Na Muhidin Amri,
Namtumbo.
MGOMBEA nafasi ya ubunge Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma, kwa
tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhandisi Edwin Ngonyani, amewakumbusha
wananchi wa jimbo hilo, kutunza shahada zao za kupigia kura na kuchagua viongozi
watakaowaletea maendeleo.
Aidha amewataka kuwakataa wagombea wanaotumia kiasi kikubwa
cha fedha kuwahonga wapiga kura, ili waweze kuwachagua katika uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Ngonyani alisema kitendo hicho ni cha aibu na fedheha, hivyo
kiongozi anayepatikana kwa mfumo huo akishachaguliwa hushindwa kutimiza ahadi alizotoa
kwa wananchi wake, badala yake hutumia nafasi yake aliyonayo kuliingiza Taifa
kwenye matatizo makubwa na kuwafanya wananchi anaowaongoza kuwa maskini.
Hayo yalisemwa na mgombea huyo, alipokuwa akizungumza na
wananchi wa kijiji cha Utwango kata ya Namabengo wilayani humo katika mkutano
wake wa kampeni huku akisisitiza kwa kuwataka wananchi kuendelea na utamaduni
wa kuheshimiana, kupendana na kuacha kubaguana kwa misingi ya itikadi ya dini au
siasa.
Ngonyani alisema kwamba, iwapo atachaguliwa kuwa mbunge wa Namtumbo atatumia uwezo na elimu aliyonayo kuhakikisha mgodi wa madini ya Uranium uliopo mto Mkuju katika pori la Selou,
unasaidia kutoa ajira kwa kundi kubwa la vijana na wanawake wa wilaya hiyo,
badala ya kuwanufaisha watu kutoka maeneo mengine.
No comments:
Post a Comment