Friday, October 2, 2015

NALICHO: PELEKENI WATOTO WENU WA KIUME WAKAPATE HUDUMA YA TOHARA TABIBU


Baadhi ya wananchi wa mkoa wa Ruvuma, wakiongozwa na wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi na sekondari wakishiriki katika maandamano wakati wa uzinduzi wa tohara kwa wanaume, yaliyofanyika wilayani Mbinga mkoani humo.


Mfanyakazi kutoka Wizara ya afya, Asha Aman upande wa kushoto akitoa elimu kwa wakazi wa mji wa Mbinga kuhusu umuhimu wa kufanyiwa tohara, katika viwanja vya Taifa vya CCM mjini hapa.
Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

WAZAZI mkoani Ruvuma, wamehimizwa kupeleka watoto wao wa kiume katika vituo vya afya ili waweze kupatiwa huduma ya tohara tabibu, ambayo hutolewa bure ikiwa ni lengo la kusaidia kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi.

Vituo ambavyo vinatoa huduma hiyo bure mkoani humo, ni vile vya serikali ambapo ni hospitali ya wilaya ya Songea, Madaba, Tunduru, Nyasa na Mbinga.

Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Namtumbo, Chande Nalicho alipokuwa akizungumza katika uzinduzi rasmi wa mpango wa huduma ya tohara ya kitabibu kwa wanaume mkoa wa Ruvuma, iliyozinduliwa wilayani Mbinga mkoani humo katika uwanja wa Taifa mjini hapa.

Nalicho ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo za uzinduzi akimwakilisha Mkuu wa mkoa huo, Thabit Mwambungu alisema kuwa lengo la serikali kutoa huduma hiyo pia inazuia tatizo la maambukizi ya kansa ya shingo ya kizazi kwa mwanamke, endapo mwenza wake atakuwa amefanyiwa tohara.


“Nitoe maagizo kwa wazazi wa mkoa huu, tusiwakataze watoto wetu kwenda kufanyiwa tohara, uzinduzi ambao leo unafanyika hapa Mbinga ni chachu kwa wanaume wote ambao hawajafanyiwa tohara kujitokeza kwa wingi kwenda kupatiwa huduma hii, imekuwa ikichangia kuzuia maambukizi ya magonjwa mbalimbali, 

“Napata faraja kwamba hapa Mbinga mjini, tayari watu 400 wamejitokeza na wengine wanaendelea kuitikia wito juu ya zoezi hili, hasa kwa watoto wetu wadogo wenye umri kuanzia miaka kumi na kuendelea”, alisema Nalicho.

Katika mkoa wa Ruvuma, alisema kuwa ifikiapo mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu, wamejiwekea malengo ya kuwafikia wanaume 33,000 ambao watafanyiwa tohara tabibu, ndani ya mkoa huo.

Pamoja na mambo mengine, akitoa maelezo mafupi kwa niaba ya wataalamu kutoka Wizara ya afya, shirika la walter read kupitia mpango wa kudhibiti ukimwi, Dokta Jackson Gissenge alisema kuwa zoezi hilo linatekelezwa katika Nyanda za juu kusini, kwa kipindi cha miaka kumi ili kuweza kufikia malengo husika.

Gissenge alieleza kuwa ni muhimu kupambana na maambukizi mapya ya ukimwi, huku akiongeza kuwa tohara, inachangia kupunguza kwa asilimia 60 maambukizi ya ugonjwa huo.


No comments: