Na Steven Augustino,
Tunduru.
ASKARI ambao watashiriki katika jukumu la kulinda amani na
utulivu, siku utakapofanyika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu, wametakiwa
kupunguza matumizi ya nguvu zisizokuwa za lazima katika uchaguzi huo.
Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Nicolaus
Mwakasanga alisema hayo alipokuwa akifungua juzi mafunzo elekezi yaliyoshirikisha
askari polisi, magereza, uhamiaji na mgambo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa
Hospitali ya wilaya hiyo mjini hapa.
Mwakasanga alisema kuwa lengo la mafunzo hayo, ni kuweza
kufanikisha na kuhakikisha kwamba uchaguzi huo unakwenda salama.
"Sisi ni
walinzi, inatupasa tuwe wavumilivu na wastahimilivu wakati wa kutekeleza
majukumu yetu, tuache kutumia nguvu kubwa pale ambapo hakuna sababu ya msingi",
alisisitiza Mwakasanga.
Alisema katika kikao hicho askari hao, watapewa maelekezo
muhimu watakayotakiwa kuyafuata wakati uchaguzi mkuu utakapofanyika.
Kamanda huyo wa Polisi alifafanua kuwa baadhi ya mambo muhimu
watakayotakiwa kuyafuata katika utekekelzaji wa zoezi hilo kwamba, askari hao
watajengewa uwezo katika masuala ya usimamizi wa haki za binadamu, utatuzi wa
migogoro kabla haijatokea, masuala ya jinsia na utekelezaji wa majukumu yao
wakati wa uchaguzi.
Wakifafanua kwa nyakati tofauti wakufunzi wa mafunzo hayo, Inspekta
Joseph Malongo na Anosisye Mwaipopo walisema kuwa asilimia 90 ya utekelezaji wa
majukumu ya Polisi, wengi wao hufanya vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu
hivyo aliwataka kuachana na vitendo hivyo na kuzingatia sheria husika na sio vinginevyo.
No comments:
Post a Comment