Na Mwandishi wetu,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani
Ruvuma, kwa kushirikiana na askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ)
wamefanikiwa kuharibu mabomu mawili, yaliyokutwa katika Kijiji cha
Ngwinde kata ya Litola, wilayani Namtumbo mkoani humo.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Revocutus Malimi alisema kuwa mabomu hayo yaliharibiwa ili yasiweze kuleta madhara katika jamii, ambapo moja liliharibiwa majira ya saa nne asubuhi na la pili saa sita mchana.
Alisema kuwa
katika mabomu hayo, moja lilikuwa aina ya Motor lenye ukubwa wa mm. 82 ambalo
lilikutwa chini ya mti na la pili ni la kurusha kwa Roketi (RPG) lenye
ukubwa wa mm. 122 ambalo lilichimbiwa chini ya ardhi.
Alifafanua kuwa Jeshi
hilo, lilipata taarifa kutoka kwa viongozi wa kijiji cha Ngwinde kwamba kuna
vyuma vimeonekana katika kijiji hicho na wanamashaka kwamba, huenda yakawa ni
mabomu.
Kamanda Malimi alisema siku iliyofuata baada ya kupokea taarifa hiyo, Polisi kwa kushirikiana na askari wa JWTZ, walifika katika eneo la tukio na kuyakuta mabomu hayo mawili ambayo yalikuwa katika kijiji hicho.
Malimi alibainisha kwamba, katika uchunguzi wa awali walibaini kuwa eneo walipoyakuta mabomu hayo ni sehemu ambayo ilikuwa ikitumika kwa ajili ya mazoezi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, pamoja na vikosi vingine vya ulinzi na usalama kutoka makao makuu ya Brigedi ya 401 Songea miaka ya nyuma na mpaka mwaka 2012, na kwamba ufuatiliaji wa karibu utafanyika ili kuweza kuona kama kuna masalia mengine ya mabomu.
Kamanda Malimi amewataka wananchi wa mkoa wa Ruvuma, kuendelea kuwa na moyo wa kutoa taarifa juu ya vitu wanavyovitilia mashaka kwenye maeneo yao na kuwajulisha viongozi wao, wa mitaa na vijiji ikiwemo hata kutoa taarifa katika vituo vya Polisi.
No comments:
Post a Comment