Friday, October 9, 2015

DED TUNDURU ACHUKIZWA WANANCHI KUUZIWA MAENEO YA MAKABURI

Na Steven Augustino,
Tunduru.

HALMASHAURI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, imewataka wananchi wake kuzingatia taratibu husika, hasa pale wanapohitaji kununua maeneo ya viwanja kwa ajili ya kujenga nyumba au kuweka makazi yao ya kudumu.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo, Tinna Sekambo alitoa rai hiyo Ofisini kwake alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu, na akatumia nafasi hiyo kuwataka kutoa ushirikiano pale wanapoona wanatapeliwa na wajanja wachache ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Sekambo alifafanu kuwa, tahadhali hiyo ameitoa kufuatia kuwepo kwa taarifa za kuibuka kwa kundi la matapeli wilayani humo, ambao wamekuwa wakiwauzia watu viwanja na kuwapatia hati bandia.

Alisema kufutia hali hiyo, Ofisi yake inafanya uchunguzi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuweza kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria haraka iwezekanavyo, kabla ya wananchi hawajapata hasara kubwa.


Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, alisema waliokuwa watumishi wa idara ya ardhi wilayani humo (Majina unanyo) ambao kwa sasa wamestaafu, baadhi yao wanadaiwa kuhusika na utapeli huo.

Aidha katika taarifa hiyo, Mkurugenzi huyo alidai kupokea malalamiko 10 kutoka kwa wananchi waliotapeliwa na kuuziwa viwanja vya makazi, katika maeneo ambayo ramani inaonyesha yametengwa, kwa ajili ya makaburi ya kuzikia.

Sambamba na kuingiliwa kwa maeneo ya makaburi, pia zoezi hilo limeathiri maeneo ya viwanja vya kucheza watoto jambo lililoisukuma Hamashauri yake kuwaandikia barua ya kuwazuia, wasiendelee na ujenzi katika maeneo hayo na akatumia nafasi hiyo kuwataka watu wote walionunua viwanja kupitia utaratibu huo, kwenda kufuatilia uhalali wa viwanja vyao kwa maafisa wa idara husika ya ardhi.

Kufuatia hali hiyo alieleza kuwa Halmashauri, imeanzisha utaratibu wa kuzuia watu wote ambao wamekuwa wakijenga nyumba bila vibali, kutoka kwa maafisa mipango miji ikiwemo pamoja na kupitishiwa ramani zao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wahanga wa utapeli huo walisema kuwa mbali na kukiri kutumia madalali wakati wananunua viwanja hivyo, walisema inaonesha kwamba mchezo huo mchafu, kwa kiasi kikubwa umekuwa ukifanywa na maafisa ardhi ambao sio waaminifu.

Kinachowafanya kuthibitisha hilo, walisema kinatokana na baadhi yao kupelekewa hati za ardhi na baadhi ya vibarua ambao hutumiwa na maafisa hao, katika kazi zao za upimaji viwanja mji wa Tunduru.

Walisema pamoja na uthibitisho huo, pia hati hizo huambatanishwa na stakabadhi halali ya serikali, huku hati hizo zikiwa na saini za maafisa wa idara hiyo.

No comments: