Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
YAKIWA yamebaki masaa machache Watanzania kushiriki katika kinyang’anyiro
cha uchaguzi mkuu, Serikali mkoani Ruvuma imewataka wananchi wake mkoani humo,
Oktoba 25 mwaka huu kushiriki kikamilifu kupiga kura katika kituo husika
walichojiandikisha na mara baada ya kukamilisha zoezi hilo, waondoke na kurudi
nyumbani.
Mkuu wa mkoa huo, Said Mwambungu alisema hayo leo alipokuwa
akizungumza na madereva wa pikipiki maarufu kwa jina la Yeboyebo, katika ukumbi
wa Songea Club uliopo mjini hapa.
“Nawasihi sana, mkisha piga kura ondokeni katika eneo la
kituo na kuwaacha mawakala wa vyama husika wakilinda kura zenu”, alisema
Mwambungu.
Aidha Mwambungu aliwasihi madereva hao, wasikubali kutumiwa
vibaya na wanasiasa kwa kufanya matendo maovu au vurugu, siku uchaguzi mkuu
utakapofanyika.
“Msikubali kutumika na hiyo ndiyo rai yangu kwenu, nawaomba
kapigeni kura kwa utulivu, waepukeni wanasiasa wenye nia ovu ambao hawalitakii
mema Taifa hili”, alisema.
Aliongeza kuwa serikali ina mkono mrefu, hivyo kila wakati
imekuwa ikitambua nini kinafanyika na kuchukua hatua haraka iwezekanavyo, kwa
lengo la kuepusha vurugu na kulinda amani na utulivu kwa raia wake.
Hata hivyo kwa upande wao, madereva hao wa pikipiki kwa
nyakati tofauti walimthibitishia Mkuu huyo wa mkoa kwamba, watazingatia
maelekezo aliyowapa na kuhakikisha hakuna vurugu itakayotokea.
No comments:
Post a Comment