Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
WANAFUNZI wanaohitimu masomo ya kidato cha nne wilaya ya
Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameshauriwa kutojiingiza kwenye masuala ya anasa kama
vile vitendo vya kimapenzi, ambavyo husababisha kukatisha ndoto ya kujiendeleza
kimasomo katika maisha yao.
Aidha wakati wote wametakiwa kuonesha dhamira ya kusonga mbele, kwa kujikita zaidi kwenye malengo ya kuongeza elimu kwa faida
ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Ushauri huo ulitolewa jana na Khalid Kingi, ambaye ni Katibu
msaidizi wa Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi Taifa (UVCCM) katika mahafali
ya kidato cha nne shule ya sekondari Agustivo iliyopo mjini hapa, ambapo katika
sherehe hizo alikuwa akimwakilisha mgeni rasmi Katibu Mkuu UVCCM Taifa, Sixtus
Mapunda.
“Ndugu zangu mnahitimu masomo yenu katika kipindi ambacho
kina changamoto nyingi, natoa wito kwenu na kwa wengine hapa wilayani ambao
wanahitimu kidato cha nne kama ninyi, huko muendako mkapambane na changamoto za
ulimwengu huu kwa kuweka malengo ya kuongeza elimu, na kuacha tabia ya
kufikiria maisha ya mtaani ambayo yatawafanya mwisho wa siku mjiingize kwenye
makundi mabaya”, alisema Kingi.
Pia alipongeza safari za mafunzo kwa vitendo ndani na nje ya mkoa
wa Ruvuma, kwa watoto wanaosoma katika shule hiyo, ambayo yamekuwa yakiwajengea
uwezo na kuwafanya waweze kufanya vizuri katika masomo yao na mitihani kwa
ujumla.
Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya shule, Makamu mkuu wa
shule hiyo Thomas Komba alisema kuwa maendeleo kitaaluma matokeo ya mitihani ya
ndani na nje ya wilaya, imekuwa ikileta taswira nzuri ya ufaulu ambapo umekuwa
mkubwa kimkoa na Taifa kwa ujumla.
Komba alieleza kuwa matokeo ya mitihani mbalimbali,
imeendelea kutia hamasa na kuonesha tumaini bora kwa wanafunzi, wazazi na walezi.
Changamoto wanazokabiliana nazo shuleni hapo, Komba alizitaja
kuwa ni upungufu wa vifaa vya maabara kwa masomo ya sayansi, vitabu vya kiada
na ziada pamoja na uzio kuzunguka eneo la shule kitendo ambacho kinasababisha
baadhi ya wanafunzi kutoroka na kuelekea nje ya eneo la shule, jambo ambalo
huchangia kushuka kwa taaluma na nidhamu.
Hata hivyo changamoto nyingine, alisema kuwa baadhi ya wazazi
kutoshiriki kikamilifu na walimu hasa kwa upande wa ufuatiliaji maendeleo ya
kitaaluma na nidhamu kwa watoto wao, badala yake wamekuwa wakiwaachia walimu
pekee mzigo mkubwa wa kuwalea watoto hao.
No comments:
Post a Comment