Mlemavu asiyeeona akisoma mfano wa karatasi ya kupigia kura, wakati wa mkutano kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Watu wenye ulemavu. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
JUMLA ya vituo 216 vimetengwa katika jimbo la Peramiho,
lililopo katika Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kwa ajili ya
kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba, 25 mwaka
huu.
Akizungumza na mwandishi wetu, kwa niaba ya msimamizi mkuu wa
uchaguzi wa jimbo hilo Sixbert Valentine, Ofisa uchaguzi wa Halmashauri ya
wilaya ya Songea Furaha Mwangakala, alisema kuwa maandalizi kwa ajili ya
uchaguzi huo yamekamilika.
Mwangakala alifafanua kuwa katika kila kituo ndani ya Jimbo
hilo, kutakuwa na wapiga kura 450 kwa lengo la kupunguza msongamano na kutoa
fursa kwa wananchi wote ambao wamejiandikisha, waweze kupiga kura bila kupata usumbufu
wa aina yoyote ile.
Alisema kuwa, kufuatia zoezi hilo jumla ya watu 67,334 kwa Jimbo
la Peramiho wenye sifa ya kupiga kura wamejiandikisha, miongoni mwao yakiwemo
makundi mbalimbali ya wazee, vijana, wanawake kwa wanaume ili waweze kutumia
haki yao ya msingi kuwachagua viongozi wao.
Kwa upande wa maandalizi alieleza kuwa yanaendelea vizuri kwa
madai kuwa mpaka sasa jumla ya wasimamizi wa uchaguzi 800 wameteuliwa, maboksi
ya nyongeza yenye rangi ya bluu 40, meusi 40 na meupe 40 tayari yamekwisha pokelewa
kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Ofisa uchaguzi huyo aliendelea kuvitaja vifaa vingine
vilivyowasili kuwa ni mabango ya hadhari, mabango ya vituo, mabango ya mshale, nyembe
za kukatia lakili, betrii za taa, vitabu vya maelekezo kwa watakaosimamia
uchaguzi pamoja na fomu kwa ajili ya mafunzo ya wasimamizi wa vituo na
makarani.
Mwangakala aliongeza kuwa kwa upande wa makundi
maalumu hususan kwa watu wasioona, tayari wamekwisha waandalia
karatasi zao maalumu za kupigia kura pamoja na kuwatengenezea utaratibu mzuri,
ambapo pia kundi hilo likiwemo la wazee na walemavu wengine wa aina
mbalimbali, akina mama wajawazito nao hawatasimama kwa muda mrefu kupiga kura
badala yake watapewa kipaumbele kwanza na wengine watafuata kutekeleza zoezi
hilo muhimu.
Hata hivyo baadhi ya wananchi wakizungumza kwa nyakati
tofauti, walieleza kuwa wanashindwa kuelewa kauli mbalimbali
zinazotolewa na viongozi wa vyama ambapo wanawaambia
wafuasi wao kuwa wakipiga kura lazima wazilinde, huku sheria ya tume inasema kuwa
ukisha piga kura unatakiwa usimame umbali wa mita
100 na vyombo vya dola vinasema ukipiga kura unatakiwa kurudi
nyumbani ili kusubiri matokeo, jambo ambalo walisema kuwa wanapaswa kuelimishwa
ipasavyo kupitia vyombo vya habari na pale mikutano ya kampeni inapofanyika.
No comments:
Post a Comment