hiyo ya ubunge.
Martin Msuha Mtonda ni mmoja kati ya wanachama wa Chama cha
mapinduzi ambaye anatikisa jimbo hilo, kwa kuhakikisha siku chache zilizobakia
kufikia siku uchaguzi mkuu anajinyakulia madaraka ya kuwaongoza wanambinga
vijijini, baada ya kumchagua kwa kura nyingi.
Msuha ambaye namfahamu vizuri ni kaka yangu wa karibu…………..amejiwekea mikakati kabambe ya utekelezaji wa maendeleo katika jimbo hilo pale
tu, wananchi watakapompatia ridhaa ya kuwaongoza.
Mahojiano yaliyofanywa kati ya mwandishi wa makala haya na
Msuha, anasema kwamba jimbo hilo tangu miaka mingi iliyopita lina wakulima
ambao ni wazalishaji wakubwa wa zao la kahawa, lakini hivi sasa uzalishaji wa
zao hilo umeporomoka kutokana na sababu mbalimbali.
Anasema anaamini kwamba kama atachaguliwa kuwa mwakilishi wao
Bungeni, atashirikiana na wakulima wa kahawa na wadau mbalimbali wa zao hilo
kuongeza uzalishaji wake, ili wananchi waweze kuondokana na ugumu wa maisha na
hatimaye wajikwamue kiuchumi.
Sambamba na kushirikiana na wakulima hao, pia atahakikisha
anahamasisha wakulima waweze kuendeleza kilimo cha zao hilo kwa kuanzisha
mashamba mapya ambayo watapanda aina mpya ya miche ya kahawa na haishambuliwi
na magonjwa kwa urahisi.
“Wananchi wa jimbo hili, ni wakulima maarufu kilimo cha
kahawa hivyo kama watanichagua hiyo Oktoba 25 ni muhimu kwangu kuwaongoza
ipasavyo, ili waweze kuwa na maendeleo hasa katika nyanja ya kilimo tofauti na
ilivyo sasa”, alisema Msuha.
Anasema kuna changamoto mbalimbali, ambazo wazalishaji wa zao
hilo wanakabiliana nazo hivyo kama mwakilishi wao atahakikisha anashirikiana
nao katika kuzikabili, kwa kuzipeleka sehemu husika serikalini na kuzisimamia
kikamilifu ili zifanyiwe kazi.
“Nitakapokuwa Mbunge nitahakikisha wataalamu wa kilimo
wanakuwa jirani na wakulima wangu, watoe elimu ya kutosha kwa wakulima juu ya
kuboresha zao hili ili uchumi ndani ya jimbo uweze kukua kwa sababu ndio zao
mama linalotegemewa kuingiza mapato makubwa ndani ya wilaya yetu ya Mbinga”,
anasema.
Kuhusiana na uzalishaji wa mazao mengine anasema kwamba,
atahamasisha wakulima wanazingatia maelekezo ya wataalamu ili waweze kuzalisha
kwa wingi hasa ikizingatiwa yapo mazao kama vile mahindi, ulezi na mengineyo
yamekuwa yakistawi vizuri jimboni humo.
Akielezea juu ya masoko ya mazao hayo, anasema kuwa kwa
upande wa kahawa atajitahidi pia kuhamasisha soko la ndani na lile la nje
atashirikiana na serikali kupitia wataalamu husika, ili waweze kupata masoko
yenye bei nzuri ambayo mkulima atanufaika baada ya kuuza kahawa yake.
Katika hilo anaongeza kuwa, atahamasisha uanzishwaji wa vyama
vya akiba na mikopo (SACCOS) ili wakulima waweze kupata mikopo kwa riba nafuu
badala ya kutegemea taasisi za kifedha kama vile benki, ambayo kwa kawaida riba
yake huwa ni kubwa.
Vilevile atahakikisha anaweka utaratibu wa kushirikiana na
wananchi atakaowaongoza, waanzishe vikundi vya ujasiriamali jambo ambalo
litasaidia kuaminiwa na taasisi hizo za kifedha na hivyo kukopesheka kwa
urahisi.
Kwa mazao mchanganyiko atahakikisha anarahisisha upatikanaji
wa pembejeo za kilimo, ambazo kwa sasa imekuwa vigumu kwa wakulima wadogo
kumudu kununua kutokana na bei kuwa ghali.
Msuha anaelezea pia kwa upande wa elimu, afya, maji na
miundombinu ya barabara atashirikiana na wananchi wake, kuboresha sekta hizo
muhimu huku akieleza kuwa pasipokuzipatia kipaumbele kamwe maendeleo ya kweli
hayawezi kupatikana.
Anasisitiza kuwa miundombinu ya barabara, katika baadhi ya
maeneo jimboni humo ni mibovu na wananchi hupata shida ya kusafirisha mazao yao
ambapo wakati mwingine huwawia vigumu nyakati za masika, hasa pale
wanapomsafirisha mgonjwa kwenda Hospitali ya wilaya kwa ajili ya kupatiwa
matibabu vyombo vya usafiri hukwama barabarani kwa muda mrefu, na kusababisha
mgonjwa kupoteza maisha.
Msuha ambaye ni mwajiriwa wa Wizara ya afya na ustawi wa
jamii, anasema ukiwa kiongozi ni lazima utekeleze majukumu ya wananchi
ipasavyo, hivyo yeye binafsi atakuwa pia akisikiliza kero za wananchi na
kuzitafutia majawabu kwa kuwashirikisha wao wenyewe na pale itakaposhindikana,
ndipo atatafuta wafadhili wa aina mbalimbali ili waweze kusaidia.
Anasema kuwa pamoja na kuajiriwa katika Wizara hiyo, pia ni
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Msingwa uliopo katika kata ya Msigani wilaya
ya Kinondoni mkoa wa Dar es Salaam, hivyo anaimani kubwa na wananchi wa jimbo
hilo kwamba ataibuka na ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu ujao.
Pia anabainisha kuwa atakuwa karibu na wananchi wake, kwa
kufanya vikao vya mara kwa mara kabla na baada ya vikao vya bunge, ili kupata
maoni ya wapiga kura wake na aweze kuyafanyia kazi.
Anasema jimbo la Mbinga vijijini, lina fursa nzuri ya
kuharakisha maendeleo na uchumi kwa ujumla hasa ikizingatiwa kuwa jimbo hilo,
linamazingira mazuri ya ardhi yenye rutuba na kama yatafanyiwa kazi ipasavyo
vipato vya wananchi vitaongezeka.
Anasisitiza, wananchi wanalojukumu la kubadilisha mtazamo wao
ili waweze kufikia kiu ya maendeleo waliyonayo sasa na kuondokana na umaskini
kitendo ambacho kinahitaji kiongozi makini, msomi na shupavu.
Msuha anasema kuwa kinachotakiwa hapa ni mwananchi kuwa
makini, kwa kuwachagua viongozi ambao watawapa maendeleo ya kweli na
wajihadhari na wagombea ambao, wanamawazo ya kutumia fedha ili kununua uongozi.
Anasema kuwa kumchagua mgombea kwa sababu ya fedha alizonazo
huku uwezo wa kuongoza wananchi ni mdogo, haileti maana badala yake watajuta
kwa kipindi chote cha miaka mitano huku mwakilishi wao akijilimbikizia mali.
Akizungumzia juu ya Chama chake cha mapinduzi, anasema yeye
anatambua wazi kuwa ni mwanachama halali wa CCM hivyo kama atachaguliwa kuwa
mbunge atahakikisha anarejesha matunda kwa chama chake, ambapo kwa kushirikiana
na wanachama kila tawi litapaswa kuwa na Ofisi yake ya tawi.
“Nilichokibaini katika jimbo la Mbinga vijijini, hakuna Ofisi
za matawi hivyo wajibu wangu nitahakikisha nashiriki kikamilifu katika ujenzi
wa ofisi za matawi, kata na hata kuboresha ofisi ya wilaya ambayo nayo kimsingi
inauchakavu mkubwa wa majengo”, anasema Msuha.
Hata hivyo, anawaasa wananchi wa jimbo hilo kuwa makini
ifikapo, Oktoba 25 mwaka huu wamchague kwa kura nyingi, ili aweze kutimiza kiu
yake ya kuwaletea maendeleo wanambinga vijijini na kuondokana na adha
wanayoipata sasa.
No comments:
Post a Comment