Na Muhidin Amri,
Songea.
MKURUGENZI mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Songea
vijijini mkoani Ruvuma, Sixbert Kaijage amewataka Wauguzi wanaofanya kazi ndani
ya halmashauri hiyo kujituma na kutekeleza majukumu ya kazi zao ipasavyo,
ili waweze kuboresha huduma husika kwa jamii, jambo ambalo litawafanya waweze
kuepukana na malalamiko yasiyokuwa ya lazima.
Alisema kufanya hivyo kutasaidia wilaya hiyo, kusonga
mbele kimaendeleo kwa haraka zaidi, na wananchi kufanya shughuli zao wakiwa na
afya nzuri.
Kaijage alisema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa katika
kijiji cha Lundusi, mji mdogo wa Peramiho, wakati alipokuwa akizungumza na
wakazi wa kijiji cha Maposeni wilayani humo kuhusiana na serikali
ilivyojipanga kukabiliana na changamoto mbalimbali, za kiutendaji kwa watumishi
wa halmashauri hiyo.
Alisema halmashauri yake inatambua kuwa wauguzi
wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, baada ya watumishi hao kuhamia
katika mji huo kutokana na kukosekana kwa vituo vingi vya kutolea huduma ya afya
na nyumba za kuishi, hata hivyo wamejipanga kukabiliana na tatizo
hilo kwa kufanya ujenzi na kuongeza bajeti ambayo itawezesha kununua dawa
na vifaa.
Mbali na hilo Kaijage alisema, serikali inatambua
changamoto hizo hivyo itaendelea kuyashughulikia na kuyapatia ufumbuzi ili
kuleta hamasa ya utendaji wa kazi kwa watumishi hao.
Aliongeza kuwa, mkakati wa kwanza wataimarisha miundombinu
ya maji, barabara pamoja na umeme katika halmashauri ya Songea vijijini, ili watumishi
waweze kuwa na mazingira mazuri ya kufanyia kazi na kupenda kuishi katika mji
huo wa Peramiho.
Kutokana na hilo alisema, tayari wamempata mkandarasi
ambaye ataanza kujenga barabara za mji huo kwa kiwango cha lami ambapo
awali wataanza ujenzi wa kilometa saba, itakayoanzia makutano ya Ofisi za
halmashauri hadi hospitali ya Mtakatifu Joseph Peramiho na nyingine
itakayoelekea chuo cha madakatari, kilichopo katika kijiji cha Morogoro wilayani
humo.
No comments:
Post a Comment