Na Muhidin Amri,
Mbinga.
MGOMBEA ubunge wa
Jimbo la Mbinga mjini, kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Sixtus Mapunda
amewataka wananchi wa jimbo hilo kukipa ushindi mkubwa chama hicho na wagombea
wake wa udiwani, ubunge na urais ili kiweze kutimiza ndoto yake ya maisha bora,
kwa kila mtanzania.
Mapunda ambaye
pia ni Katibu mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama hicho taifa (UVCCM) alisema hayo
hivi karibuni, katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya
soko kuu Mbinga mjini na kusisitiza kuwa CCM ndicho chama chenye sera nzuri na
mipango madhubuti ya kimaendeleo.
Amewaomba wakazi
wa mji huo, kumchagua kwa kura nyingi Oktoba 25 mwaka huu ili aweze kutimiza
ndoto yake ya kimaendeleo na kuleta matumaini mapya kwa wananchi na chama kwa
ujumla, hasa kwa wale walioanza kukata tamaa na vitendo vya ufisadi vilivyokuwa
vinafanywa na baadhi ya makada wake ambao wamekimbilia vyama vya upinzani,
baada ya kuona hawana sifa ya kubaki ndani ya chama hicho.
Mapunda
alifafanua kuwa yeye na Chama cha mapinduzi, wanafahamu changamoto
zinazowakabili watu wa Mbinga hata hivyo tayari serikali ya CCM imeshaanza
kuzipatia majibu huku akitolea mfano wa kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya
lami kutoka Songea hadi Mbinga, yenye urefu wa kilometa 96 ambayo imejengwa na
serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na nchi ya Marekani.
Katika
Mkutano huo wa kampeni pia wanachama 20 kutoka CHADEMA, ACT Wazalendo
na Chama cha wananchi CUF walirudisha kadi za vyama hivyo na kujiunga na Chama
cha mapinduzi, ambapo Mapunda aliwataka wananchi kutokubali kufuata propaganda
zinazotolewa na vyama hivyo, kwa kuwa zinalenga kuhamasisha kuleta vurugu
na uvunjifu wa amani hapa nchini.
Mbali na hilo, amewataka wananchi wa Mbinga na Tanzania kwa ujumla kuacha mawazo ya kumpigia kura mgombea urais wa Ukawa ambaye anaungwa mkono na vyama vingine vya upinzani, Edward Lowassa kwa sababu kama atakuwa Rais hawezi kuwaletea maendeleo kwani kila anapokuwa katika mikutano yake ya kampeni, amekuwa ni mtu wa kutoa ahadi nyingi za uongo na zisizotekelezeka badala yake ataangalia jinsi ya kurudisha fedha anazotumia kuwahonga baadhi ya wanachama wa CCM ili wahamie katika vyama vya upinzani.
Mapunda alisema kiongozi mzuri wa siasa ni yule ambaye hatoi ahadi za uongo kwa wapiga kura wake, bali ni mwenye uwezo na anayejua kero mbalimbali za wananchi ili aweze kuzitatua na kuleta maendeleo katika eneo husika, kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
No comments:
Post a Comment