Monday, October 26, 2015

CCM MBINGA YAIBUKA KIDEDEA MATOKEO YA UCHAGUZI YATANGAZWA



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kimeibuka kidedea baada ya wagombea wake kwa nafasi ya diwani, ubunge na rais kuongoza kwa kura nyingi katika vituo vyake vya kupigia kura.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu umebaini kuwa Jimbo la Mbinga mjini na vijijini uchaguzi ulifanyika kwa amani na utulivu, huku wananchi ambao ni wapiga kura wakijitokeza kwa wingi kupiga kura katika vituo husika.

Matokeo yametangazwa leo majira ya mchana, katika kituo cha utafiti wa zao la kahawa TaCRI – Ugano kilichopo Mbinga mjini ambako Wakurugenzi wa Tume ya uchaguzi katika majimbo hayo, waliweka kambi huko wakifanya kazi ya kujumlisha matokeo ya wagombea.

Akitangaza matokeo kwa jimbo la Mbinga mjini, Mkurugenzi msimamizi wa uchaguzi Oscar Yapesa alisema kuwa jimbo hilo lina idadi ya wapiga kura 61,833 likiwa na kata 19 na vituo vya kupigia kura 165 na kwamba waliojitokeza kupiga kura walikuwa 42,706, kura halali 41,442.


Katika jimbo hilo, mgombea Sixtus Mapunda kupitia tiketi ya CCM aliibuka kuwa mshindi nafasi ya ubunge kwa kupata kura 28,364 ikiwa ni sawa na asilimia 68 akifuatiwa na mpinzani wake, Mario Millinga  wa tiketi ya chama cha NCCR Mageuzi aliyepata kura 13,102 sawa na asilimia 32.

Vilevile kwa upande wa jimbo la Mbinga vijijini, Mkurugenzi msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Venance Mwamengo  naye alimtangaza nafasi ya ubunge, Martin Msuha wa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi kuwa mshindi ambaye aliongoza kwa kura 59,269 sawa na asilimia 84 akifuatiwa na Benjamin Akitanda wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) aliyepata kura 11,285 sawa na asilimia 16.

Mwamengo alisema kuwa jimbo hilo lina idadi ya wapiga kura 110,468 kata 29 vituo vya kupigia kura 312 ambapo waliopiga kura ni 72,436, kura halali zilikuwa 70,393 na zilizoharibika 1,846.

Kwa nafasi ya udiwani kata nyingi za majimbo hayo mawili zimechukuliwa na CCM, ambapo kwa upande wa vyama vya UKAWA jimbo la Mbinga vijijini CHADEMA kimenyakua kiti kimoja kwa nafasi hiyo na jimbo la mjini wamepata pia viti viwili.

Pamoja na mambo mengine, wakurugenzi hao mara baada ya kutangaza matokeo hayo walisema kuwa kwa nafasi ya rais wao hawana mamlaka ya kutangaza badala yake, wanayapeleka katika ngazi husika ili yaweze kutangazwa.

mgombea wa CHADEMA, Akitanda aliibuka na kupinga matokeo hayo kwa kil alichodai kuwa uchaguzi huo katika jimbo la Mbinga vijijini ulikiukwa kwa kutofuatwa taratibu za msingi.

Akitanda alilalamika akisema kuwa hata wafuasi wa CCM, wakati wa kampeni za uchaguzi walikuwa wakitumika kushusha bendera na mabango ya CHADEMA huku wengine wakipita katika jimbo hilo, kutoa rushwa ya fedha kwa wapiga kura.

“Kimsingi ninasema siridhiki na matokeo haya, nitakwenda kwenye vyombo vya kisheria hata Mahakamani ili haki iweze kupatikana”, alisema Akitanda.
 

No comments: